SIO ZENGWE: Haji Manara ameipa somo Simba?

TANGU Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipoagiza klabu za Ligi Kuu kuwa na sekretarieti, ambayo ingehusisha waajiriwa, ikiwemo nafasi muhimu ya ofisa habari, kumekuwepo na dhana potofu kuhusu kazi hiyo.

Ingawa waajiriwa wengi wa nafasi hiyo au wale waliopewa jukumu hilo, wamekuwa ni waandishi wa habari, lakini majukumu yao nadhani yalikuwa hayaainishwi vyema.

Hivyo wale wanaoweza kutengeneza maneno yakavutia watu, yakachekesha, yakashangaza na hata maneno mazuri ya kuponda wapinzani, wakaonekana ndio wanaoweza kuimudu nafasi hiyo, hasa kwa klabu kubwa kama Simba na Yanga.

Wapo wale wasemaji wa Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting ambao wameingia katika mtego huo, hivyo kuwa kivutio kwa maripota kila klabu zao zinapokaribia kucheza mechi muhimu au zile kubwa au baada ya mechi kuisha.

Na kwa sababu waliokuwa wanawapa hizo ajira ni wale wanaoamini kuwa kusema sana ndio utendaji mzuri, hawa maofisa habari ambao eti wanajulikana kama wasemaji wakati msemaji ni mtu mwenye mamlaka makubwa katika taasisiwakawa wasemaji hasa.

Kwani wakati mwingine kuzungumzia hata masuala ya ufundi, ikiwemo kuahidi ushindi (kitu ambacho hata makocha huchelea kuahidi) na wakati mwingine kuzungumzia masuala ya msimamo wa uongozi wakati hata katika kikao cha uongozi hawahudhurii.

Hawa ndio waliochora picha hiyo ya Ofisa Habari wa klabu kuwa ni msemachochote, anayefurahisha, mwenye uwezo wa kutumia maneno ya kila aina kuwashusha wapinzani, na ikafikia wakati hata masuala muhimu ya maendeleo ya mpira wa miguu yakageuzwa kuwa ni utani usiotaka majawabu.

Baadhi wakaanzisha makundi ya WhatAssap kujiongezea wigo wa wafuasi, hivyo kuonekana wakiongeza ufanisi wa majukumu yao kwa kuwa na makundi makubwa na hivyo ujumbe wao kuwafikia watu wengi ndani ya muda mfupi.

Haji Manara alikuwa mmoja wa maofisa hao wa habari. Kulikuwa na minong’ono ya muda mrefu kuwa uongozi ulikuwa unataka kuachana naye, ila ulikuwa ukisita kutokana na kutokuwa na uhakika wa matokeo ya uwanjani, lakini Haji aliendelea kuwepo na akaonekana kuwa mkubwa kuliko hali halisi.

Kusambaa kwa sauti yake inayomtishia Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, kulionekana kama ni mgongano wa viongozi kwa dhana iliyojengeka kwamba Manara ni kiongozi na si mtu aliye katika ajira ambayo Barbara anaisimamia na ana uwezo wa kuisitisha.

Pengine hilo ndilo lililowastua viongozi wa Simba kwamba kuna haja ya kuchukua hatua kwa kuwa sakata hilo lilionyesha dhahiri kwamba klabu hiyo bado inaendeshwa kizamani, kiasi kwamba hata ofisa habari anaweza kumbwatukia muajiri wake asifanywe lolote.

Hivyo Bodi ya Wakurugenzi ya Simba ikapata fundisho na kuchukua uamuzi huo wa kukubaliana na uamuzi wa kujiondoa kwa mtu ambaye alishaaminika kuwa ni sehemu ya mafanikio ya Simba na yuko katika ngazi moja na viongozi wengine wa klabu.

Lakini somo hilo halijakolea vizuri kwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba. Bado ofisa habari ni mtu mdogo sana katika sekretarieti au menejimenti ya klabu kiasi cha kuandikiwa barua ya kukubaliana na uamuzi wake wa kujiondoa.

Kama Barbara ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu, uamuzi wa hatma ya Manara ulikuwa mikononi mwake kama kwenye Bodi ya Wakurugenzi inataka awe na nguvu kwa waajiriwa walio chini yake.

Kwa kawaida bodi ndio inayomuajiri Ofisa Mtendaji Mkuu ili aisimamie sekretarieti au menejimenti, ikiwa ni pamoja na kuajiri au kuchukua hatua za kinidhamu kulingana na sheria za kazi klabuni. Kama bodi itachukua jukumu la kuwasiliana na ofisa habari kuhusu masuala ya kazi, basi CEO hana kazi muhimu na kama bodi ndiyo itateua mtu mwingine kushika kwa muda nafasi hiyo, Barbara anafanya nini?

Kazi ya bodi katika taasisi nyingi kubwa (corporate organisations) ni kupanga na kutoa maagizo na si kufanya kazi za kila siku wakati kuna sekretarieti au menejimenti. Kutimua na kuajiri watendaji wa chini ni jukumu la menejimenti inayoongozwa na CEO.

Pia, ni muhimu Simba, kama inavyoeleza kuwa inataka kujiendesha kisasa, kuwa na kanuni za udhibiti za uendeshaji wa akaunti binafsi za mitandao ya kijamii.