Prime
NYUMA YA PAZIA: Mpaka sasa Pep, Palmer bado ngoma ni droo

Muktasari:
- Huyu huyu Kiyosaki ndiye yule mtunzi wa kitabu maarufu cha Rich Dad Poor Dad. Nimemkumbuka Kiyosaki na hapa mezani nina simulizi ya kiungo Cole Palmer na Pep Guardiola. Simulizi nyepesi ambayo imekuwa ikijirudiajirudia katika soka.
NI wewe, tena wewe peke yako ndiye ambaye utawajibika kwa machaguo na uamuzi katika maisha yako. Aliwahi kutuandikia mtunzi mmoja maarufu wa vitabu nchini Marekani, Robert Kiyosaki. Unashangaa jina? Usishangae sana. Ana asili ya Japan.
Huyu huyu Kiyosaki ndiye yule mtunzi wa kitabu maarufu cha Rich Dad Poor Dad. Nimemkumbuka Kiyosaki na hapa mezani nina simulizi ya kiungo Cole Palmer na Pep Guardiola. Simulizi nyepesi ambayo imekuwa ikijirudiajirudia katika soka.
Wakati mwingine kila mwanaume anapaswa kuchukua uamuzi mgumu. Fikiria namna ambavyo kwa sasa Cole Palmer ni staa mkubwa katika soka. Mmoja kati ya wachezaji hatari katika Ligi Kuu England. Anafunga kwa namna ambavyo anajisikia.
Miezi michache iliyopita alikuwa mchezaji wa Manchester City. Kinda. Kipaji kilikuwa wazi katika miguu yake. Akili ya mpira ilikuwa wazi kichwani kwake. Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 19. Uamuzi na chaguo vilipaswa kufanyika katika vichwa viwili. Kichwa cha Palmer na Pep.

Palmer alijihisi kwamba anaweza kucheza katika timu yoyote ya Ligi Kuu England. Aliamini katika kiwango chake. Usingeweza kumkatalia. Alitaka ama aanze kucheza Manchester City au aondoke kwenda kwingineko ambako angeweza kucheza.
Hadi kufikia pale sisi mashuhuda tulikuwa tunajua uwezo wake. Lakini sisi ni kina nani zaidi ya Pep ambaye alikuwa anashinda naye mazoezini? Lazima Pep alijua zaidi uwezo wa Palmer kuliko sisi. Hata hivyo Pep alipaswa kuchukua uamuzi ambao angewajibika nao zaidi siku za usoni.
Uwanjani katika ule upande wa Palmer walikuwepo Riyad Mahrez na Bernardo Silva. Pep asingeweza kumhakikishia Palmer nafasi ya kucheza mbele ya wakongwe hao ambao walikuwa hawamuangushi. Bahati mbaya kwake Palmer asingeweza kusubiri.

Inapofikia hatua hii kwa mtoto anayejiamini kama Palmer, hakuna unachoweza kufanya zaidi ya kumruhusu kuondoka. Inaweza kuwa kwa shingo upande lakini hakuna unachoweza kufanya zaidi. Unaweza kuumia sana wakati mchezaji mwenye umri mkubwa aliye katika ubora wake anapotaka kuondoka. Hauwezi kuumia wakati mchezaji mwenye umri wa Palmer anapotaka kuondoka.
Pep aliamua kumuuza Palmer kwa kiasi cha Pauni 40 milioni. Kwa wakati ule ilikuwa pesa nyingi kwa mchezaji ambaye bado hajathibitisha ubora wake katika Ligi Kuu England. Leo Palmer ni hadithi nyingine. Kwa kile alichokionyesha na kwa kuzingatia uraia wake wa Uingereza nadhani dau lake linaweza kuzidi Pauni 85 milioni.

