Simba wacheze na akili za Berkane

Muktasari:
- Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyochezwa Mei 17, 2025 katika Uwanja wa Manispaa ya Berkane, Morocco, wenyeji RS Berkane waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba.
MCHEZO wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika umepangwa kuchezwa Jumapili, Mei 25, 2025, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 10 jioni.
Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyochezwa Mei 17, 2025 katika Uwanja wa Manispaa ya Berkane, Morocco, wenyeji RS Berkane waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba.
Iwe jua iwe mvua Simba inawakilisha Tanzania, ushindi ni lazima na kila mbinu za kitaalamu ni lazima zifanyike kuhakikisha inapata ushindi wa mabao 3-0 ili kutangazwa bingwa wa mashindano hayo.
Kona ya SpotiDokta inaitazama upande wa ushindi kupitia saikolojia, yaani kiakili kama moja ya mbinu rahisi ya Simba kushinda fainali hiyo ya mchezo wa pili.

KUCHEZA NA AKILI NI HIVI
Kucheza na akili ya mpinzani halihusu tu kwa wachezaji na benchi la ufundi pekee, bali pia sehemu kubwa ya mashabiki 16,000 waliokwishakata tiketi wanaotarajiwa kuhudhuria katika mchezo huo.
Hamasa ya kushabikia kwa namna yoyote ile ikiwamo kuimba, kuzomea au kupiga filimbi na mavuvuzela ni ya kipekee ambayo inamfanya mchezaji mwenyeji kuhamasika kucheza kwa bidii kubwa.
Wakati huohuo hamasa ya mashabiki ndiyo ambayo inawatetemesha wachezaji pinzani kiasi cha kuingiwa na hofu, hivyo kukosa kujiamini na kufanya makosa ambayo itakuwa ni faida kwa Simba.
Suala la kucheza na akili ya timu pinzani halijaanza leo katika soka. Kwa wafuatiliaji wa mpira wanaelewa hilo katika viwanja vya mpira kama uwanja wa Liverpool wa Anfield ambao ni maarufu kwa kuwa na mashabiki wa pekee ambao mwanzo mwisho hushangilia.
Ni wakati wa mashabiki wa soka Tanzania kuigeuza anga la New Amaan Complex kuwa anga la Anfield. Inahitajika kelele za kutosha kushangilia katika nyakati zote ikiwamo ngumu na nyepesi. Inahitajika kuifanya siku hiyo kama vile Simba ndio ilishinda mchezo wa awali.

KWA WACHEZAJI SASA
Hakuna shaka kwa wachezaji wa Simba mpaka kufikia hatua hiyo wana utulivu mkubwa wa kiakili na mwili. Hata kuelekea katika mchezo huo wako timamu.
Wanachotakiwa ni kushinda hofu ya aina yoyote. Wazo la kushindwa lisiwepo katika akili zao. Mshikamano wa mchezaji mmoja na mwingine ndani ya uwanja utawapa matokeo chanya.
Mchezaji akijengwa vizuri kiakili, huweza kucheza na hamasa na ari kubwa kiasi cha kujituma sana hata pale anapokuwa amechoka. Hamasa pia inaanza na wao kwa wao kwa kupeana mioyo nyakati zote. Kusiwepo hali ya kumlaumu mtu yanapotokea makosa ya kimchezo. Mchezaji aliyejengwa vizuri kiakili hucheza mpira kwa nguvu na kasi kubwa kuliko kile kiwango chake cha kawaida. Viongozi na wachezaji wa zamani kuzungumza nao mawili matatu inawapa hamasa na kuwafanya wajiamini. Utulivu wa kiakili kwa wachezaji wa Simba ndiyo unawafanya kufanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi. Hilo halina shaka kwa sasa kwani ndilo limewafikisha walipo.
Ikumbukwe kuwa uchovu wa kiakili ni moja ya sababu kwa wachezaji kufanya makosa ikiwamo uamuzi mbovu. Hakuna shaka katika hilo Simba kufikia hatua hiyo benchi la ufundi na wataalamu wa afya wanajua vyema viashiria vya uchovu wa kiakili vya mchezaji wakati wa mazoezi.
Ndani ya uwanja wachezaji ni muhimu wazingatie kuonyana kwa kutanguliza uungwana. Mbinu za kuvurugana kiakili ndani ya uwanja ndizo pia anazotumia adui. Wachezaji wanatakiwa kuwa makini na mbinu za wachezaji wanaotoka nchi za Kiarabu. Huwa na tabia ya kuchokoza au kujiangusha makusudi ili tu ukasirike kwa kukuudhi.
Mbinu zingine ambazo wachezaji wa Simba wanapaswa kuwa nazo wanaangalifu ni tabia ya wachezaji kufanya mambo ya kuudhi ikiwamo kupoteza muda wakati wa kurusha au kuanza mpira. Wachezaji wa Simba wanapaswa kuepuka mitego hiyo ambayo inaweza kuwafanya kukasirika na kuitoa akili mchezoni au la - kucheza na hasira na hatimaye kupata kadi zisizo za lazima.
Akili inatakiwa kuangalia zaidi lengo kuu ambalo ni ushindi wa mabao 3-0. Hawapaswi kuruhusu bao, bali kufunga mabao. Kuruhusu kuifikirisha akili na mambo mengine nje ya lengo hilo ni kuharibu lengo kuu.

KWA MASHABIKI
Mpira huwa ni furaha na burudani na huwa na matokeo makuu matatu ikiwamo kufungwa, kushinda au kutoshana nguvu.
Mashabiki waepukane na ushabiki wa kushangilia tu wakati wa kufanikiwa. Ikitokea timu inashambuliwa au mchezaji amekosea wanatakiwa kuendelea kushangilia kwa nguvu bila kuchoka. Hiyo itawafanya wachezaji kujiona siyo wakosefu, bali washindi, lakini pia kuwapa hofu wapinzani.
Kuweza kuvuruga akili za wachezaji pinzani kunahitaji pia vikundi vya mashabiki kila kona ya uwanja ikiwamo karibu na kipa wa timu pinzani, lango la kuingilia na nje ya uwanja.
Vikundi vya mashabiki vina mchango mkubwa katika kuijengea hofu na woga timu pinzani na hatimaye kuivuruga akili na kuitoa mchezoni. Kufanikiwa kuvuruga akili ya mchezaji pinzani ndiko kutawafanya washindwe kutelekeza kwa ufanisi mbinu za kushinda walizofundishwa na kocha wao.
Mashabiki wote mpaka wa wale watani zao wa jadi wanatakiwa kushirikiana kucheza na akili za Berkane ili kuhakikisha haipati mwanya wa kujenga hamasa ndani ya dimba.