Prisons na chimbo la makipa Ligi Kuu

TANZANIA Prisons imeingia kwenye sifa nzuri na kukuza makipa ambao wanahamia timu nyingine za Ligi Kuu Bara na kufanya vizuri.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya makipa waliopita Tanzania Prisons wakafanya vizuri na kutoka kwenda kujaribu maisha nje ya timu hiyo.


BENO KAKOLANYA

Baada ya Tanzania Prisons kuachana na Wilbert Mweta, mashabiki wa soka walihofu timu hiyo ingeshuka daraja, kwani katika mzunguko wa kwanza, ilikuwa ipo chini kabisa mwa msimamo wa ligi, hivyo kuondoka kwa kipa tegemeo kuliwapa wasiwasi wengi.

Marehemu David Mwamaja miaka hiyo aliamua kumuamini kipa, Beno Kakolanya ashike hatamu za timu hiyo na hakumuangusha, kwani alipigana kiume na kuisaidia timu yake kuondoka katika janga la kushuka daraja. Hata katika mchezo waliocheza na Ashanti mjini Morogoro, ambao kama wangefungwa wangeshuka daraja yeye ndiye alikuwa nyota wa mchezo.

Ubora wake akiwa Prisons uliwavuta matajiri wa Jangwani Yanga ambao waliamua kumsajili msimu wa 2016 hadi 2019 kabla ya kutimkia kwa mahasimu wa Yanga, Simba baada ya kushinda kesi ya madai.

Kakolanya aliitumikia Simba kwa misimu minne lakini hakuweza kumpa changamoto Aishi Manula kwani alikuwa anapata nafasi ya kucheza pale ambapo kipa namba moja anapokuwa na shida.

Beno ambaye kwasasa anakipiga Singida Fountain Gate, alipokuwa Simba alitwaa mataji matatu na kucheza hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.


HUSSEIN ABEL

Ni kipa ambaye alionwa na Tanzania Prisons kutoka Taifa Jang’ombe ya Zanzibar baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ikiwemo kuwa Mchezaji Bora wa mechi dhidi ya Yanga SC.

Abel ameitumikia Tanzania Prisons kwa mwaka mmoja na nusu na baada ya mkataba wake kumalizika ofa ya KMC ilimvutia na kuamua kumalizana na timu hiyo ambayo imefanya biashara na Simba katika dirisha kubwa la usajili.

Jicho la kwanza kuona kipaji chake ilikuwa ni Tanzania Prisons.


AARON KALAMBO

Ni zao la timu ya vijana ya Tanzania Prisons kabla ya kwenda kuchezea Polisi Morogoro mwaka 2015.Alirejea Prisons mwaka 2016 akacheza hadi mwaka 2020 alipohamia Mbeya City, kabla ya kujiunga na Dodoma Jiji FC msimu uliopita.

Kalambo ni kipa ambaye alijijengea ufalme ndani ya timu ya Prisons kutokana na ubora wake kwenye lango na kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.


JEREMIA KISUBI

Alitua Tanzania Prisons msimu wa 2021 akitokea Kagera Sugar ambapo jina lake halikuweza kuwika kama aliponza kuitumikia timu hiyo ambayo ilimpa ulaji wa kutua Simba na sasa anakipiga Mtibwa Sugar kutokana na kushindwa kuendana na kasi ya Aishi Manula na Beno Kakolanya kipindi hicho.

Kalambo alipata nafasi ya kusajiliwa na Simba baada ya kuikazia kwenye mechi ya ligi ya iliyochezwa Machi 12, 2021 kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, kiwango kilicho onyeshwa na kipa huyo kiliwashawishi matajiri wa Msimbazi kuwinda saini yake.

Licha ya kufanya vizuri akiwa Tanzania Prisons alipotua Simba kwa mkataba wa miaka mitatu alishindwa kupata nafasi ya kuchucheza mchezo hata mmoja hadi walipoamua kumtoa kwa mkopo Mtibwa Sugar.


METACHA MNATA

Hili ni zao la Azam FC kabla ya kujitangaza kupitia Mbao akiwa kipa namba moja baada ya timu hiyo kushuka alijiunga na Tanzania Prisons timu ambayo ilimnoa kwa msimu mmoja tu na kumuuza Yanga, alipokaa kwa miezi 12 kabla ya kusajiliwa na Yanga. Agosti mwaka juzi, Metacha alijiunga na Polisi Tanzania kabla ya kutimkia Singida Big Stars Julai mwaka jana na Januari mwaka huu akarejea tena Yanga.

Ubora wa Metacha akiwa na Tanzania Prisons ulimpa nafasi ya kuitwa hadi timu ya taifa kitu ambacho ni nadra sana kutokea kwa timu ndogo nje ya Simba na Yanga kutoa kipa wa kuitumikia Taifa Stars.

Kujituma kwake na kukampa ulaji Yanga ambayo aliitumikia kwa mafanikio na baadaye kuachwa kutokana na mkataba wake kuisha na kutimkia Polisi Tanzania baadaye Singida Big Stars sasa karudi tena Yanga.