Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simchimba: Nazitaka Simba, Yanga   

Muktasari:

  • Mmoja wa wachezaji waliong’ara kwenye ligi hiyo ni mshambuliaji wa Geita Gold, Andrew Simchimba ambaye amemaliza kinara wa kufumania nyavu akifunga mabao 18 sawa na Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Abdulaziz Shame wa TMA wakifuatiwa na Eliud Ambokile wa Mbeya City (12) na Yusuph Mhilu wa Geita Gold (10).

LIGI ya Championship msimu huu ilimalizika Mei 11, mwaka huu, kwa timu za Mtibwa Sugar (mabingwa) na Mbeya City kupanda moja kwa moja Ligi Kuu Bara, huku Stand United na Geita Gold zikisubiri kucheza mechi za mtoano (play-off).

Mmoja wa wachezaji waliong’ara kwenye ligi hiyo ni mshambuliaji wa Geita Gold, Andrew Simchimba ambaye amemaliza kinara wa kufumania nyavu akifunga mabao 18 sawa na Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Abdulaziz Shame wa TMA wakifuatiwa na Eliud Ambokile wa Mbeya City (12) na Yusuph Mhilu wa Geita Gold (10).

Licha ya ukurasa wa Ligi ya Championship kuonyesha straika huyo amefunga mabao 18, lakini kwa mujibu wa takwimu za  Geita Gold na mchezaji mwenyewe zinaonyesha amefunga mabao 19. Nyota huyo aliibuka mchezaji bora wa Ligi ya Championship mara mbili akifanya hivyo Oktoba 2024 na Februari 2025 kutokana na kiwango kizuri alichoonyesha yakiwemo mabao aliyotupia.

Simchimba aliyejiunga na Geita Gold mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja, alifunga mabao hayo katika mechi 11 ikiwemo hat trick moja na mabao mawili kwenye mchezo mmoja katika mechi sita - akifunga dhidi ya Transit Camp mabao matatu, Songea United (2), Cosmopolitan (2), Mbeya Kwanza (2), Green Warriors (2), African Sports (2), Transit Camp (2), Kiluvya United (1), Cosmopolitan (1), Bigman FC (1) na Polisi Tanzania (1).

Mshambuliaji huyo wa zamani wa KMC na Ihefu amepiga stori na Mwanaspoti na kueleza mambo mengi ikiwemo shauku yake ya kucheza Ligi Kuu Bara na namna alivyopambania ndoto na malengo huku akidai amefunga mabao 19 licha ya waendeshaji wa ligi kumpa 18.


SIMBA, YANGA FRESHI

Kama ilivyo kwa wachezaji wengi nchini, Simchimba anasema hawezi kuiacha nafasi ya kucheza timu kubwa za Simba na Yanga itakapotokea huku pia akiwa tayari kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

“Ndiyo kitu ambacho nimeshajiwekea nafasi ikitokea ya kucheza timu kubwa nitacheza. Hakuna mchezaji asiyetamani kucheza timu kubwa naamini ipo siku nitacheza. Nitasogea hapo sehemu nzuri zaidi haijalishi ni timu gani," anasema mchezaji huyo.

“Hapa kinachofuata ni kurejea Ligi Kuu hamna kingine zaidi. Ni kufanya mipango nirudi Ligi Kuu msimu ujao. Mkataba wangu na Geita Gold umemalizika na tayari timu zinaonyesha nia ya kunihitaji. Mpaka sasa hivi nimefuatwa na timu tatu na zote ni za Ligi Kuu.”

UTATA IDADI MABAO YAKE

Simchimba anasema amefunga mabao 19 na siyo 18 kama inavyochapishwa katika kurasa za Ligi ya Championship, huku akiomba wasimamizi wa ligi hiyo kushughulikia jambo hilo kwani bao moja ambalo halijawekwa ni muhimu ili ashinde tuzo ya mfungaji bora.

“Nimefunga mabao 19. Kuna goli moja nilifunga halafu halikuwekwa kwenye orodha yangu, alipewa mchezaji mwingine na hiyo inshu inajulikana kabisa, lakini nashangaa wakitoa wanaandika nina mabao 18. Sijajua shida ni nini,” anasema Simchimba.

Anaongeza kuwa, “nilifunga mabao mawili pale Mlandizi tulicheza na Cosmopolitan, alipewa mtu mwingine japo goli nilifunga mimi (alifunga mabao mawili katika ushindi wa 4-0). Ni goli muhimu ambalo linanipa tuzo sasa sijui nafanyaje.”


