SIO ZENGWE: Kwaheri Ndolanga uliyepania uhuru wa soka

Tuesday September 21 2021
ndolanga pic

KUNA wakati alichukiwa na karibu kila mpenda mpira wa miguu, isipokuwa wajumbe takriban 60 wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (Fat) ambacho sasa kinaitwa TFF baada ya mabadiliko ya muundo mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Huyu ni Alhaji Muhidini Ndolanga aliyekuwa mwenyekiti wa Fat tangu 1992 hadi 2004 aliposhindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Hoteli ya Golden Tullip jijini Dar es Salaam.

Ilibidi mengi yafanyike ili kupambana naye kwenye boksi la kura. Idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu iliongezeka kwa kuongeza vyama shiriki na hivyo ukubwa wa chombo hicho kikuu cha mpira kupanuka kutoka wajumbe wapatao 70 hadi takriban 140.

Ndolanga aliondolewa katika raundi ya kwanza baada ya Michael Wambura kuongoza akifuatiwa na Leodegar Tenga, hivyo upigaji kura kurudiwa ili mshindi apate angalau asilimia 50 ya kura zote na ndipo Tenga alipomuangusha Wambura na kuchukua usukani wa soka.

Ni kweli kwamba wakati wa uongozi wa Ndolanga wengi hawakukubaliana na mwenendo wa Fat na hivyo kufanya jitihada kubwa kumuondoa. Wale waliojaribu kutumia boksi la kura walianguka vibaya mbele ya wajumbe ambao walikuwa wakimkubali isivyo kawaida.

Lakini umaarufu wa Ndolanga ulitokana na wale waliotaka kumuangusha kwa kutumia njia za vichochoroni au kutumia wenye mamlaka serikalini. Hapo ndipo mwenyekiti huyo aliposimama kidete kuhakikisha mipango hiyo haifanikiwi na nguvu ya mkutano mkuu inaheshimika.

Advertisement

Kwa waliojaribu kupindua meza, haikuwezekana kwa kuwa tayari alikuwa na watu shupavu waliokuwa wakimuunga mkono. Wale waliojaribu kutumia viongozi wa serikali ndio waliopata shida.

Kila mara waziri alipotangaza kuuvunja uongozi wa Fat na kuweka kamati za muda, Ndolanga alilitaarifu Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambalo mara moja liliagiza viongozi wa kuchaguliwa warejeshwe madarakani la sivyo Tanzania itafungiwa kujihusisha na soka kimataifa.

Na michuano ilipokaribia ambayo Tanzania ilitakiwa ishiriki kama taifa au klabu, hofu ya kuikosa ilitanda na mara moja viongozi wa kuchaguliwa wakarejeshwa madarakani.

Suala hilo lilijitokeza kila mara kiasi kwamba Ndolanga akaonekana kama ni mbabe asiye tayari kutii hata mamlaka za serikali. Ikaonekana kama alikuwa akiwahonga wajumbe wa mkutano mkuu ili wawe upande wake wakati wote.

Lakini hoja ya Ndolanga ilikuwa moja tu; viongozi wa FAT wanachaguliwa na mkutano mkuu tu. Si mamlaka za serikali au kitu kingine chochote. Ni mkutano mkuu pekee na Fifa ndio wanaoweza kuunda uongozi wa muda au kuwawajibisha viongozi wasioenenda vizuri.

Huo ndio ulikuwa msimamo wa Ndolanga na si kwamba alikuwa mbabe au kuna kitu zaidi ya hoja hiyo alichokuwa akitegemea. Alitaka taratibu zifuatwe katika kuwaondoa viongozi au kuwawajibisha.

Bila kufuata taratibu, waziri anaweza kutafuta sababu zozote zile, halafu akavunja uongozi na baadaye kumuweka mtu wake. Ndivyo Ndolanga alivyokuwa akiamini kuwa katika sakata la kumuengua mara kwa mara kuna waziri alikuwa akitaka kumchomeka mtu wake, hivyo akawa anasisiza kuwa huyo mtu ni lazima atumie mchakato uliowekwa na katiba ya FAT na si njia nyingine.

Yapo mengi unayoweza kusema kuelezea ushupavu wa Ndolanga, lakini kubwa ni hilo la kupigania uhuru wa vyombo vya maamuzi vya mpira, kupigania uhuru wa FAT na kusimamia katiba na taratibu katika kusimika viongozi.

Angeweza kubadili katiba ili kuweka mazingira magumu kwa wengine kuupata uenyekiti wa FAT, lakini hakuwa na uchu wa kiasi hicho cha kuchezea katiba kwa maslahi yake binafsi. Alichotaka ni katiba iliyokuwepo ifuatwe na ndio maana hakuwa mbishi pale Golden Tullip alipotangazwa kuwa hakupata kura za kutosha kuingia raundi ya pili ya kura.

Na hata alipotoka hakuingia msituni kupambana na mwenyekiti aliyeshinda, bali aliendelea na shughuli zake za kawaida huku akiitwa katika baadhi ya shughuli za mpira.

Uhuru huu alioupigania Ndolanga hauna budi kulindwa na kila mtu. Si vizuri kupora mamlaka ya vyombo vya maamuzi vya TFF na kuyapeleka kwa watu binafsi, hasa wanasiasa, ili kujilinda.

Viongozi wa mpira wanatakiwa walindwe na mafanikio yao kiungozi na pia katiba na si walindwe na wanasiasa.

Kufanya hivyo ni kuenzi vita aliyoipigania Muhidini Ndolanga wakati wote akiwa mwenyekiti wa FAT.

Kwaheri Ndolanga, shujaa uliyepania uhuru wa soka.

Advertisement