Senzo aja na mambo mawili Yanga

Senzo aja na mambo mawili Yanga

Muktasari:

MSHAURI wa uongozi wa Yanga, Senzo Mazingisa ametangaza mambo mawili ya kufurahisha kwa mashabiki wa klabu hiyo

MSHAURI wa uongozi wa Yanga, Senzo Mazingisa ametangaza mambo mawili ya kufurahisha kwa mashabiki wa klabu hiyo. Kwanza amesema ujenzi wa uwanja wa Yanga uliopo Kigamboni; “Kila kitu kimeenda sawa baada ya kamati kukaa na kuona nini ambacho kinaendelea, tumeshatengeneza tenda hivyo wanaohitaji wanatakiwa kuja na kuomba ili tenda iendelee.

“Upande wa kuanzia tutaanza na uwanja wa nyasi halisi, bandia na bwawa la kuogelea, hosteli pamoja ofisi kisha mengine yataendelea,” alisema ambaye wachambuzi wa soka wanasema moja ya mafanikio yake ya awali Yanga ni kuitoa timu hotelini na kuipeleka kambi ya Avic Town na kukamilisha duka la jezi rasmi klabuni.

Kama inavyoonekana kwenye picha ya ukurasa wa mbele wa gazeti hili la Mwanaspoti, Senzo alisema wanataka kutengeneza uwanja ambao utakuwa wa aina yake na watawekeza hapo kwa heshima ya timu ya wananchi na mashabiki wake. Alisema wanaamini watapata wataalam sahihi wa kuutengeneza na kutoa kitu cha mfano kama walivyopania. Kama Yanga itakamilisha uwanja huo itafuata nyayo za Azam na Simba kwa jijini Dar es Salaam ingawa Senzo amesisitiza kwamba, miundombinu yao itakuwa ya kisasa na yenye ubunifu mkubwa. Lakini, akaongeza kuwa; “Jumatatu au Jumanne natakiwa kwenda Hispania kuchukua ripoti ya mabadiliko na kuirejesha Tanzania, ni ripoti kubwa ambayo haiwezi kutumwa kwa barua pepe, lazima ichukuliwe kwa mkono na tupate maelezo yake. Hili ni jambo zuri na nadhani Desemba Mosi tutakaa na kuwaambia nini ambacho kinaendelea, lakini hii ni baada ya kukaa katika kamati zetu.

“Mabadiliko kiukweli yanaendelea vizuri kwa sababu kila kitu kinaenda sawa mpaka sasa, tutaenda watu wawili kuchukua ripoti yetu,” alisema Senzo ambaye ni Ofisa Mtendaji wa zamani wa Simba.

KUHUSU MORRISON

Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela amelikumbusha Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) juu ya majibu ya kesi zao walizopeleka.

“Sisi hatuna tatizo na TFF, lakini kuna kesi ya Kabwili (Ramadhan) na tulipeleka PCCB (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) lakini TFF tunawaomba warejeshe majibu kwani huku sisi tulishapewa majibu,” alisema. Kesi ya Kabwili ilikuwa ni madai kuwa amerubuniwa na baadhi ya viongozi wa soka ili aihujumu Yanga kwenye mechi dhidi ya Simba. “Suala la pili ni kesi ya Morrison, sisi tulizungumza wazi kuwa mkataba sio sahihi ni batili, tuliomba tupewe majibu lakini hatujapata mpaka sasa.

“Shaka yetu ni Desemba 15 dirisha dogo linafunguliwa hivyo wanaweza kubadilisha mkataba, tunawaomba TFF waitishe kesi hii mapema ili isiwe kabla ya dirisha dogo kufunguliwa.

“Jambo lingine ni kuhusu propaganda za soka zinazoendelea, Yanga ni timu imara, viongozi imara na wafadhili imara ndio maana hatujapoteza mchezo mpaka sasa.”

………………………………………………………………………………………….

Na THOMAS NG’ITU