Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PELEMBELA: Nilimuokoa mshkaji nikacheza pambano, nikashinda

Muktasari:

  • Ni ngumu kuzungumzia mchezo wa ngumi bila kutaja jina la Kinyogoli kutokana na rekodi aliyoacha kwenye mchezo wa ngumi kutokana na aliyofanya na anayoendelea kufanya kwa mabondia waliokuwa chini yake.

AHMED Pelembela ni mmoja kati ya mabondia wachanga wanaohitaji kuangaliwa mwaka huu kutokana na uwezo wa mkubwa ndani ya ulingo alionao akiwa chini ya bondia wa zamani ambaye pia ni kocha mkongwe, Habibu Kinyogoli.

Ni ngumu kuzungumzia mchezo wa ngumi bila kutaja jina la Kinyogoli kutokana na rekodi aliyoacha kwenye mchezo wa ngumi kutokana na aliyofanya na anayoendelea kufanya kwa mabondia waliokuwa chini yake.

Ibrahim Class, Abdallah Pazi, Ibrahim Makubi na Ahmed Pelembela ni miongoni mwa mabondia walio chini yake ambao mara zote amekuwa akiwafundisha mwenyewe mbinu mbalimbali za kufanya vizuri katika mapambano yao.

Lakini, kwa mujibu wa rekodi yake Pelembela aliyeanza kupanda ulingoni 2018, amecheza mapambano 10 kati ya hayo ameshinda matano na moja likiwa ni kwa Knockout.

Bondia huyo amepigwa katika mapambano matatu kati ya hayo moja likiwa ni kwa Knockout huku akitoka sare mara mbili.

Kwa sasa Pelembela anakamata nafasi ya 10 katika mabondia 111 wa uzani wa light nchini wakati duniani akiwa wa 572 kati ya mabondia 2489 wa uzani huo, huku akiwa amepewa hadhi ya nyota mmoja.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, bondia huyo anaeleza nini kilimfanya aingie kwenye mchezo wa ngumi akiwa anasoma darasa la nne katika shule ya msingi kwao mitaa ya Mabibo.

“Binafsi nimeanza kupenda mchezo wa ngumi tangu wakati nipo shule ya msingi. Nakumbuka ilikuwa darasa la nne na sababu kubwa kuna bondia anaitwa Abdul Zedi nilikuwa naona akifanya sana mazoezi ila sasa ameacha ngumi,” anasema Pembelela.

“Yeye ndiyo nilimuomba, lakini kwa sababu nilikuwa mdogo ikabidi aniombee kwa wazazi wangu ili niwe nafanya mazoezi na kwa bahati nzuri nilikubaliwa nikawa nafanya naye mazoezi ya ngumi.

“Niliendelea nikawa nacheza ngumi za ridhaa, lakini baadaye shule ikanifanya nisiendelee kutokana na kubanwa na muda hasa nilipoingia sekondari nilikuwa nasoma Yusufu Makamba (sekondari) ingawa sikumalizia pale.”


SWALI: Nini kilifanya usimalize shule?

JIBU: “Unajua ukichanganya utoto na mambo ya shule ukweli upepo wa makundi ulinichukua - sasa nikawa siyo mtu wa kufika shule ingawa familia ilikuwa inajua nafika shule kila siku.

“Nakumbuka hali hiyo ilichukua kati ya miezi mitatu hadi minne shule sifiki kazi yangu kuzurura na kundi la wanafunzi wenzangu katika shule nyingine na hakuna mtu yeyote kwenye familia alikuwa akitambua kama nilikuwa sifiki.

“Lakini wakati huo naishi kwa dada yangu na walinipa simu ambayo kawaida nilikuwa natakiwa niache nyumbani nikienda shule, lakini kwa kuwa nilikuwa sifiki na wao hawajui nikawa natoka nayo.

“Sasa nakumbuka ulitokea msiba wa babu yangu upande wa mama, dada akanifuata shule kuniombea ruhusa ili tusafiri kwenda Bagamoyo kuzika, lakini alipofika walimu walimuambia kwamba hawajui nilipo maana nilikuwa sifiki shule kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

“Basi dada yangu alitoka shule akanipigia nikawa sipokei kwa sababu nilihisi jambo tofauti na haikuwa kawaida kupigiwa na watu wa familia wakati wa masomo, ila muda huo ndiyo nipo na kundi la marafiki tunakata mitaa.

“Dada yangu akanitumia ujumbe wa taarifa ya msiba akinitaka nirudi nyumbani kwa sababu shule hakuweza kunikuta. Basi nilirejea nyumbani tukaenda kuzika, nashuruku nilimzika babu yangu.

