Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Presha za kina Sarpong ziwaamshe Azam FC

SIKUMBUKI vizuri ilikuwa ni lini, ila ni mwanzoni mwa miaka ya 2000 nje ya ofisi za Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) zilizokuwa majengo ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ilala Boma nilikuwa nabadilishana mawazo na aliyekuwa Katibu Msaidizi wa Azam, Twalib Seleman ‘Chuma’.

Huyu Chuma, hatajwi sana katika historia ya Azam, ila kwa wale wanaoijua Azam tangu ikiwa Mzizima wanazijua pilika zake akiwa bega kwa bega na Daud Kanuti, mmoja wa viongozi wa soka wilayani Ilala aliyeshiriki kwa kiasi kikubwa kufanikisha timu za wilaya hiyo kupata mafanikio.

Siku hiyo, tulikuwa tunapiga stori baada ya Shirikisho la Soka (TFF) chini ya Leodegar Tenga kufuta mfumo wa ligi. Azam ilikuwa imepanda Daraja la Pili pamoja na Navy ya Kigamboni kutoka Dar es Salam walikuwa wakijindaa kufanya yao, lakini kazi ikaishia hapo na kuleta Ligi ya Taifa.

Chuma aliniambia; “Pamoja na ligi kufutwa, nakuhakikisha Azam lazima ije kucheza Ligi Kuu baada ya muda mfupi. Sio kucheza Ligi Kuu tu, lakini tunataka kuja kuvunja ufalme huu wa Simba na Yanga kwa kubeba ubingwa na kupata mafanikio makubwa kimataifa.”

Kauli hii aliitoa kwa uchungu mkubwa. Ni kama ile tu iliyowahi kutolewa baadaye na aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohammed Seif ‘King’.

Binafsi niliamini kauli hizo kwa vile nilikuwa naona walivyokuwa wakichakarika ndani na nje ya uwanja.

Kama utani, Azam ikapasua kuanzia tena chini pale Ilala, ikapenya Ligi ya Mkoa ikiwazidi ujanja Cosmopolitan katika mechi tamu iliyopigwa Uwanja wa Shule ya Benjamin Mkapa, eneo la Uhuru Mchanganyiko. Ikavutiwa na John Bocco ‘Adebayor’ aliyekuwa moto kinoma ndani ya ligi hiyo akiichezea Cosmo. Wakaenda naye Dodoma na kupanda daraja katika msimu huo wa 2007-2008 sambamba na Villa Squad kutoka Kinondoni.

Azam ikaanza kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2008-2009 ikitimiza zile ndoto ambazo Chuma, King, Kanuti na viongozi wa Azam wakiongozwa na Father waliiota tangu wakicheza ngazi za chini.

Azam ikasukwa kibabe, wale vijana waliotwaa ubingwa wa Copa Coca Cola 2007 kutoka Kinondoni ambao walikuwa chini ya makocha John William ‘Del Pierro’, Mbwana Makatta na Heri Chibakasa ‘Mzozo’ asilimia kubwa wakachukuliwa Azam na kuunganishwa na wengine mambo yakaanza.

Azam ikatisha. Ikajenga uwanja. Ikamiliki hosteli na miundo mbinu yote inayohitajika kwa klabu ya Ligi Kuu. Ikazitikisa Simba na Yanga.

Kila mdau wa soka nchini alikuwa akiiangalia kama moja ya klabu itakayoleta mapinduzi makubwa katika soka la Tanzania na ukanda nzima wa Afrika Mashariki, kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa.

Kwa kiasi kikubwa ilifanikiwa kwani baada ya kutokwa ushamba wa ligi msimu wa kwanza 2008-2009, ilitisha na kupanda kimafanikio kwa haraka, kwani ilishaizoea na kucheza ndani ya Nne Bora, kisha Tatu Bora na kuja kutenganisha vigogo hao.

Mipango yao na jinsi ilivyokuwa ikipambana haikuwa ajabu, 2013-2014 ilipobeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Azam ilibeba ubingwa huo baada ya kuzitenganisha Simba na Yanga katika ile ligi yao ya timu mbili. Tena ikabeba bila kupoteza mchezo.

