NYUMA YA PAZIA: Neymar, tukutane Doha kwa karata ya mwisho

Sunday May 09 2021
NEYMA PIC
By Edo Kumwembe

FEBRUARI 5 alizaliwa Cristiano Ronaldo pale Funchal, Ureno. Tarehe kama hiyo alizaliwa Laura Linney mwigizaji wa Marekani. Tarehe kama hiyo alizaliwa Michael Manne, mwongoza filamu wa Marekani. Tarehe kama hiyo alizaliwa Carlos Tevez. Tarehe kama hiyo alizaliwa Neymar kutoka Brazil.

Wote na wengineo hao wanaisubiri tarehe hiyo kusheherekea siku yao ya kuzaliwa. Neymar pia anaisubiri. Atakuwa akitimiza miaka 30. Nyakati zimekwenda wapi? Majuzi tu alikuwa kijana mdogo aliyevuka bahari kutoka Brazil mpaka Hispania kucheza soka. Alikuwa na miaka 22 tu. Februari mwakani atatimiza miaka 30.

Nilikuwa namtazama majuzi pale Manchester. Sura yake ilikuwa imesinyaa. Timu yake PSG iliondolewa na Manchester City katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Neymar anaweza kuwa Thierry Henry mpya katika soka. Anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji mahiri ambao hawajawahi kuwa wanasoka bora wa dunia.

PSG kuondolewa nusu fainali kunamaanisha kwamba Neymar anaweza kushinda taji la Ufaransa tu. Taji la League One haliwezi kukufanya uwe mwanasoka bora wa dunia. Haliwezi. Wafaransa hawapo walau katika ligi bora nne duniani. Wapo nyuma ya Waingereza, Wahispaniola, Waitaliano na Wajerumani.

Neymar alikuwa anategemea zaidi michuano hii kwa ajili ya kuwa mwanasoka bora wa dunia. Amepambana kwelikweli lakini imeshindana. Msimu uliopita walicheza kitoto wakafungwa kizembe katika pambano la fainali dhidi ya Bayern Munich.

Msimu huu tena hadithi imekuwa ileile tu. Hakuna jipya ambalo wanaweza kufanya tena. Kuchukua ubingwa wa Ufaransa sio jambo jipya. Na sasa analazimika kusubiri kitu kimoja kikubwa. Michuano ya Kombe la Dunia pale Qatar, mwakani.

Advertisement

Wote tutakwenda Doha kwa ajili ya kumsaka bingwa mwingine wa dunia. Mwaka huo mwanasoka bora wa dunia ana asilimia kubwa ya kupatikana kutokana na michuano hiyo. Huwa inatokea nyakati fulani ambazo tunalazimika kusaka mwanasoka bora wa dunia kupitia michuano hiyo.

Nyakati hizi ambazo Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wamekwenda chini kuna uwezekano mkubwa tukapata mwanasoka bora wa dunia kupitia michuano hii ya Doha. Iliwahi kutokea mwaka 2006 wakati mastaa wakubwa walipoonekana kuchemsha mwaka huo, basi tukalazimika kumchagua beki aliyekuwa nahodha wa Italia, Fabio Cannavaro kuchukua kiti hiki.

Wakati huo kina Rivaldo na Luis Figo walikuwa wanakwenda chini. Zinedine Zidane ndio kwanza alikuwa ametoka katika kustaafu na kujaribu kuitafutia Ufaransa taji la pili la Kombe la Dunia. Haikuwezekana. Mechi ya fainali alimtandika mtu kichwa akatolewa kwa kadi nyekundu.

Kilichofuata kilikuwa ni kumpa tuzo hii Cannavaro ambaye anabakia kuwa mlinzi pekee kuwahi kutwaa tuzo hizi. Kama usingekuwa mwaka wa Kombe la Dunia sidhani kama Cannavaro angetwaa tuzo hii. waitaliano wenzake walimsaidia.

