RIPOTI MAALUM: Janga, Kwa nini kamari zinaongezeka licha ya athari mbaya? - 2

Muktasari:

  • Tuliona namna watoto hususan wanafunzi wanavyotumia fedha wanazopewa na wazazi ili kutumia shuleni wakiziteketeza kwenye mashine za kamari maarufu kama Dubwi kwa lengo la kujiongezea kipato.

KATIKA mfululizo wa ripoti maalumu hii juu ya uraibu wa michezo ya kamari nchini, tuliona namna watoto wenye umri chini ya miaka 18 wanavyojiingiza, licha ya kuwepo kwa sheria kali zinazowazuia kujihusisha nayo.

Tuliona namna watoto hususan wanafunzi wanavyotumia fedha wanazopewa na wazazi ili kutumia shuleni wakiziteketeza kwenye mashine za kamari maarufu kama Dubwi kwa lengo la kujiongezea kipato.

Leo tunaendelea sehemu ya pili ya ripoti hiyo juu ya namna michezo ya kamari na kubahatisha inavyozidi kukua ndani ya jamii hususani ukanda wa Afrika Mashariki na Kati licha ya kuwa na athari kibao na viongozi wa dini nao wametia neno katika jambo hilo. Endelea nayo...!

Inapingwa na viongozi wa kidini na baadhi ya wananchi wa kawaida, lakini kwa serikali, kamari na shughuli nyingine za michezo ya kubahatisha ni chanzo cha mapato.

Michezo ya kubahatisha inaruhusiwa Tanzania ikiwa na vikwazo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18, baadhi ya maeneo na inahitaji leseni kabla ya kuanza shughuli hizo.

Hata hivyo, ukuaji mkubwa wa sekta hiyo katika miaka ya hivi karibuni umesababisha kuenea kwa shughuli hizo, hasa kwa mashine za slot ambazo zinawavutia watoto na kuongeza uwezekano wa uraibu, licha ya uwepo wa sheria na kanuni kali zinazotekelezwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha ya Tanzania.

Bodi hiyo imewalaumu “waendeshaji haramu” kwa kuvunja sheria za michezo ya kubahatisha, ikifikiria kuchukua hatua zaidi kudhibiti ukiukwaji huo.


MICHEZO HII INAKUZWA?

Serikali imefanya michezo ya kubahatisha kuwa chanzo cha mapato kwa kuchukua hatua mahususi kukuza sekta hiyo.

Katika miaka saba ya kifedha iliyopita, mchango wa sekta ya michezo ya kubahatisha kwa mapato ya serikali umekua kwa asilimia 407.1 hadi Sh170.4 bilioni mwaka 2022/23, kwa mujibu wa bodi hiyo.

Katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa sasa, sekta hiyo ilikusanya Sh108.16 bilioni, ikiongeza matumaini inaweza kuvuka Sh200 bilioni mwishoni mwa mwaka wa fedha wa sasa.

“Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa baadhi ya nchi za Afrika kutokana na ukuaji wa sekta hii,” ilisema bodi hiyo katika uwasilishaji wa hivi karibuni kwa wahariri, ikitaja Kenya, Uganda, Zimbabwe, Malawi na Ethiopia kama nchi ambazo zimejifunza kutoka taifa hilo la Afrika Mashariki.

Aidha, Serikali inasukuma kuanzishwa kwa Bahati Nasibu ya Taifa iliyotarajiwa kuanza shughuli zake katika mwaka wa fedha wa 2023/24.

Katika mwaka wa fedha wa sasa, bodi ya michezo ya kubahatisha inatarajia kutoa leseni 11,880 kwa waendeshaji wa michezo ya kubahatisha, zikiwemo leseni mpya 2,273 na kuzifufua leseni 9,607.

Wakati maendeleo haya yanaonekana kuwa chanya kwa serikali, lakini ni kinyume kwa viongozi wa kidini ambao hawakubali kamari kwa sababu za kimaadili na hata kiuchumi na baadhi ya wataalamu wanalaumu mazingira ya udhibiti.

“Hii michezo sio mizuri licha ya kwamba serikali inairuhusu kwa watu wazima,” anasema Mchungaji Mstaafu Richard Hananja wa Kanisa la Kilutheri Tanzania.

“Ni bahati mbaya kuwa sisi viongozi wa kidini hatuzungumzi kwa nguvu dhidi ya kamari. Tunatayarisha taifa la watu wavivu wanaotegemea bahati ili kufanikiwa maishani, badala ya kufanya kazi,” anasema, akiongeza alishuhudia mtu aliyeuza kiwanja kwa sababu ya uraibu wa kamari.

“Wabobezi wa kamari wako tayari kuuza chochote, pamoja na miili yao, ili kupata pesa za kubeti,” anasema.

Kwa mujibu wake, Hananja anasema watoto wanazidi kuwa wahanga wa kamari kutokana na ukweli sheria na kanuni zilizopo hazitekelezwi kwa umakini.

Januari 2019, serikali ilipiga marufuku matangazo ya shughuli za michezo ya kubahatisha kwenye redio na televisheni, baada ya tuhuma kwamba matangazo hayo yalihatarisha hali ya uwajibikaji.

Marufuku hiyo ilikuja baada ya mkutano kati ya Rais wa wakati huo John Pombe Magufuli na viongozi wa kidini walioeleza wasiwasi wao kuhusu ukuzaji uliopitiliza wa shughuli za michezo ya kubahatisha Tanzania.

Katibu Mkuu wa Taasisi ya Maimamu na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka, anasema michezo ya kubahatisha inakatazwa kwa watu wote chini ya kanuni za Kiislamu kutokana na athari zake mbaya kwa jamii.

