Simba ilistahili ubingwa

Muktasari:

SIMBA imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo juzi Jumapili. Mwanaspoti linakuletea maeneo ambayo mabingwa hao walikuwa imara, pengine tofauti na timu nyingine mpaka kutwaa taji hilo.

SIMBA imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo juzi Jumapili. Mwanaspoti linakuletea maeneo ambayo mabingwa hao walikuwa imara, pengine tofauti na timu nyingine mpaka kutwaa taji hilo.


MASTRAIKA

Wamefunga mabao 73, huku mastraika wao watatu wakichangia kwa kiasi kikubwa kwa kufunga mabao 39. John Bocco ambaye ndio kinara wa ufungaji ana mabao 15 akifuatiwa na Chriss Mugalu aliyefunga 13 na mfungaji bora mara mbili mfululizo misimu miwili iliyopita, Meddie Kagere akiwa na mabao 11.

Katika misimu yote minne ambayo Simba ilitwaa ubingwa walitoa pia mfungaji bora akianza Emmanuel Okwi, akafuata Kagere mara mbili na msimu huu kama sio Bocco, basi Mugalu au Kagere atatetea tuzo yake.

Ukimtoa mshambuliaji wa Azam, Prince Dube mwenye mabao 14, hakuna mshambuliaji mwingine ambaye ameufikia moto wa mastraika hao wa Simba ambao licha ya kucheza mechi chache wameonyesha kwenye kutupia.


UBORA WA WACHEZAJI

Kikosi cha Simba kina wachezaji wengi bora - pengine tofauti na timu ambazo wanakutana nazo. Hii ni kutokana na uwezo wa kutimiza majukumu na rekodi mbalimbali walizoweka.

Ukiachana na wachezaji ambao wanacheza mara kwa mara kikosi cha kwanza Simba, wengine waliobaki ukiwapeleka katika timu nyingine wanacheza kikosi cha kwanza na kuwa tegemeo. Uwezo kama anaoonyesha Kagere, Hassan Dilunga, Said Ndemla na wengineo sio wachezaji wa kutegemewa Simba, lakini katika vikosi vingine ni mastaa.

Kutokana na ubora wa wachezaji Simba wameacha tena kumtegemea Jonas Mkude ambaye alipokuwa akikosekana walipagawa. Simba hii ni bora maeneo yote.

Mchezaji kama Clatous Chama aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu uliopita, msimu huu mpaka sasa ametoa pasi za mwisho 14 na kufunga mabao nane, Luis Miquissone, Larry Bwalya, Mohammed Hussein, Shomary Kapombe, Aishi Manula na wengine wako moto kutimiza majukumu yao na kuonyesha ubora vitu ambavyo ni nadra kuviona katika timu nyingine.


BENCHI LA UFUNDI

Kocha Didier Gomes rekodi zake kwenye timu mbalimbali zinaonyesha kuwa amekuwa akichukua mataji. Benchi lake lina mtaalamu wa kusoma wapinzani, Culvin Mavunga ambaye amekuwa akikaa zake jukwaani na kushinda chumbani akiwasoma wapinzani ambao hucheza nao. Hakuna timu nyingine kwenye ligi yenye mtaalamu wa aina hiyo. Simba ina Selemani Matola, kocha msaidizi mzawa ambaye ana uwezo mkubwa wa kufundisha na anaifahamu vizuri ligi ya ndani, ndio maana yupo pia Taifa Stars.

Simba kabla ya Gomes, ilianza msimu na Sven Vandenbroeck ambaye kabla ya kutimkia Morocco aliipa mafanikio kwa kuchukua ubingwa wa ligi msimu uliopita, Kombe la Shirikisho, Ngao ya Hisani na kuifikisha hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.


NGUVU YA MO DEWJI

Tangu alipoingia Simba, bilionea Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ katika misimu minne iliyopita kikosi chake kimeimarika. Wachezaji, benchi la ufundi na waajiriwa wote wanapata stahiki zao kwa wakati - tena muda mwingine zinakuwa pesa nyingi pindi wanapofanya vizuri.

Simba wanaishi katika hoteli kubwa na nzuri mahala popote ugenini wanapokwenda kucheza. Wanasafiri kwa ndege sehemu zenye umbali mrefu, jambo ambalo wachezaji kazi yao inabaki kucheza.

Mo Dewji amefanya usajili wa wachezaji wenye tija Simba kutoka ndani na nje ya nchi ambao wamerahisisha safari ya ubingwa msimu huu na mitatu iliyopita.


HESABU

Simba msimu huu walikuwa na hesabu nzuri kwani katika mechi 32, ambazo wamecheza mpaka muda huu wamefungwa tatu, wametoka sare nne na kushinda 25.

