SIO ZENGWE: Kwanini dua kwa Simba, Yanga ni muhimu CAF

KATIKA soka lolote laweza kutokea hata pale inapoonekana haiwezekani kabisa. Labda iwe ni utashi wa Mola tu, lakini ni vigumu mno kuona Simba na Yanga zikishindwa kufikia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika msimu huu baada ya matokeo ya mechi zao za kwanza za raundi ya kwanza ugenini.

Simba ililazimisha sare ya mabao 2-2 na wenyeji Power Dynamos ya Zambia, mjini Ndola na hivyo kuhitaji sare yoyote ya chini ya mabao mawili au ushindi katika mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam ili kutinga makundi.

Yanga ndio ilijiweka katika nafasi nzuri zaidi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Al Merrikh iliyolazimika kuchezea mechi yake jijini Kigali, Rwanda kutokana na machafuko yanayoendelea Sudan.

Matokeo hayo yanaziweka Simba na Yanga katika uwezekano wa kuandika historia ya kuwa timu mbili za Tanzania kufuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano mikubwa barani Afrika kwa ngazi ya klabu tangu mundo wake ulipobadilishwa mwaka 1998 kwa kuingiza kucheza kwa mtindo wa ligi baada ya hatua mbili za awali za mtoano.

Mwaka huo, Yanga iliandika historia ya kuwa moja ya timu nane zilizoasisi muundo huo, ingawa matokeo yake katika hatua hiyo ya robo fainali iliyochezwa kwa mtindo wa ligi, si ya kusimulia sana.

Na matokeo ya mechi za Jumamosi jijini Kigali na Ndola si ya kubahatisha kiasi cha kuwafanya mashabiki wasiwe na uhakika sana. Ingawa Simba ilitanguliwa mara mbili, bado ilisawazisha na wakati fulani ilionekana kama imeuchukua mchezo kama si washambuliaji wake, hasa Jean Beleke kupoteza nafasi tatu za wazi ambazo zingeweza kuifanya Simba ipumzike vizuri wakati ikisubiri mechi ya marudiano.

Yanga ndio iliishika mechi kabisa, ikishambulia kwa muda mwingi huku ikimiliki mpira kana kwamba ilikuwa inacheza nyumbani. Wakati fulani unaweza kuamini kuwa matokeo hayo ya ushindi wa mabao 2-0 hauakisi jinsi mchezo ulivyokwenda, labda kama Yao Kouassi na Maxi Nzengeli wangeweza kuzitumia vizuri nafasi walizopata mapema katika kipindi cha kwanza kibao cha magoli kingesomeka kwa jinsi ambayo kila mtu angeridhika.

Haya ni mafanikio makubwa kwa klabu zetu, ingawa hayaakisi mpira wetu kwa ujumla. Kati ya mabao manne yaliyofungwa na klabu hizo mbili, ni bao moja tu lililofungwa na Mtanzania, Clement Mzize, dakika chache kabla hajabadilishwa.

Katika kikosi kilichoanza, wazawa walikuwa wanne tu, yaani Ibrahim Bacca, Dickson Job, Mudathir Yahya na Mzize na baadaye akaingia Zawadi Mauya.

Hali haikuwa tofauti sana jijini Ndola ambako Simba ilianza na wachezaji wenyeji wanne; Shomary Kapombe, Mohamed Hussein, Kibu Denis na Mzamiru Yassin na baadaye John Bocco kuingia.

Hiyo si nzuri sana kwa soka la Tanzania, lakini halina uzito sana kwa ngazi ya klabu ambako kinachotakiwa zaidi ni ushindi, hasa katika mashindano ya kimataifa kama hayo.

Tunahitaji ushindi na mafanikio ya namna hii—kama timu zote zitaingia makundi—ili kusimika jina la Tanzania katika ramani ya Afrika kwa kuwa kuna faida kubwa.

Hivi sasa kampuni zinazowekeza au kujitangaza kwenye klabu zetu ni zile za hapa hapa nchini, ukiondoa za michezo ya kubahatisha ambazo zimesambaa kote duniani.

Lakini angalia udhamini kama wa mavazi na vifaa, bado ni kampuni ambazo hazijaweza kujijenga vizuri, si tu katika soko la ndani bali hata kimataifa. Ungetegemea kusikia kampuni kama Nike, Adidas, Puma, Umbro, Admiral, ASICS na Brooks zikimiminika kuja kudhamini klabu zetu kama Adidas inavyofanya kwa Al Ahly, lakini kwa sababu hatujaweka alama kimataifa, bado zinasita.

