NYUMA YA PAZIA: Wote tunaipenda Man City kimya kimya, tunaitamani

Sunday May 16 2021
man city pic
By Edo Kumwembe

MZUNGU mmoja aliwahi kutupa usemi aliposema “If wishes were horses, beggars would ride.” Alikuwa akimaanisha kama mafanikio yangekuwa yanapandwa kama farasi, basi kila mmoja, hata maskini angeyapanda.

Nilikumkumbuka huyo mzungu baada ya wachezaji na mashabiki wa Manchester City kusherehekea ubingwa wa England wakiwa katika sebule zao Jumanne usiku. Hawakuingiza miguu yao uwanjani na bado wakawa mabingwa.

Walistahili? Ndio. Kwa sababu gani? Wana bonge la kocha na wana bonge la timu. Hawakuchukua ubingwa msimu uliopita kwa sababu Liverpool walizing’ang’ania kila pointi tatu zilizokuwa usoni mwao na walikuwa katika fomu ya hali ya juu. Wakati huohuo Mungu alikuwa anawakumbusha Manchester City kwamba wao ni binadamu wa kawaida tu wasipofanya juhudi hawapati chochote.

Nje ya suala la ubinadamu, Manchester City ni timu iliyo sayari nyingine kabisa. Wote tunaoshabikia timu nyingine tungependa timu zetu ziwe kama Manchester City. Hatuwezi kusema hadharani, lakini tunakiri kuwa wote tungependa kocha wetu awe Pep Guardiola na wachezaji wetu wawe wale wa Man City.

Kwanza kabisa Man City wana utajiri wa wachezaji katika nafasi mbalimbali ni tofauti na kila timu England. Mechi ya leo haujui nani na nani wataanza pale mbele. Mechi ya kesho pia hivyohivyo. Na hakuna kikosi ambacho kitakupa unafuu mkubwa ingawa wote tunakubali kwamba Kelvin De Bruyne ndiye mchezaji wao muhimu zaidi.

Pale Man City leo wanaweza kuanza Raheem Sterling, Gabriel Jesus na Ber-nardo Silva. Mechi ijayo wanaweza kuanza Phil Foden, Sergio Aguero na kulia akacheza Riyad Mahrez. Cha kushangaza wataicheza mechi katika ubora uleule tu. Hakuna kitakachoharibika.

Advertisement

De Bruyne anaweza kuanzia benchi, lakini Ilkay Gundogan akipangwa hakupi unafuu. Si ajabu msimu huu amekuwa mchezaji bora kuliko De Bruyne mwenyewe ambaye wakati fulani alikuwa anasumbuliwa na majeraha. Hawa ndio Manchester City ambao kila mtu anatamani kuwa nao.

Sisi katika vikosi vyetu akiumia mchezaji muhimu zaidi kikosini, basi anayefuata kunakuwa na pengo kubwa kati yao. Ni tofauti na pengo ambalo lipo kati ya De Bruyne na Gundogan. Huu ni ukweli unaoumiza kidogo. Manchester United asipocheza Bruno Fernandes basi kazi ipo.

Katika pambano dhidi ya PSG, Pep Guardiola alimuweka benchi mmoja kati ya walinzi wake bora, Joao Cancelo na nafasi yake ikaenda kwa Kyle Walker. Kisa? Walker ana kasi zaidi na angeweza kwenda sambamba na kasi za mastaa wa PSG kina Kylian Mbappe, Angel Di Maria na Neymar.

Hii ndio tofauti ya Man City na wengineo. Huku kwetu akiumia Trent Alexander Arnold ni tatizo. Sijui atacheza mzee James Milner au nani - hatujui. Hapa ndipo ambapo kila mtu anatamani timu yake ingekuwa Manchester City kwa maana ya utajiri wa wachezaji.

Man City pia wana kocha hasa. Pep Guardiola. Kwanza amejua kukusanya kundi la wachezaji mahiri. Wengine walikuwa ghali, wengine bei za kawaida. Kisha amewafanya wacheze mpira wake ambao tunaujua siku zote.


Mpira ambao wote tunatamani ungekuwa unachezwa na timu zetu.

Man City ifungwe, ishinde, itoke sare daima watakuwa na mpira wao mguuni. Hawakupi. Wanakaa nao katika staili ya tiktak. Wanamfanya adui kuwa mnyonge. Kila mtu angependa timu yake iwe kama Manchester City kwa namna ambavyo wanacheza. Huu ndio ukweli mchungu.

Pep huyuhuyu ana kitu kingine ambacho wengine hawana. Watu wanasema anatumia sana pesa, lakini ukweli ni kwamba wachezaji anaonunua wanacheza staili yake ya soka na pia wanaimarika chini yake. Sidhani kama kuna mchezaji aliyenunuliwa na Pep ambaye amefeli Man City. Labda wale aliowakuta kina Nicolas Otamendi na wengineo.

Na bahati nzuri ni kwamba wanaingia katika mfumo wake taratibu. Ni kama ilivyokuwa kwa Mahrez. Tulidhani amepotea njia, lakini sasa hivi amekuwa tishio. Sasa hivi Mahrez amekuwa moto zaidi. Hivi ndivyo ambavyo Pep amekuwa akifanya kazi zake.

Huyuhuyu Fernan Torres ambaye watu wanamuona mchezaji wa kawaida watu watakuja kuulizana baadaye kama ndiye yeye. Anaingia katika mfumo taratibu. Baadaye atakuwa tishio kubwa. Pep anajua namna ya kuwatumia watu wake kwa akili.

Phil Foden ingawa hakumnunua, lakini angalia jinsi alivyomgeuza kuwa staa mkubwa kimyakimya. Sasa hivi tunashangaa. Msimu huu amekuwa staa mkubwa na hapana shaka ataendelea kuwa mkubwa na kuchukua umuhimu ule ule wa De Bruyne.

Wote tunatamani tuwe kama Man City. Tunatamani tuwe na Guardiola, tuwe na De Bruyne, tuwe na Silva tu na kila mtu wa City. Tunaficha tu lakini huu ndio ukweli halisi. Timu yao ikiondoka siku moja tutasema.

Advertisement