Hesabu zinaonyesha Simba wamepoteza pointi 13 kutokana na kufungwa pamoja na kutoka sare. Kama kungekuwa na timu yenye hesabu ya matokeo mazuri maana yake wangewafikia mpaka kwa pointi.


TIMU NYINGINE

Simba wanatoka Dar es Salaam kwenda kucheza mechi Mwanza wanatumia si zaidi ya saa tatu, wakati Biashara United wakitoka Musoma kwenda Lindi kucheza na Namungo wanatumia siku mbili njiani.

Ni wazi kwa hali hiyo wachezaji wa Simba watakuwa katika hali nzuri ya kucheza tofauti na wale wa timu nyingine wanaotumia muda mrefu njiani na pia wtatumia muda wao mwingi kufanya mazoezi na kupumzika.

Ukiangalia wachezaji na benchi la ufundi la Simba wanapata kila kitu kwa wakati, huku ukiwasikia Mwadui wanalalamika hakuna mishahara kwa miezi minne unaona kuna timu nyingine ziliachwa mbali na vinara wa ligi. Unategemea kuona Yanga wakishindana na Simba, lakini ghafla unasikia matatizo yakiwemo ya kinidhamu - tena ya wachezaji tegemeo zaidi, ni wazi timu hiyo kupambana kushindana na watani inakuwa kazi ngumu.

Kiukweli ukiangalia wachezaji wa Simba wanavyoishi pindi wanapokuwa kambini kujindaa na mechi na hata wanapokuwa nje ya kambi katika maisha ya kawaida ni tofauti na timu nyingine.


UZOEFU

Kikosi cha Simba kimetwaa ubingwa huku wakiwepo wachezaji wazoefu kwenye ligi, wakiwamo walioanza pamoja safari ya mafanikio misimu minne mfululizo.

Wapo kina Erasto Nyoni, Kapombe, Ndemla, Mzamiru Yassin, Tshabalala na wengineo ambao hakuna aliyewahi kuondoka tangu walipoanza safari yao ya mafaniko ya kutwaa mataji ikiwemo hili.

Ukiangalia timu nyingine zimekuwa na ingia - toka ya wachezaji na kushindwa kukaa pamoja ili kuzoeana na kujuana, kwani kila msimu kunakuwa na mabadiliko mpaka katika mabenchi ya ufundi.

Kukosa utulivu kwa timu nyingine hasa ingai - toka ya wachezaji na maboresho ya mara kwa mara kwa benchi la ufundi ni jambo ambalo linakosesha uwepo wa wachezaji wazoefu. Kikosi cha Simba kina wachezaji wazoefu wenye uwezo ambao wamerahisisha safari ya ubingwa kama Bocco na Chama kutokana na rekodi zao katika timu mbalimbali.

Uzoefu wa kucheza mechi ngumu za kimataifa dhidi ya Al Ahly, Kaizer Chiefs na timu nyingine zinawapa ushindani na maandalizi ya kutosha wachezaji wa Simba ambao wakihamishia katika ligi kazi inakuwa sio ngumu kwao.


USAJILI

Miongoni mwa sehemu ambayo imerahisisha safari ya ubingwa wa Simba ni kufanya usajili sahihi kulingana na upungufu ambao waliuonyesha msimu uliopita.

Katika madirisha mawili ya usajili wa ndani Simba walisajili wachezaji nane ambao kati ya hao saba wameonekana kutoa mchango na kufanya vizuri, huku mmoja tu, Perfeck Chikwende mambo hayakumwendea vizuri. Kwenye dirisha kubwa Simba waliwasajili Rally Bwalya, Mugalu na Joash Onyango ambao wameingia katika kikosi cha kwanza na kuwa na msaada katika kikosi.

David Kameta na Ibrahim Ame ambao walisajiliwa katika dirisha kubwa ndio wamekuwa na ingia - toka katika kikosi kutokana na ubora ambao unaonyeshwa na Onyango, Pascal Wawa, Kennedy Juma na Nyoni katika nafasi ya Ame, kama ilivyo kwa Kameta ambaye nafasi yake hutumika zaidi Kapombe.

Katika dirisha dogo, Simba walijiimarisha vyema eneo la kiungo mkabaji walipomsaini Taddeo Lwanga ambaye moja kwa moja ameingia katika kikosi cha kwanza na amekuwa mchezaji wa kutegemewa kutokana na mchango wake.

Ubora ambao ameonyesha Lwanga umewafanya mpaka Simba kumsahau Mkude ambaye ndio alikuwa akicheza mara kwa mara katika eneo hilo.

Simba ni moja ya timu ambazo ilifanya usajili bora kwenye ligi kulingana na upungufu tofauti na timu nyingine ambazo zilisajili wachezaji wengi lakini wachache ndio wamekuwa msaada.