Kuanzia pale Palmer ambaye Waingereza wanamuita Cold Palmer ameudhihirishia ulimwengu kwamba alikuwa sahihi kuondoka Manchester City. Sio tu kuondoka katika klabu yenyewe, lakini pia alikuwa sahihi kuondoka katika jiji lenyewe alilozaliwa la Manchester na kuhamia London.
Anajua kupiga chenga. Mtulivu. Anajua kufunga. Ana uamuzi wa busara uwanjani. Haitafika miaka 25 atakuwa mmoja kati ya wachezaji bora zaidi duniani kama Chelsea itampa sapoti uwanjani kwa kupata mafanikio katika michuano mbalimbali.
Tatizo kubwa lililopo ni kwamba mpaka sasa ngoma ni sare kati yake na Pep. Hii ni kwa sababu hakujawahi kuwa na sababu za msingi za kumlaumu Pep kwa kumruhusu Palmer kuondoka klabuni. Tangu Palmer ameondoka zake na kuwa mmoja kati ya wachezaji bora duniani, Pep ameendeleza moto wake uleule pale England na kwingineko.

Alipoondoka Palmer, Pep amekwenda kuchukua mataji matatu kwa mpigo (treble). Msimu uliofuata akatwaa tena ubingwa wa England. Unawezaje kulaumu uamuzi wake wa kumuondoa Palmer? Makali yake yameendelea kuwa vilevile.
Kuna hofu kwamba huenda Pep akaondoka mwishoni mwa msimu, lakini hata kama akiondoka hatuwezi kuwa wanafiki na kumlaumu kwa kumruhusu Palmer aende zake Chelsea. Ataondoka akiwa mmoja kati ya makocha bora zaidi kuwahi kutokea katika Ligi Kuu England. Atakumbukwa pia kwa kuchukua uamuzi mwingi bora. Hatuwezi kumkumbuka kwa tukio la Palmer.
Wakati mwingine iliwahi kutokea huko nyuma. Iliwahi kutokea kwa Sir Alex Ferguson wakati Paul Pogba alipolazimisha kuondoka klabuni kwa sababu hakuiona nafasi yake mbele ya Paul Scholes. Pogba alikuwa kinda anayejiamini kwamba angeweza kung’ara kwingineko.

Sir Alex asingekubali kwa haraka haraka kumhakikishia nafasi Pogba mbele ya Scholes ambaye alikuwa katika ubora wake. Bahati nzuri kwa Pogba ni kwamba hakupata sana mushkeri katika kuondoka kwa sababu alikuwa anaelekea kuwa mchezaji huru.
Wachezaji wengine ambao hawakuweza kujitanua katika nafasi zao wakiwa makinda na wakalazimika kutimkia kwingineko ni pamoja na Kevin De Bruyne na Mohamed Salah wakati walipokwenda Chelsea. Nafasi zao zilikuwa zimejaa na wakati ule usingeweza kuwalaumu Chelsea kwa kutowapatia nafasi uwanjani.
Pep na Palmer wamenikumbusha kauli ya Kiyosaki kwamba kila mmoja atawajibika kwa uamuzi wake katika maisha. Ni kweli kila mmoja amewajibika kwa uamuzi wake, lakini mpaka sasa sijaona ambaye anapaswa kulaumiwa.
Palmer ametumia nafasi yake vyema kuondoka City. Huenda kuna wachache ambao wangeweza kumlaumu kuwa ameondoka katika mikono ya mmoja kati ya makocha bora duniani. Hata hivyo, amefanikiwa kujitengenezea ufalme wake binafsi pale Stamford Bridge.
Upande wa Pep nadhani tangu aanze kufundisha soka huwa hatuna cha kumlaumu kwa kuwapoteza wachezaji kama Palmer. Sio tu kinda kama Palmer, lakini aliwahi kuchukua uamuzi mgumu wa kuwapoteza baadhi ya wachezaji wakongwe kama Ronaldinho, Samuel Eto'o, Deco De Souza na Zlatan Ibrahimovich, lakini uamuzi wake wote ukaonekana kuwa sahihi.
Kwa hili la Palmer na yeye nadhani mpaka sasa hivi ni ngoma droo. Hakuna mshindi. Kila mtu amewajibika kwa uamuzi wake. Na hata mmoja akifanikiwa zaidi kuanzia sasa bado mwenzake hatakuwa na kitu cha kujutia katika siku za usoni.