Siku ya Stars na Aggrey Morris

Leo Jumanne, beki wa kati mkongwe Agrey Morris Ambrose ataagwa rasmi kwenye kikosi cha Taifa Stars baada ya kutangaza kustaafu kuichezea timu hiyo baada ya miaka 11.

Morris ambaye ni mchezaji wa Azam alianza kuichezea Stars 2009 huku timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ alianza kuichezea 2004, nayo amestaafu. Baada ya kutangaza kustaafu leo ambapo Stars itacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya DR Congo ndiyo imetengwa pia kama mechi maalumu ya kumuaga nahodha huyo wa Azam, mechi itakayochezwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Morris yaliyofanyika mjni hapa ambapo ameeleza mambo mbalimbali katika soka.

“Nilianza kucheza timu za madaraja ya chini hapa Zanzibar na baadaye nilijiunga na timu ya Mafunzo FC chini ya kocha Mshenga (marehemu), huyu ndiye aliyeniona hasa kwamba nina kitu cha kufanya kwenye mpira.”

“Kocha huyo nakumbuka alituchagua wacheza saba ambapo nilicheza kwa miaka mitano na kujiunga Azam FC. Nikiwa Mafunzo nilibahatika kuichezea kombaini ya Zanzibar ambayo ilishiriki mashindano ya Karume Cup.

“Mashindano hayo sidhani kama yapo mpaka sasa hivi, ingawa wakati wetu tulichukua ubingwa, baadaye pia nilichaguliwa kuichezea Zanzibar Heroes ambayo nimeichezea kwa miaka 10,” anasema ambaye alijiunga na Azam kwenye dirisha la usajili la 2009.

KUMBE SIMBA WALIMTAKA

Kocha wa zamani wa Azam FC, Mohammed King King anasema baada ya mchezaji huyo kusaini kwao akiwa kwenye boti kurudi Zanzibar, Simba waliinua simu wakitaka huduma yake.

“Alipigiwa simu na (anamtaja kigogo) wa Simba kutaka kwenda Dar kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo, hapo hapo Morris alimjibu tayari amesaini Azam, basi habari ikaishia hapo.

“Pengine wasingemsajili Azam angeenda Simba, lakini alikokuwa amesaini ndiko kulikuwa sehemu sahihi kwa Morris maana hajawahi kuhama wala kufanya vibaya, sasa ni kama nyumbani kwao,” anasema King akisifu jitihada za mchezaji huyo kwenye mazoezi binafsi.

SABABU ZA KUSTAAFU

Hata hivyo, akizungumzia dhamira yake ya kustaafu, Morris anasema: “Ni wakati wa kuachia kijiti kwa wengine kama nilivyoachiwa mimi, umri umeenda na nimecheza kwa muda mrefu, naamini mchango wangu nilioutoa ni mkubwa pia. Ni wakati wa vijana nao kuonyesha kile walichonacho sasa maana wapo wengi wazuri wanaocheza nafasi kama yangu.

“Sijastaafu Stars pekee, bali hata Zanzibar Heroes ambapo mara ya mwisho niliitwa kikosini, lakini nilimweleza kocha kuwa sasa ni wakati wa kustaafu ili wengine wacheze maana hata Zanzibar kuna vijana wengi wazuri wenye uwezo wa kucheza kwa mafanikio makubwa, kocha All Bushiri alinielewa hilo.”

VIPI KUHUSU AZAM

Anasema ana mkataba wa mwaka mmoja na miezi mnane na Azam FC, hivyo ukimalizika nako atastaafu rasmi na kufanya shughuli zingine ingawa alianza kusomea mambo ya ukocha.

“Hata huku mkataba wangu ukimalizika nastaafu na kufanya mambo mengine, naamini Azam ina wachezaji wengi wazuri wanaoweza kucheza kwenye ubora mkubwa kama mimi ama zaidi,” anasema Morris ingawa hakutaka kuweka wazi nini atafanya baada ya kustaafu soka.

Kwa upande, King anasema: “ (Morris) ana kila sababu na sifa za kuwa kocha, ameanza kusoma ukocha ngazi ya awali hivyo ni vyema akistaafu aendelee na kazi ya ukocha ili kuwasaidia vijana wenzake, hicho ndicho kitu pekee ambacho kitakuwa zawadi kwa taifa.” Hata hivyo, habari ambazo Mwanaspoti limezipata kutoka ndani ya Azam ni kwamba mchezaji huyo akistaafu hata kwenye klabu yake atakuwa kocha, huku akiwa ndani ya Azam hiyo hiyo.

CHANGAMOTO

Moja ya changamoto ambayo imewahi kumkuta na kumuweka katika wakati mgumu beki huyo ni pale alipotuhumiwa kuihujumu Azam ingawa yeye anasema zipo nyingi na zinakatisha tamaa.

“Usipokuwa na moyo wa ujasiri unaweza kukata tamaa kucheza mpira, lakini changamoto ni nyingi sana ambazo kama mchezaji ili uwe bora ni lazima ukabiliane nazo.

“Binafsi nimekutana nazo nyingi hata kabla sijaingia Azam, yaani kucheza soka Bara, nilipokuwa huku (Zanzibar) nikiwa timu ya kombaini ya Karume niliwahi kuvuliwa jezi nikiwa benchi na kuvalishwa nguo nyingine, ilikuwa kama ovaroli, kiukweli niliumia sana.

“Sitaki kumtaja huyo mtu ila namshukuru sana mama yangu alikuwa akinipa sapoti kubwa na kunitia moyo hasa pale anapoona nataka kukata tamaa, mama ndiye aliyenifanya niupende mpira zaidi ingawa hata huyo mchezaji mwenzangu aliniongezea hatua kwa kunipa changamoto hizo za kunikatisha tamaa kwamba siwezi,” anasema beki huyo.

