Simulizi ya bondia kifo cha Mgaya
Muktasari:
Kifo cha bondia Hassan Mgaya bado kimekuwa mzigo wa mwiba kwa bondia chipukizi katika ngumi za kulipwa nchini, Paul Elias kiasi ambacho kinamfanya akose amani kwa kujiona mkosaji licha ya ushindi ambao aliupata kwenye pambano hilo lililofanyika Desemba 28, 2024, Ukumbi wa Dunia Ndogo uliopo Tandale jijini Dar es Salaam.
MIONGONI mwa mambo yaliyokuwa gumzo mwishoni mwa mwaka 2024 hadi mapema Januari 2025 ni tukio la bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mgaya kufariki baada ya kumalizika kwa pambano lake dhidi ya Paul Elias.
Kifo cha bondia Hassan Mgaya bado kimekuwa mzigo wa mwiba kwa bondia chipukizi katika ngumi za kulipwa nchini, Paul Elias kiasi ambacho kinamfanya akose amani kwa kujiona mkosaji licha ya ushindi ambao aliupata kwenye pambano hilo lililofanyika Desemba 28, 2024, Ukumbi wa Dunia Ndogo uliopo Tandale jijini Dar es Salaam.
Maandalizi yako yalikuaje kuelekea pambano na Mgaya?
"Binafsi upande wangu yalikuwa mazuri lakini siwezi kuongelea upande wake (marehem) kwa sababu nilikua sijui chochote, nilijiandaa kama ninavyojiandaa wakati mwingine pamoja na kumuomba Mungu anisaidie niweze kushinda.
"Lakini hata ukiangalia rekodi ya mpinzani wangu yeye alikuwa amecheza mapamano mengi na mzoefu wa ulingoni kuliko mimi.
Niliona kipande cha video wakati mnapima uzito marehemu alikuwa akiongea kuwa umeyakanyaga, kisaikolojia ilikuwaje upande wako?
"Kwa jinsi nilivyolelewa hadi kufikia umri huu hali ya kupendwa au kuchukiwa ni jambo la kawaida lakini kwenye mchezo huu maneno ya tambo ni sehemu ya mchezo, nilichukulia kawaida kwa maana yeye alikuwa akiwahamasisha mashabiki zake wawe na morali na siyo kukaa kinyonge.
"Nilipokea kama sehemu ya mchezo na siyo yeye peke yake ambaye anatumia tambo za hivyo na wala sikulichukulia kama jambo baya.
Pambano lenyewe lilikuaje?
"Kama unavyojua pambano lilikuwa raundi la sita, tumecheza raundi ya kwanza alikuwa ana score (kupata pointi), tukaingia raundi pili ikaisha vizuri mpaka tatu nayo tulimaliza vizuri.
"Lakini ilivyofika ya nne, kama uliona video kuna sehemu wakati tunapigana, alidondoka, mwamuzi akamfuata, tukaendelea na mchezo.
"Kwa kawaida bondia anacheza kulingana na mchezo ulivyo huku mwamuzi ndani ya ulingoni akisisitiza anataka kuona ngumi na ndiyo maana hata alivyoanguka na kufuatwa, alikubali kuendelea na mchezo.
"Lakini ilifika wakati akaweka gadi ya kujilinda maana yake ameshachoka, nikawa nashambulia nataka kumaliza mchezo mapema, mwamuzi akaingilia kati kumaliza pambano kwa kuwa mpinzani hakuweza kurusha ngumi jambo ambalo ushindi wake unakuwa Technical Knockout.
"Baada ya kumaliza nikawa natembea kurejea kwenye kona yangu na yeye akawa anaelekea kwenye kona yake lakini ghafla kabla hajafika vizuri kwake nikaona ameanguka haraka daktari na watu wake wakaanza kumpa huduma ya kwanza.
"Nilitaka kusogea lakini nilishindwa kwa sababu mashabiki zake tayari walikuwa wamepaniki, ikabidi nitulie kwenye kona yangu kwa sababu sikutarajia wala kutegemea kuona kile ambacho kimetokea wakati ule.
"Kiukweli ilinivuruga kwa sababu sikumpiga ngumi ambayo ilimdondosha, mwamuzi alimaliza pambano akiwa kwenye hali nzuri halafu ghafla naona mwenzangu anapewa huduma ya kwanza, nikawa sielewi kinachoendelea.
"Baada ya hapo ndiyo walimpeleka hospitali na sikutegemea kama ingefika huko halafu linatokea jambo la ghafla ikiwa na yeye alikuja kwa lengo zuri la kucheza ngumi.
"Kuna wakati nilijiuliza labda alikuwa na shida nyingine ambayo pengine haikugundulika kwa madaktari wakati anafanya vipimo.
Taarifa ya msiba uliipokea wakati gani na ilikuwaje upande wako?
"Kabla ya taarifa ya kifo, nilikuwa napewa taarifa za hali yake kuwa mbaya huku nikiambiwa tuongeze maombi hali yake ikae sawa lakini kwa bahati mbaya ndiyo ikawa imetokea hiyo ya kifo.
"Kiukweli baada ya kuambiwa mwenzetu hatupo naye, nilikosa nguvu kwa sababu ni jambo ambalo sijategemea na limeniweka kwenye wakati mgumu sana, imefika sehemu nawaza mambo mabaya kutokana na kilichotokea.
