SIO ZENGWE: Nchi inapokubaliana kuwa Kigonya alikosa

Tuesday January 18 2022
kigonya pic
By Angetile Osiah

KITENDO alichofanya kipa wa Azam, Mathias Kigonya kuufuata hewani mpira kuudaka na baadaye kurudisha chini mguu aliouonyoosha kutafutia nguvu za kuruka na kuonekana umemgonga Sakho, ndio lilitawala wiki ya kilele cha mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Ukiangalia video ya lile tukio, unaona jinsi kipa huyo Mganda alivyokuwa akianza kuruka huku mshambuliaji huyo wa Simba akiwa kama hatua nne mbele.

Ni dhahiri kuwa mwili umeumbwa hivyo. Unapoanza kuruka kuufuata mpira mbele ni tofauti na unaporuka kuufuata mpira unaokuja juu ya utosi. Ili kupata uwezo wa kuruka, ni lazima utatanguiliza mguu mbele na unapofikia mwisho, ule mguu hauwezi kubakia huko juu. Ni lazima uushushe ili uweze kutua vizuri.

Na ni wazi kuwa Sakho alikuwa katika kasi hivyo ama angemkwepa kipa au kwenda kumgonga kwa kuwa hakuwa tena na uwezo wa kuufikia mpira. Kwa ujanja alikwenda kuingia uvunguni kwa mguu ambao ulitakiwa kushuka na inawezekana aliguswa au hakuguswa na hivyo kuigiza kuwa ameumizwa.

Kwa tafsiri yake, refa aliona kipa aliingiliwa lakini katika kujitetea akamuumiza Sakho na hivyo akatoa kadi ya njano kwa Kigonya na kuamuru penalti.

Uamuzi huo ulitafsiriwa kuwa mbovu na takriban kila mtu aliyeshuhudia tukio hilo. Kila mtu anamshambulia refa kuwa alitakiwa kutoa kadi nyekundu eti kwa kuwa ule ulikuwa mchezo hatarishi na hivyo Kigonya hakustahili kubakia uwanjani.

Advertisement

Cha ajabu ni kwamba ni kama nchi nzima inatofautiana na refa, ambaye alikuwa karibu zaidi na tukio na ambaye aliona mazingira yote na ndiye mwenye mamlaka ya mwisho kutafsiri sharia anapokuwa uwanjani.

Kingine cha ajabu ni kwamba wale wa kwenye mitandao wanatumia video ambazo hazionyeshi uhalisia wa tukio, kuhitimisha kuwa ule ulikuwa mchezo hatarishi. Mmoja anatumia video inayomuonyesha Sakho mgongoni kana kwamba anatumia mionzi ya x-ray kuona mguu wa Kigonya ulio mbele ya Sakho.

Ni kama nchi imekubaliana tu kwamba yule refa alifanya makosa na hivyo kutafuta hata uongo kuthibitisha.

Na huu umekuwa utamaduni wa watu wa mpira. Kwamba kama kuna kitu kimetokea, basi ulimwengu mzima unakuwa na mawazo ya aina moja, hata yule ambaye akili yake inamwambia kuwa anavyoona si wengine wanavyoona, anajilazimisha kukubaliana na asichoamini.

Moja ya sababu za kuwa na akili ya aina moja, ni woga wa kuisema anachoamini kwa kuwa ataonekana wa ajabu kwa watu fulani, na sababu nyingine ambayo imekuwa kubwa kwa kizazi hiki ni ‘uchawa’.

Kwamba ili mradi Ma-PDG (mapedezyee) wako upande fulani, basi likitokea jambo tu, anaangalia aseme nini ili liwapendeze badala ya kukuna kichwa kuangalia jambo hilo vizuri na kutoa maoni yake kulingana na anavyoona.

Wanafalsafa wanaona jamii haiwezi kuendelea kama hakuna mawazo yanayopishana na ndio maana Mungu alitupa akili tofauti. Wako waliobuni hata ile kanuni ya asili ya “mkano wa mkano”, kwamba ni lazima kitu kikanwe ndipo kikae sawa na kisonge mbele.

Kama jamii itakuwa na mawazo ya aina moja dhidi au sawa na waamuzi, maana yake tutakuwa tunawaharibu. Pale wanapopatia wataona kuwa kundi kubwa linaona wanakosea na mwisho wataanza kufanya kazi kwa mtazamo wa kundi kubwa, hali kadhalika kundi kubwa linapoona amepatia.

Tunahitaji akili tofauti katika kuzungumzia maendeleo ya michezo au katika kuchambua kwa kuwa hilo husaidia wahusika kujitathmini na kufikiria ni jinsi gani ya kuboresha ili kusonga mbele.

Tabia ya kupotosha jamii kwa sababu za ‘uchawa’ haziwezi kutufikisha popote zaidi ya kusifu pasipostahili na kuponda pasipostahili.

Turudi kwenye akili zetu na kuyaangalia mambo kwa akili zetu kabla ya kutoa maoni yetu.

Advertisement