Prime
RIPOTI MAALUM-2: Kilichojificha nyuma ya kufeli wanamichezo

Muktasari:
- Siyo kwamba hawafanyi vizuri mara zote, lakini inapotekea wamefanikiwa inakuwa kama bahati, huku kukiwa na mambo mengi yamejificha nyuma yao katika kufeli kwao.
KILIO cha wanamichezo wa Kitanzania kushindwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa bado hakijapatiwa ufumbuzi.
Siyo kwamba hawafanyi vizuri mara zote, lakini inapotekea wamefanikiwa inakuwa kama bahati, huku kukiwa na mambo mengi yamejificha nyuma yao katika kufeli kwao.
Kuna mambo yamekuwa yakitajwa kusababisha wanamichezo na michezo kwa ujumla kutofanya vizuri hasa kimataifa. Kati ya yote jambo kubwa linalotajwa kuchangia hayo ni fedha za uendeshaji kutokidhi mahitaji yaliyopo.
Ofisa mmoja wa Baraza la Micheza la Taifa (BMT), ambaye hakupenda kuandikwa jina lake anasema baraza hilo linakabiliwa na upungufu wa rasilimali fedha zinazohitajika kwa ajili ya mafunzo, matengenezo ya viwanja na ununuzi wa vifaa vya michezo.

Hata hivyo, ofisa huyo anasema kwamba, angalau mchezo wa mpira wa miguu una nafuu kulinganisha na mingine kwa sababu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapokea misaada mingi kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na lile la dunia (Fifa).
“Ni kweli suala la miundombinu halipo vizuri, lakini tunashukuru mchezo wa mpira wa miguu angalau unaweza kusema kuna nafuu kwa sababu CAF na Fifa huwa wanatoa misaada inayokwenda moja kwa moja TFF na inafanyiwa kazi ikiwemo kuboresha viwanja, kutoa misaada ya vifaa na hata mafunzo.
“Ukiangalia michezo mingine hali ni mbaya zaidi, angalau na mashirikisho yao nayo yangekuwa yanatoa msaada kama ilivyo kwa CAF na Fifa pengine tungeona mabadiliko.
“BMT tunapambana japo fedha hazitoshi. Tunategemea zaidi ada za wanachama, lakini pia fungu kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambao ndiyo kama mabosi wetu kwa sababu wapo juu wakiwa wanatupa maelekezo ya kufanya kuendeleza michezo hapa nchini,” anasema ofisa huyo wakati wa mahojiano yaliyofanyika Oktoba 23, 2024 katika Ofisi za BMT zilizopo ghorofa ya pili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika kuhakikisha BMT inakuwa vizuri kifedha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Methusela Ntonda, anaishauri menejimenti ya BMT kufikiria kuwa na miradi mikubwa ili kuifanya kung’ara zaidi katika kusimamia sekta ya michezo.

Ushauri huo aliutoa Oktoba 02, 2024 wakati wa ziara yake ya kwanza BMT baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Agosti 2024, kuungana na kikosi kazi kilichopo katika wizara hiyo kusukuma gurudumu la maendeleo ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Twende mbali zaidi tuwe na vitegauchumi vya Baraza. Jitahidini muweke alama,” alisema wakati wa ziara hiyo, akisisitiza kwa kuitaka menejimenti kufanya kazi kwa karibu na Chuo Cha Maendeleo ya Michezo (Malya), ili nchi iendelee kupiga hatua katika sekta nyeti ya michezo.
Mbali na fedha kutajwa kama sababu kuu, pia kumekuwapo na usimamizi duni kuhakikisha matamasha ya michezo yanakuwa na usawa na siyo kutoa kipaumbele kwa mchezo mmoja.
Kwa mujibu wa wadau mbalimbali wa michezo, mchezo wa mpira wa miguu ndiyo unaonekana kupewa kipaumbele kikubwa kwani hata yanapofanyika mabonanza asilimia kubwa huhusisha mchezo huo.
Hilo linathibitishwa na Ofisa Michezo wa BMT, Charles Maguzu anaposema asilimia 98 ya mabonanza yanayofanyika katika halmashauri ni mpira wa miguu.

“Tunawaomba waandaaji katika hayo mabonanza yao wawashirikishe kinamama, inapendeza kuona wanapocheza mpira wa miguu kuwepo netiboli ambayo ni mchezo pendwa kwa kinamama,” anasema Maguzu. Kama ambavyo Sera ya Maendeleo ya Michezo inavyosisitiza kazi za baraza kipengele cha (i) ni kuhakikisha fedha za vyama na vilabu vya michezo zinakaguliwa na matumizi mabaya ya yanaondolewa, lakini ufuatiliaji wake umekuwa ukisuasua.
Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kwamba, taarifa hizo zimekuwa hazitolewi kwa wakati licha ya kwamba BMT mara kwa mara huvikumbusha vyama.
Agosti 13, 2024, BMT ilitoa agizo kwa vyama vya michezo vinavyojumuisha mashirikisho, klabu, vituo vya michezo, shule za michezo, mawakala na yeyote aliyesajiliwa na baraza kuendesha shughuli ya michezo kuhakikisha wanawasilisha hesabu za mapato na matumizi hadi kufikia Agosti 30, 2024.
Hata hivyo, muda ulipofika na mwitikio kuwa mdogo, BMT iliuongeza ambapo Kaimu Msajili wa Vyama vya Michezo, Evordy Kyando alisema ifikapo Oktoba 10, 2024 atavichukulia hatua vyama vya michezo vinavyokaidi maelekezo, huku akieleza mwitikio mdogo wa wadau waliosajiliwa chini ya BMT kuwasilisha hesabu za mapato na matumizi ya vyama vyao.