Ungetara-jia kampuni kubwa za uwekezaji zikimiminika kununua hisa za umiliki wa klabu zetu, lakini bado soka halijachanganya sana kiasi cha kampuni kubwa kama za Marekani, Arabuni, Asia na kwingine kutofikiria kuja nchini.

Tunachoendelea kukiona ni ule utamaduni wa ajabu wa klabu kuinunua klabu nyingine iliyo daraja la juu ili ipande kirahisi, kama Lipuli ilivyofanya hivi karibuni kwa kuinunua Ruvu Shooting iliyo Championship. Huku ni kutaka mafanikio ya haraka bila ya kuwa na uwekezaji kamilifu.

Kwa hiyo, tunahitaji sana kutangaza Ligi Kuu yetu kwa kupata mafanikio kama haya ambayo Yanga na Simba wanatarajia kuyapata ili kuanza kustua wenye fedha huko nje ya nchi.

Kama Simba na Yanga zitafuzu kucheza hatua ya makundi na ikiwezekana hadi robo fainali, huku Simba ikifanya vizuri katika michuano mipya ya Ligi ya Afrika na mwakani Yanga ikajumuishwa na zote zikafanya vizuri, sina shaka kwamba tutakuwa tumepiga hatua kubwa mbele kuelekea kuitangaza Tanzania na kustua wawekezaji kuwa kuna kitu kikubwa nchini kinachoweza kuwalipa iwapo wataweka fedha zao.

Dua letu ni kwa Simba na Yanga, si tu kufika hatua ya makundi, bali kwenda mbele hadi, ikiwezekana, fainali na hapo sasa tutaanza kuzungumza mengine.

Pengine hata huu ushabiki wa kipuuzi wa kuombeana mabaya utaisha na wananchi wataunganisha nguvu na kuwa nyuma ya yeyote atakayekuwa akiwakilisha taifa.

Wakati tukitarajia haya makubwa, ni wakati pia wa kuangalia mfumo wetu wa uendeshaji soka katika ngazi ya klabu kama unakaribisha hao wawekezaji kuja nchini, ama tutaendelea kuwa nao huu wa sasa wa kutukuza wanaokuja kufanya biashara na klabu bila ya kuwawekea mifumo salama kwa pande zote mbili—klabu na mwekezaji.

Hadi sasa Simba na Yanga zinahaha kuwa na mfumo bora wa umiliki, lakini zimewahiwa na wawekezaji kiasi kwamba mageuzi wanayotaka kuyafanya yanawekewa mwongozo na hao wawekezaji, huku kukiwa na ilani kuwa wasipofuata mwekezaji atasusa.

Kunahitajika mageuzi yenye njia salama na isiyo na vitisho vya kususa au kujitoa ili kuwe na mabadiliko ya kweli.

Ni kwa vipi hao wawekezaji wakija wataridhjishwa na watendaji waliopo kwenye klabu kubwa. Idara kama za masoko, ambazo naweza kusema ni muhimu sana, zinafanya kazi yake ipasavyo, au utafutaji wadhamini hutegemeana na urafiki wa viongozi kwa wenye kampuni au vigogo walio katika kampuni kubwa?

Pia katika kipindi hiki tunachotarajia mafanikio, tunajiaandaaje kukuza vipaji vya wazawa? Bado watawala wetu wa soka la Tanzania hawana mfumo wowote wa kuendeleza vipaji. Ni kitu cha kushangaza kwamba mchezaji kama Said Ndemla, aliyesajiliwa na Simba akiwa kinda, anaondoka kama mchezaji wa kawaida na si yule aliyeonekana hazina.

Hakuwahi kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza na ameondoka bila heshima yoyote kubwa. Ndemla anawakilisha vijana wengi wanaovundikwa na klabu kubwa bila ya kufuatiliwa hadi wanaoza na baadaye kutupiliwa mbali.

Uwekezaji kutoka nje unatakiwa ukutane na mazingira mazuri ya kukuza na kuendeleza vijana.

Yapo mambo mengi yanayoweza kuibuka iwapo klabu hizo mbili zitaendelea kufanya vizuri Afrika, lakini nimeona nianze na hayo.