MAJERAHA YAMPELEKA CHAMPIONSHIP

Anasema safari ya kutoka Ligi Kuu kwenda Championship kujitafuta ilitokana na majeraha ya nyonga aliyoyapata akiwa KMC na kumuweka nje miezi miwili, hivyo alihitaji sehemu ambayo atapata muda wa kutosha wa kucheza ili kurejesha kiwango.

“Kuja kwangu Championship kulikuwa na maana sikuja tu, nilihitaji kupata mechi nyingi kwa sababu Ligi Kuu nisingepata nafasi kama niliyopata huku. Niliona hii sehemu yangu nzuri ya kurudisha kiwango changu nikiamini nitapata nafasi na kurejea Ligi Kuu nikiwa vizuri kabisa,” anasema nyota huyo.

Anasema katika mchezo wa soka wachezaji wanapopata majeraha hawapaswi kukata tamaa na kupoteza mwelekeo, bali wanatakiwa kuwa na subira, kukubali hali waliyonayo na kuwa wavumilivu na kusimamia malengo.

“Kwa mfano mimi ningesema labda nimekuja Championship nijikatie tamaa nione nimeshafeli nisipambane tena ndiyo ningezidi kujididimiza huku chini, lakini nikaamua kusimamia malengo yangu,” anasema Simchimba.

“Na unapofanya uamuzi kama hu hautakiwi kumwangalia mtu usoni, unajua watu wengi waliongea maneno kwamba nitakuwa ndiyo nimefeli, lakini hapana nikasema hili jambo la muda tu nimetoka kwenye majeraha.”


MANENO YAMPA UFUNGAJI BORA

Anasema ukali wa kucheka na nyavu na ubora wa kiwango chake haukuja tu kwa wepesi, isipokuwa kwa kujituma na kutaka kuwaonyesha baadhi ya watu walioamini kuwa amekwisha na hawezi kucheza tena Ligi Kuu.

“Maneno ya watu muda mwingine ni mazuri yanakupa tiketi hayakunifanya nikate tamaa mtu anaamini umefeli anaongea maneno yake kisa umetoka Ligi Kuu, huku ni aina tu ya maisha siku nyingine unakosa au unapata,” anasema Simchimba.

“Sikuja huku kisa nimefeli nilikuja kuboresha kiwango changu kuwa kama zamani, niliamua kujituma tu nikihitaji nifike pale juu huku nafanya tu kama njia. Kufanikiwa kunakuwa na njia nyingi kila mtu anapita njia yake, huwezi kujua ya kesho tusikate tamaa.”

Simchimba mwenye mke na mtoto mmoja anasema familia yake imekuwa moja ya sababu iliyomfanya kupambana na kupata mafanikio aliyonayo msimu huu kwenye Ligi ya Championship.

“Unajua watu wengi unakuta wanakutazama wengine wanakutegemea kwahiyo unasema nikifeli mimi hata hawa walioko nyuma yangu wananitegemea familia na ndugu nawaangusha,” amesema mshambuliaji huyo.

“Unaona bora utie bidii kwasababu ukipambana lazima upate, ni bora upambane ionekane huyu kapambana na amekosa kuliko kutojituma kabisa, kwahiyo ni kitu ambacho nilikuwa nawaangalia sana watu ambao wako nyuma yangu.”


GEITA GOLD ILIKWAMA HAPA

Simchimba anaamini kwamba mabadiliko ya benchi la ufundi baada ya kuondoka kwa Kocha Mkuu, Amani Josiah, aliyetimkia Tanzania Prisons na ujio wa Mohamed Muya ni miongoni mwa sababu zilizowayumbisha na kupoteza mwelekeo kupanda Ligi Kuu moja kwa moja, huku kwa sasa wakipamana kupitia mechi za mtoano (play off).

“Unaweza ukasema mabadiliko ya kocha yalichangia kwa sababu alivyoondoka tu mambo yakabadilika, lakini huko hatuwezi kuangalia sana ni mimi binafsi ninavyoona. Inawezekana tu ni upepo wa timu wakati mwingine mnakosa ari ya ushindi,” anasema Simchimba.

“Lakini kusema ukweli tulikuwa na timu nzuri sana, wachezaji bora, lakini tumeshindwa kufikia malengo unaweza ukaanza vizuri ukamaliza vibaya.”

Licha ya changamoto ya klabu kutotimiza malengo, lakini anaamini ulikuwa msimu bora na wa mafanikio kwake binafsi tangu ashiriki Ligi ya Championship.