Prime
Si mchezo huyu kapatia, yule kachemsha

SIO kazi ndogo kumuona mchezaji anang'ara ndani ya vikosi vya Simba, Yanga na Azam, lazima afanye kazi ya ziada kuonyesha kiwango cha kujitofautisha na wengine, hiyo inatokana na aina ya wachezaji wanaowasajili.
Timu hazishiki top 3 kwa bahati mbaya, waandaa vikosi ambavyo vina wachezaji wa viwango vya juu, hivyo ushindani wao unaanzia kwenye namba wenyewe kwa wenyewe kabla ya kukutana timu pinzani.
Kabla ya kuanza msimu na baada ya kufunguliwa kwa dirisha dogo kwa msimu ulioisha, wapo wachezaji waliotabiriwa kufanya makubwa, ajabu wamejikuta wanakwama.
Mwanaspoti linakuchambulia mastaa ambao wamefanya vizuri ndani ya vikosi hivyo na wengine mambo yao yamekwenda sivyo, yaani waliofunika na wale waliochemka, hivyo kuwa na deni iwapo watabahatika kubakizwa kwenye vikosi vyao kwa msimu ujao.
TUISILA KISINDA (LUZA)
Winga huyo maarufu kama TK Master, wakati anaondoka mwishoni mwa msimu uliopita kwenda kujiunga na klabu ya RS Berkane ya Morocco, kiwango chake kilikuwa cha juu, lakini Yanga ilipoamua kumrejesha kwenye dirisha dogo kwa mkopo mambo yalienda kombo.
Ile kiu ya mashabiki ya kumuona Kisinda anayeteleza kama kambale kwenye maji, ilikuwa tofauti na badala yake alionekana wa kawaida, japo kocha Nasreddine Nabi alipenda kumtumia kutokana na mbinu zake kiufundi, lakini ukweli ni kwamba jamaa alichemsha mbaya tofauti na matarajio.
AZIZ KI (LUZA)
Usajili wake ulitikisa wakati Yanga inamchukua kutoka Asec Mimosas, baada ya kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF na utambulisho wake ulifanywa usiku wa manane huku wakiweka utambulisho wa kufuru, pamoja na hilo bado hajacheza kila kiwango ambacho mashabiki walikitarajia na kwa kikosi cha Nabi aliyekuwa panga pangua ni kinara wa mabao 17, Fiston Mayele na kipa Diarra.
IBRAHIM BACCA (WINA)
Baada ya kocha Nasreddine Nabi, kumpa nafasi Bacca ameweza kuitendea haki na alifanikiwa kucheza kwa kiwango cha juu na ghafra akawa habari ya mjini na kugeuka kipenzi cha mashabiki.
JOYCE LOMALISA (WINA)
Kwa mara ya kwanza wakati anajiunga na Yanga, akitokea Sagrada Esperança ya Angola, Lomalisa raia wa Kongo, hakuwa na mwanzo mzuri na nafasi yake aliitawala Shomari Kibwana, baadaye akarejesha kwa kishindo na akawa anatumika zaidi na aliisaidia timu kwa kupeleka mashambulizi.
JESUS MOLOKO (WINA)
2021/22 hakuwa kwenye kiwango kikubwa kilichopelekea kilele za mashabiki kutomuelewa na kuna kipindi zilitawaliwa tetesi za kutaka kutemwa, akaamua kujitafuta ambapo msimu ulioisha ulikuwa mzuri kwake na akawa muhimu kikosini.
MUDATHIR YAHYA (WINA)
Wakati anasajiliwa alikaa nje miezi sita baada ya kuachana na Azam FC, Mudathir licha ya uwezo wake kujulikana mkubwa hakutarajiwa angeaminiwa moja kwa moja ndani ya kikosi hicho, lakini alifanyika mchezaji muhimu na alicheza kwa kiwango cha juu.
YANNICK BANGALA (LUZA)
Ikumbukwe 2021/22 ndiye alikuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara, tofauti na msimu huu ambapo hajabahatika kuchukua tuzo ya aina yoyote, ingawa katika hilo, Nabi aliwahi kumkingia kifua akisema alimtumia kwenye nafasi nyingi zaidi na kumfanya mchezaji huyo kuchoka.
BERNARD MORRISON (LUZA)
Ni kama ana mechi na mechi za kufanya maajabu, haizuiliki kwamba Morrison anajua mpira, lakini kwenye msimu ulioisha hakuwa na namba ya kudumu kikosi cha kwanza, jambo linalomfanya awe na nafasi finyu ya kuendelea kusalia kikosini hapo, kwani tayari kamaliza mkataba wake.
