SIO ZENGWE: Kwanini haikuwa sahihi kumtimua Gamondi

Muktasari:
- Ramovich alikutana na kipigo cha mabao 2-0 alipowaongoza mabingwa hao wa Tanzania katika mechi ya kwanza ya makurdi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan takriban wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
BILA shaka mtu anayeumiza kichwa zaidi kwa sasa ni kocha Saed Ramovich, baada ya timu anayoinoa ya Yanga kupoteza mechi mbili kati ya tatu zilizopita, vipigo ambavyo ni vya kuanzia mabao mawili tofauti na mwenendo wa Wanajangwani katika miaka mitatu iliyopita, kama si wakati wote.
Ramovich alikutana na kipigo cha mabao 2-0 alipowaongoza mabingwa hao wa Tanzania katika mechi ya kwanza ya makurdi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan takriban wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akapata ahueni wakati Yanga iliposhinda 2-0 dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Lakini mambo yamekwenda tena mrama jana Jumamosi baada ya Yanga kupoteza mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa ilipofungwa tena 2-0 na MC Alger ya Algeria na hivyo kuendelea kushikilia mkia wa kundi ikiwa haina pointi, haijafunga bao huku ikiruhusu mabao manne katika mechi mbili.

Ahueni ni kwamba hakuna tofauti kubwa ya pointi katika kundi na hivyo kuweka uwezekano wa timu yoyote kuweza kufuzu kucheza robo fainali iwapo itacheza vizuri karate zake katika mechi nne zilizosalia. Al Hilal alikuwa akipambana na TP Mazembe mwishoni mwa wiki. Akishinda atafikisha pointi sita wakati Wakongo hao walikuwa na pointi moja kabla ya mchezo huo.
Matumaini ya Ramovic kufufua matumaini pengine ni kuwa na kikosi kamili wakati Yanga itakapoenda Lubumbashi kuivaa TP Mazembe katika mechi inayofuata. Tatizo kubwa la kikosi cha Yanga limekuwa ni kukosekana kwa kiungo tegemeo, Khalid Aucho. Nahodha huyo wa Uganda amekuwa akikosekana au kuchezeshwa nafasi tofauti katika mechi tano zilizopita ambazo vigogo hao wa Kariakoo walipoteza nne.
Katika mechi dhidi ya Tabora United, Yanga ilianza bila nyota wake Ibrahim Bacca, Dickson Job, Chadrack Boka na Yao Kwasi huku Aziz Andambwile aliyepangwa kushirikiana na Bakari Mwamnyeto akiumia mapema na hivyo Aucho kulazimika kurudi kucheza beki wa kati. Yanga ikachapwa 3-1.

Baada ya hapo Aucho hajaonekana. Na orodha ya majeruhi bado ikawa inawajumuisha Job, Aucho, Boka, Clement Mzize na Kouassi ambaye Jumamosi alirejea kikosini.
Huenda Ramovic atakuwa akitegemea majeruhi kurudi kikosini kuunda timu itakayoweza kwenda kuondoka na ushindi huko DR Congo na kurejesha matumaini ya Yanga kufikia robo fainali na kufikia ndoto yao ya kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza nusu fainali.
Lakini muda atakaokuwa nao kuweza kukiandaa kikosi kamili kuwa moto wa kuotea mbali nchini Congo ni mdogo wakati atakapoelekea kucheza mechi ya nne kati ya tano ambazo kocha mpya hupimwa uwezo wake.

Na kikubwa zaidi ni ile chapa ya Yanga kuanza kupotea huku ikionekana kuanza kuishi zaidi kwa matumaini kuliko uhalisia wa ubora wa kikosi kama kilichokuwa chini ya makocha wawili waliopita; Nasredine Nabi aliyekuwa akifanya vizuri kwa ushindi mdogo huku akitumia wachezaji wengi, na Miguel Gamondi aliyekuwa akipata mafanikio na ushindi mpana.
Anachokosa Ramovic kwa Nabi ni uwezo wa kutumia wachezaji wengi kwa kubadilisha wachezaji na baadhi kuwapanga nafasi zisizo za asili kwao kulingana na mahitaji ya wakati huo. Kibwana Shomari na Farid Mussa ni wachezaji waliochezeshwa nafasi tofauti kuziba mapengo ya majeruhi au kulingana na mbinu aliyopanga siku hiyo.
Kwa hiyo, kwa Nabi tatizo la kukosekana kwa baadhi ya wachezaji kutokana na kuwa majeruhi ama kadi , halikujitokeza sana kwa sababu alikijenga kikosi kuwa kipana huku akilinda staili yake ya mchezo na mbinu.
Pengine anayokosa Ramovich kwa Gamondi ni mengi zaidi na magumu. Tangu Gamondi aanze kuifundisha Yanga mabao ya krosi ya vichwa ni machache na yanakumbukika; la Bacca, la Job au la Joseph Guede.