“Kamari husababisha umaskini kwa wengi na kuunda matajiri wachache,” anasema Sheikh Mataka, akiongeza uraibu huo unaweza pia kuchochea wizi.

“Kuna pia athari za kisaikolojia kwani watu walioathirika kawaida hutegemea mapato ya haraka ya kamari na kusahau shughuli nyingine za kiuchumi. Hii ni hatari kwa taifa na ustawi wa mtu binafsi,” anasema.


NJIA YA KUJIOKOA

Maoni yake ni sawa na yale ya Naibu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Mashirika ya Ansar Sunnah Tanzania (Basuta), Sheikh Mohamed Issa, anayesema kamari na michezo inayofanana nayo sio mbaya tu kwa watoto bali pia hairuhusiwi (haramu) kwa watoto na watu wazima.

“Kamari ni miongoni mwa maovu ya kijamii yanayolaaniwa sana katika Quran na Hadithi za Mtume kutokana na athari zake za kuingiza uvivu na kupenda vitu vya haraka bila kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kujitahidi,” anasema Sheikh Issa, akiongeza kwa watoto, ina madhara kwani inaunda kizazi kinachoamini katika faida za haraka huku ikikatisha tamaa kufanya kazi kwa bidii.

“Kizazi kama hicho kinasababisha wizi, udanganyifu, ubadhirifu, rushwa na aina zote za umiliki bila kazi halali na ujasiriamali,” anasema.

Kwa mujibu wake, kuwafundisha watoto imani na kumcha “Muumba (Allah),” kuwaelimisha njia za kipato halali, kuwaelimisha dhidi ya ubaya wa kamari, kupiga marufuku matangazo ya kubeti kwenye michezo, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kunaweza kuwa baadhi ya hatua za kuokoa vizazi vijavyo.

“Lakini zaidi ya yote, kuimarisha uhusiano wa familia na kuwafundisha watoto tabia njema katika familia ni muhimu,” anasema Sheikh Issa, akihimiza sheria kali iwepo dhidi ya kufichua watoto kwenye kamari.

Kwa wanasaikolojia, kuwafungua watoto kuhusu athari mbaya za kamari kunaweza kusaidia katika kukabiliana na michezo hii “dhambi” iliyohalalishwa.

“Watoto wetu wako hatarini kupata shida kupitia kamari, kwani kamari inatangazwa kuwa halali na mamlaka chini ya masharti fulani huku kukiwa hakuna udhibiti mkali kudhibiti michezo hii hatari,” anasema mwanasaikolojia Saldin Kimangale kutoka Kituo cha Afya cha Somedics Polyclinic kilichoko Dar es Salaam.

“Kama mzazi, ni muhimu kutambua tabia za kamari kwa watoto wako haraka iwezekanavyo ili kuzuia madhara zaidi na kutoa msaada unaofaa,” anaongeza.

Kwa mujibu wake, wazazi wanapaswa kufuatilia na kuzingatia kuhusu ongezeko la pesa miongoni mwa watoto wao zisizokuwa na maelezo ya kueleweka, kujificha na simu zao za mkononi na kujihusisha na kamari za mtandaoni.

“Wazazi wanapaswa kujadili na watoto wao katika mazungumzo ya wazi bila kuwahukumu, kuwapa elimu juu ya hatari na athari za kamari kwa maneno yanayoeleweka na ambayo yanaweza kusaidia sana,” anasema Kimangale.

“Pia ni muhimu kupunguza upatikanaji wa fursa za kamari na kuhamasisha shughuli mbadala kama michezo au shughuli za ubunifu ili kuelekeza mawazo ya watoto kwa njia chanya. Wazazi pia wanapaswa kuwa karibu na watoto wao kwani kuwa nao mbali ndio sababu ya watoto hao kujiingiza katika tatizo hili baya,” alisema.

Kwa wengine, utekelezaji wa sheria zilizopo haujatekelezwa kwa ukali ili kuwalinda watoto.

Mhadhiri mwandamizi katika idara ya uchumi ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk. Lutengano Mwinuka, anasema wazazi na taasisi za elimu wanapaswa kuchukua jukumu la kuwalinda watoto.

“Nadhani hatua kubwa zaidi ni kutekeleza sheria zilizopo zinazowazuia watoto kucheza kamari,” anasema Dk. Mwinuka, akiongeza kuwa mtaala wa elimu unapaswa kuwa na vipengele vya michezo ya kubahatisha ili kuongeza uelewa miongoni mwa watoto.

Maoni yake yaliungwa mkono na mwanasaikolojia mkongwe, Fr Leon Maziku, ambaye pia aliomba utekelezaji wa sheria zinazolinda watoto.

“Ikiwa tutatekeleza kikamilifu sheria zilizopo za ulinzi wa mtoto, nadhani tunaweza kudhibiti uwezekano wa uraibu wa watoto,” anasema.


TEKNOLOJIA NA MICHEZO HIYO

Maendeleo ya kiteknolojia yamefanya iwe rahisi kucheza michezo ya kubahatisha kupitia majukwaa ya mtandaoni.

Majukwaa ya mtandaoni huomba namba ya simu ya mkononi na kuchagua kukubaliana na sharti kwamba mteja ana zaidi ya miaka 18, bila utaratibu wowote wa uthibitishaji wa hilo.

Unajua madhara ya uraibu wa kucheza michezo hii ya kubahatisha na kamari kwa ujumla? Soma kesho Jumatatu katika hitimisho la ripoti maalumu huu na namna wazazi wanavyokabiliana na janga hilo.

ITAENDELEA