Kyando aliyasema hayo Septemba 30, 2024 wakati wa mkutano na waandishi wa habari akisisitiza kuwa ni vyama na mashirikisho 16 yaliwasilisha taarifa kwa wakati. “Vyama vilivyowasilisha hesabu za fedha ni vichache kulinganisha na vilivyopaswa kuwasilisha taarifa hizo, tunavyo vyama jumla 13,392. Kati ya vyama hivi vyama vilivyowasilisha ni 16 tu, lakini vipo ambavyo havijawasilisha na vimeomba muda zaidi wa kuwasilisha taarifa zao.
“Kutowasilisha taarifa hizo kama ilivyoelekezwa ni kutenda kosa dhidi ya Sheria za Baraza la Michezo la Taifa na adhabu au hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria na moja ya hatua zinazokwenda kuchukuliwa ni kuvifuta vilabu ambavyo vitathibitika havijafanya hivyo pasina sababu yoyote,” anasema Evordy Kyando.
SHIDA IPO HAPA
Wakati BMT makao makuu ikisisitiza mara kwa mara kufuatwa kwa sheria, walio chini wameonekana kuwa ndilo tatizo. Hali hiyo inawalazimu viongozi wa juu wa BMT kutembelea mara kwa mara wasaidizi wao mikoani kuwakumbusha ili tu mambo yaende sawa, jambo linalodhihirisha wanaopewa mamlaka ya kusimamia hawafanyi kazi ipasavyo.

Kuanzia Septemba 2024, maofisa wa BMT wamefanya ziara katika mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ili kukutana na kamati za michezo, viongozi wa vyama na wadau wa michezo ili kujadiliana mafanikio pamoja changamoto kwa ajili ya kuleta maendeleo ya michezo nchini.
Ofisa Habari wa BMT, Najaha Bakari anasema katika ziara zao kuna changamoto nyingi hukutana nazo ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya michezo.
“Tumekutana na wadau mbalimbali katika mikoa tuliyofanya ziara ambapo ni kweli kuna changamoto kubwa katika hizo ngazi,” anasema Bakari.
“Kwanza makatibu na wenyeviti wa kamati za michezo ngazi ya wilaya na mkoa wengi wao hata hawayajui yale majukumu vizuri. Kama wasimamizi ndiyo maana tumeenda kwa ajili ya kukumbushana ili basi kazi ya usimamizi wa shughuli za michezo isimamiwe vile inavyotakiwa.
“Ukweli ni kwamba hatuwezi kufanikisha maendeleo ya michezo bila mtu kufahamu wajibu wake kwa mujibu wa kanuni na sheria zote zinazotakiwa na Baraza la Michezo la Taifa.

“Tumegundua watu wengi wanafanya shughuli za michezo bila ya kufuata miongozo na taratibu juu ya sheria inataka nini. Tumewafahamisha kwamba wasajili kwani kitu cha kwanza kabisa ili uendeshe michezo lazima usajili kwanza, taasisi yako ambayo unataka kuifanyia kazi ili ufanye kihalali shughuli yoyote ile ya michezo.
“Lakini tumefanya uhakiki wa kutambua ni vyama vipi vipo hai na vinavyofanya kazi ya michezo kwa mujibu wa katiba waliyoisajili na tumebaini kwamba wengi wao hawakufuata zile taratibu.
“Unakuta kweli wamesajili, lakini hawafuati kwa mujibu wa katiba zao na mambo ambayo tumesisitiza sana kwanza ni kufanya usajili, kulipa ada kwa mujibu wa mwongozo wa Baraza la Michezo la Taifa, lakini pia wawe wanaoandaa taarifa za mapato na matumizi ya chama husika na je wanaonekana uwanjani.
“Mtu anaweza kusajili halafu anaweka makaratasi mfukoni, hakuna kinachoendelea kwamba amesajili kwa ajili ya maendeleo ya michezo, haonekani uwanjani, hakuna mashindano yoyote yanayoendelea, hakuna mafunzo yoyote.

Haya yote ni mambo ambayo Baraza limekuwa likifuatilia ili kuhakikisha kwa pamoja tunalichukua jukumu la kufanya maendeleo ya michezo nchini.”
ITAENDELEA KESHO