Gamondi amekuwa akilazimisha mabao kupitia katikati ya ngome ya wapinzani au yale yanayotoka pembeni kidogo ya katikati (half space). Ndiyo mabao yanayotokana na pasi za Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Mzize au Clatous Chama hivi sasa, huku Aucho akilazimisha kuanzisha gonga nyingi za kuchana ngome za wapinzani.
Hakuna aliyeamini wakati Gamondi anampanga Jonas Mkude kushika nafasi ya Aucho wakati Yanga ikienda Afrika Kusini kurudiana na Mamelodi Sundowns katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita. Lakini kiungo huyo wa zamani wa Simba alimudu kuiunganisha timu, kuiwezesha kumiliki mpira zaidi ya wenyeji, kuipandisha timu mbele wakati sahihi na kuwa kinda ya mabeki wake. Aucho alikumbukwa baada ya mechi kuisha.
Lakini kwa Ramovich inakuwa rahisi kumkumbuka Aucho mapema kabisa. Kocha hamuandai mbadala wake mapema? Mbona Mkude, Andambwile, Abuye na hata Sureboy bado wapo?
Mbinu hiyo ya kufunga mabao kupitia katikati ya ngome ndiyo oliyoonekana ingekuwa nzuri zaidi kwa Prince Dube kiasi cha uongozi kufanya kazi kubwa kumpata mshambuliaji huyo Mzimbabwe. Na mechi zake za kwanza ilinekana ulikuwa uamuzi sahihi alipofunga katika mechi za kirafiki.

Na hata msimu ulipoanza alipenyezewa pssi nyingi, lakini hakuwa makini kumalizia, akikosa mabao ya wazi dhidi ya Simba na Azam wakati mashabiki walishasimama kuanza kushambulia.
Nafasi hizo zimeanza kupotea chini ya Ramovic ambaye anaonekana kuanza kumjaribu Kennedy Musonda.
Hadi Gamondi anaondoka hakuwa amepata mshambuliaji sahihi wa kati ambaye angekuwa chaguo la kwanza baada ya uongozi kumrundikia washambuliaji wanne; Kennedy Musonda, Prince Dube, Jean Baleke na Clement Mzize. Ameondoka akiendelea kujaribisha na Ramovich ataendelea kujaribisha kabla ya kumpata mtu sahihi.
Ile nguvu ya Yanga kuonekana ikizidi katika kipindi cha pili sasa inaanza kutoweka. Badala yake Yanga imeanza kuruhusu zaidi ya bao moja katika kipindi cha pili kitu kilichokuwa cha nadra sana kwa Gamondi na mara chache kwa Nabi.
Hayo yanatokea wakati kocha anayehusika na utimamu wa miili akiwa amefungashiwa virago na kuajiriwa mpya saa chache kabla ya timu kucheza mechi ya pili ya Ligi ya Mabingwa.
Mtu mwingine aliye na wasiwasi huku akiishi kwa matumaini ya kuwathibitishia wanaomkosoa kuwa bado uongozi uko sasa ni rais wa Yanga, Hersi Said, ambaye pamoja na kamati yake wanakosolewa kwa uamuzi wa kumtimua Gamondi katika muda ambao pengine alihitajika zaidi kuliko wakati mwingine kuiongoza Yanga kuandika historia ya kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa tangu mashindano hayo yabadilishwe muundo mwaka 1998.
Haijaelezwa sababu hasa za kumtimua raia huyo wa argentina lakini kuliibuka habari za kamati ya utendaji kutaka kikao na mtaalamu huyo usiku mara baada ya Yanga kutandikwa mabao 3-1 na Tabora United badala ya kupewa muda wa kawaida wa japo saa 24 kuandika ripoti na kukutana kwa dharura.
Kama nilivypeleza hapo juu, kuna uwezekano mkubwa udhaifu huu wa Yanga sasa unatokana na uamuzi huo wa kamati ya utendaji kumtimua kocha aliyekuwa akihitajika sana wakati huu kuliko wakati mwingine wowote kwa matumaini kwamba mbadala sahihi atapatikana mapema kama tairi jipya la gari.