“Lakini msala ukabaki kuwa shule maana baada ya kurudi dada alichukua jukumu la kunipeleka shule, lakini kwa bahati mbaya walimu waligoma kabisa kunipokea. Nikasimamishwa kwa kipindi cha miezi mitatu nadhani kama walinifukuza maana walikuwa wakidai nitawaharibu na wanafunzi wengine kama nitabaki pale.

“Kutokana na hali hiyo familia ikalazimika kunipeleka shule ya bweni Tanga. Wakafuatilia uhamisho wangu nikaenda kumalizia shule huko ambapo ilikuwa ni mwaka 2015.


SWALI: Kwa Mzee Kinyogoli ulifikaje?

JIBU: “Unajua nilianza kuishi Mabibo Makutano, hivyo kuna wakati nikawa nafanya mazoezi kwa mwalimu kocha Jafarin Ndame, lakini baada ya kumaliza shule nilihamisha makazi nikaenda kuishi Airpot kwa dada yangu.

“Kule nikaanza kusaka gym, lakini kwa bahati nzuri nilikutana na bondia anaitwa Abdul Kazumari yeye ndiyo alikuwa mwenyeji wangu akanipeleka kwa kocha Sakwe Mtulya. Wakati huo Kazumari asubuhi anaenda Ngome - Lugalo kufanya mazoezi na timu ya ngumi za ridhaa jioni tunafanya naye mazoezi.

“Lakini kwa habati mbaya kutokana na mambo ya kimaisha Sakwe mambo yakawa yanambana ndiyo alinichukua na kunipeleka kwa kocha mzee Habibu Kinyogoli.

“Nashukuru nilipokewa vizuri na mzee akaona juhudi zangu ila zaidi akaja kugundua kwamba baba yangu mdogo ni rafiki yake wakati wanatafutana, hivyo mzee ananichukulia kama mtoto wake. Mafunzo napata ya kutosha kutoka kwake na kila siku anakuwa na vitu vipya.

“Kuhusu kupigana ulingoni binafsi nashukuru Mungu naendelea kupambania ndoto yangu, lakini bado naupenda huu mchezo kwa sababu sasa umekuwa ajira ya vijana wengi, hivyo naamini katika kutimiza ndoto na malengo.


SWALI: Ulishawahi kupigwa ukatamani kuacha ngumi?

JIBU: “Mara nyingi siyo sawa kusema kwa sababu tunapaswa kukubaliana na matokeo, lakini kuna pambano nilipoteza kwa kupigwa, ila sijui nilipigwa vipi au kitu gani kilitokea kwa sababu uwezo na kiwango changu kilikuwa juu, lakini ajabu nilipoteza kiasi cha kukata tamaa ya kuendelea na mchezo ila nashukuru nilikaa sawa naendelea kupambania ndoto.


SWALI: Jambo gani huwezi kulisahau katika ngumi?

JIBU: “Nakumbuka kuna wakati nilichukua pambano la rafiki yangu bila ya mazoezi ili kumuokoa na deni la promota na hakuwa na uwezo wa kulipa.

“Rafiki yangu alipata mapambano mawili ambayo yalikuwa nayapishana mwezi mmoja sasa akapoteza pambano lake la kwanza na kawaida unatakiwa ukae siyo chini ya siku 30 bila ya kupigana, ukiangalia sehemu zote alishachukua pesa zote kurudisha hawezi na kupigana hawezi.

“Lakini kwa kuwa alikuwa ni mtu wangu wa karibu ilinibidi niingilie kati kumsaidia kwa kucheza pambano lake kwa kuwa kilo zetu zinafanana. Mungu aliweka baraka zake nikashinda japo sikuwa na mazoezi ila naamini nilifanya kumsaidia rafiki yangu, nikashinda.

SWALI: Nje ya ngumi unafanya kazi gani?

JIBU: “Nafanya biashara ya nguo za mtumba na viatu. Kawaida mimi ni wale ambao wanaitwa ‘ma-pointer’ nanunua nguo zangu kwenye mnada hasa Soko la Karume ndiyo kijiwe changu na wakati mwingine nachukua viatu, ndiyo tunaendesha maisha.

“Uzuri kazi zangu za biashara ni Ilala na mazoezi nafanya Ilala. Huwa nikimaliza kazi zangu naingia mazoezi kwa sababu ni karibu.


SWALI: Una mipango gani kwenye ngumi?

JIBU: “Nataka kufika mbali. Nataka kuwa bingwa wa dunia ambaye natambulika duniani jambo ambalo naamini linawezekana kwa asilimia mia.


SWALI: Ukiwa na mzee Kinyogoli unadhani kitu gani huwa kinamkera?

JIBU: “Kiukweli katika suala nidhamu mzee hataki masihara kabisa kwa sababu anaamini nidhamu ndiyo msingi wa mafaniko ya bondia, sasa kama huna nidhamu kwake huwezi kutoa maana kama mimi najivunia kupata nafasi ya kufundishwa na yeye.”