Kama mmoja ya wadau waliokuwa bega kwa bega na Azam kipindi hicho, nilifarijika! Niliamini zile ndoto za kina Chuma na King na wengine walioishuhudia safari nzima ya kuzaliwa kwa klabu hiyo zilikuwa zikienda kutimia tena haraka tofauti na ilivyofikiriwa.

Hata hivyo, nimewakumbuka kina King na Chuma baada ya kuona Azam ikiyumba. Haijulikani kitu gani kilichoitokea timu hii. Azam haijawahi kubeba tena ubingwa wa Bara. Imekuwa iking’ara Kombe la Mapinduzi. Imewahi kubeba ubingwa wa Kombe la Kagame, lakini hakuna anayejua kitu gani kinachoizuia kurejea tena mafanikio katika Ligi Kuu. Kimataifa licha ya kupata nafasi ya uwakilishi kwa miaka michache, lakini haikuwa na maajabu, zaidi ya kufika 16 Bora ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa kwa bahati mbaya kabla ya kuingia play-off dhidi ya FAR Rabat ya Morocco.

Hakuna siri, Azam ina kila kitu. Imezizidi Simba na Yanga kwa kila kitu juu ya klabu ya kisasa ya soka. Ila imekosa tu wanachama na mashabiki wa kuwapa presha nyota wao uwanjani.

Kama hawa kina Sure Boy na hata wenzao waliopita wangepigwa presha kubwa nje ya uwanja pale Azam ikipata matokeo mabaya kama inavyokuwa wa Simba na Yanga, wangezinduka na kuipigania timu yao. Lakini kwa vile hawakutani na hali hiyo, Azam imekuwa timu ya kawaida sana. Inaumiza!

We angalia tu namna nyota wa Yanga na hata kocha wake, Cedric Kaze wanavyoishi katika presha kubwa. Angalia hata Simba walipojikwaa kidogo na joto walilopata kutoka kwa mashabiki na wanachama na namna walivyobadilika ndani ya muda mchache.

Hii ndio inazozifanya klabu hizo kongwe kuwa mbali kulinganisha na Azam hata kama zimeachwa mbali kwa mambo mengi hususani ya miundo mbinu na uwekezaji.

Ukiangalia vikosi vya Azam kwa miaka yote ya uwepo wao katika Ligi Kuu, ikiwamo cha sasa wamekuwa wakisajili nyota wenye uwezo mkubwa na kufundishwa na makocha wakubwa, hata hivyo hawajawahi kupata presha kubwa. Presha waipatayo wachezaji na hata makocha labda ni zile za mabosi wao wa juu tu, lakini uwanjani wanapumua na ndio maana Azam inaonekana ya kawaida.

Kuna wakati huwa natamani hizi presha wanazokutana nazo kina Clatous Chama, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu, Pascal Wawa, Beno Kakolanya, Mukoko Tonombe, Michael Sarpong, Farid Mussa na wenzao wengine zingehamia Azam.

Kuna wakati unaweza kudhani labda tatizo ni viongozi wa klabu hiyo au fitina za Simba na Yanga ndio zinazoiangusha Azam, lakini ukiangalia namna wachezaji wao wanavyocheza unabaini wanarelax sana kama kwamba wapo mazoezini. Hawana presha yoyote nje ya uwanja. Hili ni tatizo!

Naamini zile presha za Simba na Yanga zingekuwa zikiwapata nyota wa Azam tangu walipopanda Ligi Kuu na kwa namna ya uwekezaji uliofanywa kwa timu hiyo ni wazi ingekuwa mbali sana hata kama watakuwa wakifanyiwa fitina na timu hizo za Kariakoo.

Ila bado naendelea kuamini kuna siku mambo yatabadilika na hasa kama viongozi wa Azam na wamiliki wake watakapotambua kuwa timu yao ni kubwa na lazima iwe na mambo makubwa ikiwezekana ije kusajili wachezaji watakaojua dhima yao ya kuipa heshima klabu hiyo.


Imeandikwa na Badru Kimwaga