CLEMENT MZIZE (WINA)
Si rahisi mchezaji anayepandishwa kikosi B kwa timu kama ya Yanga, akapata nafasi ya kucheza kama yeye, ili kuonyesha alikuwa na msimu bora amefanikiwa kunyakua tuzo ya U-20 ya Ligi Kuu Bara.
SIMBA
NELSON OKWA (LUZA)
Namna lilivyokuwa linatamkwa kwa ukubwa jina la Okwa kwenye usajili wa Simba msimu uliopita, uliwafanya mashabiki kujenga imani naye, ajabu akaishia kutolewa kwa mkopo kwenda Ihefu na mwisho wa siku kuachana naye.
AUGUSTINE OKARH (LUZA)
Alifunga mabao manne na asisti moja kwenye msimu wake wa kwanza Simba na kisha kuondoka kiwango chake kikiwa chini na kusahaurika masikioni mwa mashabiki wake, tofauti na alivyojiunga nao akitokea klabu ya Bechem United.
VICTOR AKPAN (LUZA)
Wakati yupo Coastal Union ya Tanga, kiwango chake kilikuwa cha juu, lakini baada ya kujiunga na Simba hakuwa na nafasi kikosini na kutolewa kwa mkopo Ihefu ambako pia hakuweza kufanya vizuri.
HABIBU KYOMBO (LUZA)
Kama kuna usajili ulipondwa mitandaoni na mashabiki wa Simba, ulikuwa wa straika Habibu Kyombo akitokea Mbeya kwanza ambako alimaliza na mabao saba, pamoja na hilo alishindwa kujitetea kwa kuonyesha kiwango chake akiishia kufunga mabao mawili.
PETER BANDA (LUZA)
Ni kama kuchukuliwa mchezaji chipukizi anayetakiwa kukua kulimlemaza Banda,kwani tangu ajiunge Simba takribani misimu miwili sasa hakuweza kuonyesha uwezo wa moja kwa moja kama ilivyo kwa Luis Miquissone aliyeuzwa na klabu hiyo Al Ahaly ya Misri ambaye huduma yake inakumbukwa hadi sasa na mashabiki wa Simba.
JEAN BALEKE (WINA)
Anacheza Simba kwa mkopo kutoka TP Mazembe, tangu ajiunge nao dirisha dogo alianza na baraka za kucheka na nyavu kwenye mechi yake ya kwanza na Dodoma Jiji na akawa na muendelezo mzuri wa kutupia mabao.
JONAS MKUDE (LUZA)
Haipingiki Mkude ni mkongwe ndani ya kikosi cha Simba, kutoka kwenye kikosi cha kwanza na msimu ulioisha kuonekana kwa nadra uwanjani, mkataba wake umemalizika na imekuwa ngumu kumuongezea mwingine kirahisi na ikitokea akabahatika kubaki biashara yake ya kukunja kibunda kirefu ni mtihani.
ISMAIL SAWADOGO (LUZA)
Timu yake ya mwisho kabla ya kujiunga ilikuwa ni Difaa El Jadid ambako alikuwa hapati nafasi ya kucheza, baada ya kumchukua dirisha dogo ilitarajia angeongeza nguvu kikosini, ajabu ni mchezaji aliyecheza kwa kiwango cha chini kabisa.
Moses Phiri (wina)
Isingekuwa majeraha ambayo yalimkumba Moses Phiri huenda angekuwa na mabao zaidi ya 10 aliyomaliza nayo msimu,kwani baada ya kupona tayari Baleke alikuwa kwenye kiwango kikubwa, kwa vyovyote kocha anayesaka matokeo asingeweza kujiweka lehani.
SAID NTIBAZONKIZA (WINA)
Ni mchezaji aliyecheza kwa kiwango kikubwa na wakati Ligi Kuu inaelekea ukingoni aliwapa burudani mashabiki wake, akilingana mabao ya kufunga 17 na Fiston Mayele wa Yanga na alijikusanyia tuzo kwenye vipengele mbalimbali.
WENGINE HAWA HAPA
Baadhi waliofanya vizuri katika timu nyingine kamani Idris Mbombo, Ayubu Lyanga, Abdu Seleman 'Sopu', James Akaminko, huku Singida Big Stars iliyomaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ni Bruno Gomes, Meddie Kagere, Pascal Wawa na Deus Kaseke.
Wengine ambao ni luza ni Gadile Michael,Nassoro Kapama, Kennedy Juma, Mohammed Mussa, Mohamed Outtara (Simba), Erick Johora, Abdallah Shaibu 'Ninja', David Byrason,Dickson Ambundo,Chrispin Ngushi, Mamadou Doumbia (Yanga), Amissi Tambwe (SBS) na Cleophace Mkandala, Ali Ahamada, (Azam).