Opah alivyotua kusaka namba Mexico

Muktasari:
- Ni wazi Juarez haijakosea kumsajili nyota huyo wa Twiga Stars mwenye mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa na Simba Queens, uwezo wake wa kuliona lango ni moja ya mambo yaliyoivutia miamba hiyo huku pia akitolewa macho na timu nyingi duniani.
MSHAMBULIAJI Opah Clement wiki hii ametambulishwa FC Juarez ya Mexico inayoshiriki Ligi ya Wanawake nchini humo na kumfanya aongeze idadi ya nyota wa Tanzania wanaocheza ligi hiyo baada ya Julietha Singano anayekipiga timu hiyo na Enekia Lunyamila wa Mazaltan.
Ni wazi Juarez haijakosea kumsajili nyota huyo wa Twiga Stars mwenye mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa na Simba Queens, uwezo wake wa kuliona lango ni moja ya mambo yaliyoivutia miamba hiyo huku pia akitolewa macho na timu nyingi duniani.
Ukiachana na Simba Queens alikopata mafanikio makubwa ya soka la wanawake, nyota huyo alichezea Kayseri Kadın ya Uturuki kwa mkopo 2022, msimu uliofuata akasajiliwa Beşiktaş ya nchi hiyo na 2023/24 akiichezea Henan Jianye ya China kwa msimu mmoja.

MSIMU 2021/22
Kama kuna msimu bora kwa mshambuliaji huyo tangu aanze maisha yake ya soka la kulipwa basi ni huu wa 2021/22.
Msimu huo aliisaidia Simba Queens kutwaa taji la Ligi kwa msimu wa pili mfululizo akikosa kiatu cha ufungaji bora.
Kuna msemo unasema 'Omba bahati' kwa kuwa bahati haikuwa upande wa mrembo huyo na tuzo ikaenda kwa Aisha Masaka aliyekuwa anakipiga Yanga Princess na sasa yupo zake Brighton akifunga mabao 35 tofauti ya bao moja na Opah aliyeweka kambani 34.
Tangu hapo Opah hajawahi kufikisha mabao hayo ndani ya msimu mmoja na badala yake msimu uliopita akiwa na Henan Jianye ya China alifunga mabao matano.
Kwa ujumla hadi sasa ana mabao 16 kwenye timu tatu alizopita tangu aondoke Simba, Jianye na Kayseri Kadin akifunga mabao matano huku Besiktas ya Uturuki akiweka kambani mabao sita.

KUMALIZA UKAME WA MABAO
Usajili wa mshambuliaji huyo unaweza kuwa dawa kwa timu hiyo ambayo hadi sasa imefunga mabao saba kwenye mechi sita za Ligi ikiwa miongoni mwa timu zilizofunga mabao machache.
Licha ya timu huwa na washambuliaji lakini hadi sasa kiungo wao, Grace Asantewaa raia wa Ghana ndiye anayeongoza kwenye ufungaji akiweka kambani mabao mawili.
Karime Abud raia wa Mexico ndiye mshambuliaji pekee wa timu hiyo aliyofunga bao moja na msimu uliopita akiwa na timu hiyo kwenye mechi 32 alifunga bao moja tu kwenye mashindano yote.
Unaona ni namna gani Opah anaweza kuingia kwenye kikosi hicho moja kwa moja na kama ataendeleza ubora aliokuwa nao akiwa na Henan ya China huenda akawa miongoni mwa wachezaji wa kutegemewa eneo hilo.
Ubora wa viungo wa Juarez kwenye kutengeneza nafasi unaweza kumrahisishia nyota huyo kufunga mabao kwenye ligi ya Mexico.

AWAFUATA SINGANO, LUNYAMILA
Wote wawili waliichezea Simba Queens kabla ya kutimkia nchi nyingine, Julietha akitimkia Mexico na Opah akitambulishwa Uturuki.
Usajili huo unaifanya timu hiyo kuwa na nyota wawili Watanzania Singano anayecheza beki wa kati kwa msimu wa tatu sasa tangu ajiunge nao msimu 2022/23.
Hata hivyo Opah anakuwa mchezaji wa kike watatu kusajiliwa nchi hiyo baada ya msimu uliopita Enekia Lunyamila kutambulishwa Mazaltan inayoshiriki Ligi hiyo.

Msimu uliopita akiwa na Henan amefunga mabao matano, Besiktas akifunga mabao msita na Kadin alipoweka kambani mabao matano.
Hadi sasa yeye pekee ndiye mgeni kwenye Ligi hiyo huku Lunyamila ukiwa msimu wake wa pili sasa baada ya mwaka jana kumaliza na mabao sita.
Hata hivyo ni kama Lunyamila ana bahati ya kucheza na watanzania wenzie kwani kabla ya kuichezea Mazaltan aliwahi kukipiga Ligi moja na Clara Luvanga (Al Nassr) wote wakicheza Saudia Arabia.
Kiraka huyo alikuwa akiitumikia Eastern Flames ambayo ilimaliza mkiani kabla ya hapo pia aliwahi kucheza Morocco na Mtanzania mwenzake Diana Msewa anayekipiga Uturuki.
Ikumbukwe wote watatu wanafahamiana vizuri hasa kwa Opah na Singano ambao wote walicheza Simba kwa mafanikio makubwa wakiipa ubingwa wa Ligi.

WASIKIE HAWA
Kocha wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka alisema ni hatua nzuri kwa soka la wanawake kuona wachezaji Watanzania wanacheza Ligi mbalimbali.
"Hadi anasajiliwa ni wazi wameona ubora wa nyota huyo, natamani watoto wa kike pia wafike mbali zaidi naamini kitendo cha kusajiliwa hapo kitaleta matunda kwa sababu ni mshambuliaji mzuri sana," alisema Chobanka.
Kocha wa Alliance Girls, Sultan Juma alimpongeza nyota huyo wa zamani wa Simba akiamini soka la wanawake sasa ni biashara kubwa tofauti na awali.
"Hawa akina Opah ndio wanawaamsha hata wachezaji wengine kuendelea kupambana kuamini siku moja na wao wanaweza kucheza Ligi kubwa kama anayocheza Aisha Masaka wa Brighton ya Uingereza."