Naziona hizi dalili mwakani. Tunaweza kupata mwanasoka bora wa dunia kupitia michuano hii ya Doha. Sina uhakika kama mwaka huu nani anaweza kuchaguliwa, lakini siamini kama Neymar anaweza kuingia hata Top Three.

Karata anayoweza kuicheza ni Doha. Hapa kazi anayo. Inategemea Wabrazil watakuja vipi Doha. Bahati mbaya siwaoni wakiwa tishio sana kwa kutazama majina yao katika karatasi. Timu ambayo mpaka sasa inatisha katika karatasi ni Ufaransa wenyewe ambao ni mabingwa watetezi.

Sijui kocha wao anaweza kupanga vipi kikosi chao, lakini ni wazi kwamba Wafaransa ni tishio sana na kuna uwezekano mkubwa wakamsaidia Kylian Mbappe kuwa mwanasoka bora wa dunia kama watacheza kama vile wanavyotazamika katika majina yao.

Brazil? Sina uhakika sana. Wana watu wazuri lakini wengi kati yao wanakwenda chini. Willian yuko hoi pale London. Philippe Coutinho yuko hoi pale Catalunya. Namuona Vinicius akiwa anarukaruka tu pale Santiago Bernabeu huku Richarlison akiwa mchezaji pekee anayenipa moyo.

Neymar ananisikitisha. Anaweza kuwa kama Thierry Henry ingawa Neymar anasikitisha zaidi. Baada ya Messi na Ronaldo kumalizika ungeweza kudhani dunia ilikuwa inamsubiri Neymar kutawala peke yake kwa miaka mingi.

Tofauti yake na Henry ni kwamba Henry licha ya uhodari wake mkubwa lakini alikuwa akicheza katika zama za magwiji wengi waliokuwa katika ubora mkubwa. Figo, Ronaldinho, Rivaldo, Ronaldinho, Ronaldo de Lima na wengineo.

Neymar alikuwa na nafasi nzuri zaidi. Kwanza ana kipaji kikubwa zaidi ya Mbappe na wengineo. Tatizo lake la kwanza hatuwezi kumlaumu. Majeraha. Tatizo lake la pili ni matumizi mazuri ya Ubrazil wake. Sherehe za ndani kwa ndani katika majumba yake ya kifahari zimekuwa nyingi.

Wakati tukimsubiri Doha atakuwa na miaka 30. Ni nyakati ambazo mwanasoka anaweza kwenda chini muda wowote ule. Tazamia kwamba hizi ni dakika za mwisho kwa Neymar kutwaa tuzo hizi. Usitazamie kwamba atapanda juu zaidi na zaidi. Hapana. Atakwenda chini.

Msimu uliopita hatukuwa na tuzo hizi. Hata kama tungekuwa nazo bado Neymar asingepewa. Mtu aliyekuwa katika nafasi kubwa ya kuipata alikuwa Roberto Lewandowski. Niliandika hapa wiki chache zilizopita kwamba Wazungu waliamua kumnyima kwa makusudi tu. Kwanini wasinge-mpelekea nyumbani bila ya sherehe? Waliamua tu kutumia kisingizio cha corona kumnyima.

Itasikitisha sana kama Neymar ataondoka katika soka bila ya tuzo hizi lakini kuna kila dalili kwamba jambo hilo litatokea. Halafu kwa ninavyoona kuna kila dalili Mbappe ataihodhi tuzo hii kwa miaka mingi ijayo. Sioni mpinzani wa karibu katika tuzo hizi. Labda aibuke mtu kutoka kusikojulikana na kuwa mchezaji mkubwa ghafla.

Tazama wachezaji kama Eden Hazard walivyo leo. Pengo limekuwa kubwa kati yao na Mbappe. Hazard anaendelea kunenepa tu. Mbappe akienda Real Madrid mwishoni mwa msimu basi maisha yatakuwa magumu zaidi kwa Hazard.

Advertisement