Robertinho, Nabi wapo kamili gado

NI mechi za kisasi!! Wawakilishi wa Tanzania, Simba na Yanga watakuwa na kazi za kufanya  leo, Jumamosi na Kesho, Jumapili kupigania nafasi ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika huku kila mmoja akiwa na hesabu zake.

Simba ya Roberto Oliveira 'Robertinho' ndio watakuwa wa kwanza kutupa karata yao dhidi ya Horoya leo saa 1:00 usiku kwenye Ligi ya Mabingwa wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Guinea huku Yanga ikifuata Jumapili kwenye Shirikisho kucheza dhidi ya vinara wa kundi lao (D), Monastir.

Kwenye michezo mitano iliyopita, takwimu zinaonyesha kuwa Horoya ambao ni vinara wa Ligi Kuu Guinea msimu huu, wanawastani wa kuruhusu bao kwenye kila mchezo kwani wamefungwa jumla ya mabao matano huku yote yakiwa dhidi ya Raja Casablanca.

Walifungwa kwenye mchezo wa kwanza mabao 2-0 nchini Morocco na walipokuwa nyumbani kwenye mchezo wao wa mwisho kwenye hatua ya makundi wakatandikwa mabao 3-1, takwimu hizo zinaonyesha kuwa wababe hao wa Guinea wanafungika kipindi cha kwanza kwani kati ya mabao waliyoruhusu matatu walifungwa kipindi hicho.

Ukirejea hata kwenye michezo yao ya Ligi Kuu Guinea ambayo ni maarufu kama Ligue 1, unaweza kuona mabao manne waliyoruhusu robo tatu wamefungwa kipindi cha kwanza.

Hivyo Robertinho na vijana wake wanapaswa kutumia mwanya huo, licha ya kuwa Horoya imekuwa ikiruhusu mabao hasa kipindi cha kwanza, ni timu ambayo inaweza kukufunga muda wowote hiyo inatoa picha kuwa ukuta wa Simba unaoongozwa na Henock Inonga na Joash Onyango unatakiwa kuwa macho muda wote wa mchezo.

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' anaamini kuwa  Simba inaweza kutinga hatua ya robo fainali kulingana na maandalizi ambayo wamekuwa nayo, "Hakuna cha kuturudisha nyuma, tutacheza kama timu kuhakikisha tunavuka hatua ya makundi, hii ni nafasi yetu, tunapaswa kuitumia vizuri mbele ya mashabiki zetu ambao watakuwa wakituunga mkono, heshima yetu kwa wapinzani wetu ni kubwa lakini hilo haliwezi kutuzuia kushindwa kutekeleza mpango wetu,"

Robertinho anataka kumaliza shughuli dhidi ya Horoya ili mchezo wao wa mwisho katika hatua ya makundi dhidi ya Raja Casablanca uwe wa kulinda heshima tu.


TISHIO HOROYA
Pape Abdou N'Diaye ni miongoni mwa wachezaji hatari wa Horoya, nyota huyo wa Kimataifa wa Senegal ndiye aliyefunga mabao yote ya timu hiyo kwenye hatua ya makundi nya Ligi ya Mabingwa Afrika, moja ikiwa dhidi ya Simba na lingine, Raja Casablanca.

MSIMAMO KUNDI C
                             Pld     W      D       L        GF        GA         Pts    
1. Raja CA (A)     4         4      0      0         13         1         12    
2. Simba               4        2       0      2           2          4           6      
3. Horoya              4        1       1      2          2           5           4        
4. Vipers                4        0       1      3          0           7           1

Ufunguo:
(A)- Imefuzu

MECHI ZILIZOSALIA  
Machi 18
Vipers Uganda    v     Raja CA    
St. Mary's-Kitende, Entebbe
Mwamuzi: Mohamed Athoumani (Comoros)

Simba v    Horoya
Kwa Mkapa, Dar es Salaam
Mwamuzi: Mohamed Adel (Misri)

Machi 31 – Aprili 1
Raja CA Morocco    v   Simba
Mohammed V, Casablanca

Horoya  v Vipers
General Lansana Conte, Conakry


WAJE TUMALIZANE
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi anaamini kuwa kikosi chake kinaubora wa kuifunga US Monastir licha ya kwamba kwenye mchezo wa kwanza Tunisia walipoteza kwa mabao 2-0.

"Tunatakiwa kuwa kwenye kiwango chetu, ni jukumu la kila mchezaji kutoa zaidi ya asilimia 100 kwa ajili ya timu, hakuna ambacho kinaweza kushindikana," alisema.

Takwimu zinaonyesha kuwa US Monastir ni timu ambayo inafungika kipindi cha pili kwani kwenye mabao mawili ambayo wamefungwa ndani ya michezo mitano iliyopita yote ni kipindi hicho na ilikuwa, Februari 15  dhidi ya Ben Guerdane kwenye Kombe la Tunisia (1-0) na Februari 19 dhidi ya Real Bamako (1-1).

Licha ya Yanga kufungwa na  US Monastir kwenye mchezo wake wa kwanza kwenye hatua ya makundi, ilizinduka na kufanya vizuri kwenye michezo mitatu mfululizo ambayo imeifanya timu hiyo kupewa nafasi ya kuvuka hatua hii ya makundi.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, wameonyesha ni timu yenye uwezo wa kufunga vipindi vyote kwani kwenye mabao 10 waliyofunga kwenye michezo yao mitano iliyopita kwenye mashindano yote sita ilikuwa kipindi cha pili huku manne ikiwa cha kwanza.


TISHIO US MONASTIR
Boubacar Traore wa Mali ndiye mshambuliaji tisho wa wapinzani hawa wa Yanga, wakati kwa Wananchi, Fiston Mayele akiweka kambani mabao mawili kwenye hatua hii ya makundi, jamaa ametupia mabao matatu na ndiye kinara kwa timu hiyo.

Mbali na Traore, Monastir imekuwa ikimtegemea pia Zied Aloui ambaye kwenye hatua hii amefunga mabao mawili.

MSIMAMOKUNDI D
                                       Pld    W    D    L    GF    GA     Pts    
1. US  Monastir (A)          4    3    1    0      6      1         10    
2. Yanga                            4    2    1    1     6        4          7    
3. TP Mazembe                4   1     0    3      4       7          3    
4. Real Bamako                4    0    2    2      3       7          2        
 

Ufunguo:
(A)- Imefuzu

MECHI ZILIZOSALIA
Machi 19
Real Bamako v  TP Mazembe
Stade du 26 Mars, Bamako
Mwamuzi: Amin Omar (Misri)
 
Yanga v    US Monastir
Kwa Mkapa, Dar es Salaam
Mwamuzi: Alhadi Allaou Mahamat (Chad)

Aprili 2
TP Mazembe  v Yanga
Stade TP Mazembe, Lubumbashi

US Monastir  v    Mali Real Bamako
Hammadi Agrebi, Tunis