"Nimeshindwa hata kupiga simu kwa taarifa zilivyokuja na hata ukiangalia kile kipande cha video, tumepima kwa amani sana tukawa tunataniana, tulikuwa marafiki kwa sababu haikuwa vita bali mchezo.
"Binafsi nimeshindwa kufanya chochote hata kutuma ujumbe wa pole nimeshindwa kwa sababu nimeogopa kufikiriwa tofauti, nimeshindwa hata kwenda kushiriki mazishi kwa sababu hofu kubwa ambayo imekuwepo kwangu ila wenzangu walienda kuniwakilisha.
"Sikuwa naweza hata kupokea simu kwa sababu nilikuwa naona matatizo ndiyo yananikuta na sijazoea ugomvi, nimekuwa mtu wa ndani hata chakula bado imekuwa ngumu kwangu kula.
Malipo yako yalikuwaje maana marehem imetajwa amelipwa shilingi elfu sitini?
"Sijui niseme nini ila sisi bado tunajitafuta, inabidi upigane hivyo ili kuweza kufikia malengo, aliyeandaa ni kocha wangu (Ngoswe), tulikubaliana akipata chochote atanipa lakini kwa hali ambayo imetokea nilimwambia afanyie majukumu ya kwenye msiba, siwezi tena kuichukua maana roho inaniuma.
Watu wanasema nini mtaani dhidi yako?
"Sijawa maarufu kiasi cha watu kunijua zaidi ya wale ambao wananizunguka ndiyo wamekuwa wakinitia moyo ili niweze kukaa sawa, salamu za pole zimekuwa nyingi kwa sababu ni jambo la bahati mbaya.
Familia inasemaje juu ya tukio lenyewe?
"Kiukweli wao baada ya kujua kwanza hawana amani kama nilivyokuwa mimi ingawa hao ni juu ya mambo ya kimamlaka kwa sababu wanajua nitakamatwa," anasema Elias ambaye ni mzaliwa wa Mwanza katika Wilaya ya Sengerema eneo la Itabagumba, akiwa ni kijana wa miaka 27 huku maisha yake ya ukuaji akilelewa na shangazi yake kwenye Kisiwa cha Kome kinachopatikana Ziwa Victoria.
Bondia huyo siyo mgeni katika mchezo wa ngumi za kulipwa kutokana na kucheza mapambano kadhaa licha ya rekodi zake kutowekwa kwenye mtandao wa ngumi uitwao Boxrec.
Katika mtandao huo, Elias anaonekana amecheza mapambano sita, akiwa ameshinda manne likiwemo dhidi ya marehem Hassan Mgaya, kati ya hayo matatu ameshinda kwa Technical Knockout (TKO) na moja mpinzani wake akiacha kwa kushindwa kuendelea. Pia amepoteza mapambano mawili kati ya hayo moja kwa Knockout (KO).
Elias katika uzani wa Welter, amepewa asilimia 100 za kushinda kwa Knockout huku akiwa bondia wa 39 katika mabondia bora 57 wa uzani huo nchini Tanzania na duniani akiwa wa 1322 kati ya mabondia 2419.
Mwanaspoti limefanya mahojiano maalum na bondia huyo ambapo ameeleza mambo mengi kwa uchungu tangu kitokee kifo cha mpinzani wake aliyezikwa Januari 2, 2025.
Elias anasema alikuja jijini Dar es Salaam mwaka 2015 akitokea Kome, Mwanza kwa lengo la kutafuta maisha akiwa amefikia Mbezi na kazi yake ikiwa ni kutunza bustani.
"Nimekuja Dar mwaka 2015, wakati nakuja lengo lilikuwa ni kutafuta maisha licha ya kwamba nilikuwa napenda mchezo wa ngumi tangu nipo mdogo.
"Nilikuwa nafanya sana mazoezi kwa sababu ndoto yangu kwanza nilitaka kuwa mwanajeshi lakini bahati mbaya elimu yangu haikuweza kunisogeza kabisa upande huo.
"Sasa kutokana na hivyo ndiyo niliamua kuingia kwenye ngumi kwa sababu tayari nina mapenzi na mchezo wenyewe huku ishu kubwa ni kuona siku moja nafikia malengo yangu ya kimaisha. Nikatafuta chama cha ngumi, pia nikapata mwalimu.
"Mwaka 2020 nadhani ndiyo nilianza rasmi mchezo huu, nikitokea kwa kocha Haji Ngoswe ambaye ndiye aliandaa pambano langu na Hassan Mgaya.
Familia yako ilisema nini baada ya kuingia kwenye ngumi?
"Baba na mama yangu tayari walishafariki nikiwa mdogo, nimelelewa na shangazi yangu ndiyo maana nilikwambia nimelelewa kisiwani kwa sababu alinichukua baada ya baba na mama kufariki.
"Lakini hata nilivyomueleza yeye juu ya uamuzi wangu wa kuwa bondia hakunizuia zaidi ya kutaka niwe makini kwa sababu ni mchezo wa hatari ingawa mara kadhaa ameonyesha wasiwasi wake kama ninauweza mchezo wenyewe.
Kwa sasa hapa Dar unaishi na familia yako mwenyewe?
"Hapana, bado sijaoa na wala sina mwanamke kwa sababu bado najitafuta kwani nimeona naweza kufanya hivyo kwa sasa nikazuia ndoto zangu, subiri kwanza nipambane nitakapofikia nadhani hilo litatokea kwa uwezo wa Mungu.