PACHA BORA MUDA WOTE

Anawataja Kevin Yondani na Nadir Haroub “Canavaro’ kuwa ndio walikuwa pacha wake bora akiwa Stars. Wachezaji hao wawili waliichezea Yanga ambapo Canavaro alistaafu soka na ni neneja wa Stars kwa sasa wakati Yondani yupo Polisi Tanzania.

“Nilikuwa nafurahi zaidi nikicheza na mmoja wapo kati ya Yondani au Canavaro, nilicheza kwa kuufurahia zaidi mpira, kiukweli hizo ndizo pacha zangu bora za wakati wote.”

USHINDANI WA NAMBA

Morris anasema alivyotua Azam na Stars kote alikutana na ushindani wa namba kwani aliwakuta nyota waliokuwa kwenye viwango vya juu zaidi.

“Azam walikuwepo kama kina Said Swedy ‘Kussy’, Said Morad, Atudo kutoka Kenya, David Mwantika, Canavaro na sasa wapo kama Yakubu Mohamed, Daniel Amour, Abdallah Kheri na Oscar Masai.

“Stars nilikutana nao kama Kussy, Canavaro, David Naftal, Juma Nyosso na wengine ambao kiukweli walikuwa vizuri lakini ili ufanikiwe ni lazima uzingatie mafunzo ya kocha pamoja na kujiongeza binafsi,” anasema. “Kikubwa ambacho nilikuwa nakipenda Stars ni wakati ule wa kocha Mbrazil Marcio Maximo alipenda kuwaandaa wachezaji kwa ajili ya kurithi nafasi za watu kwa baadaye na hivyo ndivyo inavyotakiwa, mchezaji anapaswa kuandaliwa kwa malengo ya baadaye na sio kubadilisha badilisha tu wachezaji, mpira unaandaliwa ili uwe katika ngazi nzuri.

“Niliowakuta walipewa nafasi wakati wengine tukiendelea kujifunza hivyo tulivyoanza kucheza tayari tulikuwa tumeandaliwa maana tulijifunza pia kwa waliotutangulia, ndiyo wachezaji walikuwa imara zaidi.”

HALL KOCHA BORA

Akizungumzia makocha waliomfundisha, anaeleza kuwa amepitia kwa wengi, lakini Stewart Hall ndiye kocha wake bora wa nyakati zote.

“Hall alivyokuja alikuta wachezaji hatujui lolote kuhusu mpira ingawa tunacheza, alitufundisha zaidi ya ukocha wake tukaujua mpira na tukaufurahia, yaani Azam alianza nayo kama akademi tu hivyo tulielewa mambo mengi.

“Huyo kwangu atabaki kuwa kocha bora wa nyakati zote, anajua mpira na anajua kuufundisha na namna gani mchezaji anatakiwa kuwa, wakati wa mazoezi na wakati wa mechi, mafunzo yake tuliyajua vyema na kuyafanyia kazi kwa mafanikio makubwa.”

OKWI NA CHIDIEBERE

Matukio ya kuwachezea rafu wachezaji yapo katika soka. Hali hiyo iliwahi kumkumba Morris kwa kuwachezea rafu nyota Abisarim Chidiebere wakati huo anaichezea Stand United na Emmanuel Okwi akiwa Simba, yeye anayakumbuka na kueleza: “Ni matukio ambayo yaliniumiza sana maana kila upande ulinishambulia kana kwamba nilifanya kusudi wakati ukweli haukuwa hivyo, hakuna mtu anayeingia uwanjani na lengo baya kumuumiza mwenzake labda kama ana tatizo la akili.

“Hayo matukio sikuyakusudia ingawa nilishambuliwa mno na kila kona, kuna wachezaji wengine wanafanya matukio uwanja kama niliyowahi kufanya, lakini watu wanapiga kimya kana kwamba hayapo na hayaonekani, hivyo nawaomba wadau wa soka wawe waelewa kwa kila mchezaji anayefanya kosa uwanjani kwa kumuumiza mwenzake si kwamba anakusudia,” anasema.

KUYUMBA KWA AZAM FC

Azam FC ni timu ambayo imewekeza kwa kiasi kikubwa, lakini haina mafanikio makubwa hasa kwenye Ligi Kuu Bara ukiachana na ubingwa waliowahi kuuchukua kwenye mashindano ya Kagame na Kombe la Mapinduzi.

“Ligi Kuu tumetwaa ubingwa mara moja lakini mashindano mengine tumetwaa mara nyingi hayo pia ni mafanikio, malengo ya Azam ni kitwaa ubingwa wa ligi hivyo yapo na yanaendelea kupambaniwa ila tu hatujayafikia kama ilivyokusudiwa.

“Ni kweli Azam kwa sasa haina matokeo mazuri, lakini katika soka ni kitu ambacho kipo hata ukiangalia timu za Ulaya zina uwezo mkubwa kipesa na zimewekeza, lakini ukija kweli ligi matokeo yao si mazuri, naamini Azam itakaa sawa na kupata kile kilichowekwa kwenye malengo,” anasema

MAFANIKIO

Morris anasema kupitia soka amepata mafanikio mengi ingawa kwake si rahisi kuyaanika, akisisitiza kuwa: “Mpira umenipa mafanikio mengi na hii yote ni kwa sababu nimeuheshimu na umeniheshimu, na ndio maana pia nimecheza kwa muda mrefu, najivunia hilo ingawa pia si rahisi kuyaanika mafanikio yangu binafsi bali ieleweke tu kuwa soka limeninufaisha.”