Nyota watano Simba wanafunika VPL yote

Muktasari:

UMESOMA msimamo wa Ligi Kuu Bara? Simba ipo kileleni ikiwa imekusanya pointi 61 kwenye michezo 25, imeshinda 19, sare nne, imepoteza mechi mbili, wamefunga mabao 58 na wamefungwa 10.

UMESOMA msimamo wa Ligi Kuu Bara? Simba ipo kileleni ikiwa imekusanya pointi 61 kwenye michezo 25, imeshinda 19, sare nne, imepoteza mechi mbili, wamefunga mabao 58 na wamefungwa 10.

Hao ndio Simba, mabingwa watetezi wa ligi hiyo, ambao ukikutana nao ujipange kutokana na ile safu yao hatari ya ushambuliaji, unafungwa muda wowote.

Kwenye mechi 25 walizocheza wababe hao wa Msimbazi, wamefunga mabao mengi kuliko timu nyingine yoyote ile kwenye ligi hiyo huku mastaa wake watano, Meddie Kagere, John Bocco, Chriss Mugalu, Luis Miquissone na Clatous Chama wakisimamia shoo nzima.

Ni mabao 15 tu kwenye kikosi cha Simba ndiyo ambayo hayajafungwa na wakali hao watano.

Kagere amefunga 11, Bocco (10), Mugalu (8), Miquissone (8) na Chama (6).

Hiyo ndiyo fowadi anayotamba nayo Didier Gomes, ambapo mabao yao yana maajabu mengi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.


Yanazidi mabao yote ya Yanga

Mabao ambayo wamefunga washambuliaji hao watano yamekwenda kuleta maajabu katika kikosi cha Yanga ambacho kipo katika mbio za ubingwa msimu huu.

Kikosi kizima cha Yanga mpaka sasa katika ligi kimefunga jumla ya mabao 41, ambayo yanakuwa mawili pungufu ya yale ambayo wamefungwa washambuliaji hao watano wa Simba.

Kiujumla, hakuna timu nyingine ya VPL hadi sasa inayofikia mabao ya wakali hao watano wa Simba. Azam nzima ina mabao 40. Hamna timu nyingine inayokaribia mabao 40, ya jirani zaidi ni KMC yenye mabao 31. Inaonyesha kiasi gani kuwa Simba msimu huu ina kasi kubwa ya ufungaji mabao katika kikosi chao kwani wachezaji watano wamefunga idadi kubwa ya mabao ambayo inashindwa kufikiwa na timu ambazo wanakimbizana nazo katika kuwania ubingwa.


Mtibwa + Kagera Sugar = mabao 38

Washambuliaji hao wameweka maajabu mengine katika ligi kwani timu mbili zinazomilikuwa na kiwanda cha sukari wameshindwa kufikia idadi ya mabao hayo.

Mtibwa Sugar wamefunga mabao 13 wakati Kagera Sugar wamefunga 25, na ukijumlisha zote mbili maana yake watakuwa wamefunga mabao 38 mpaka sasa.

Timu hizo zinazomilikiwa na kiwanda cha sukari watakuwa na wakati mgumu kufikia idadi ya mabao ambayo wamefungwa na wakali hao kutokana na kushindwa kupata matokeo mazuri msimu huu.


Timu za

Halmashauri zimewazidi

mawili tu

Katika ligi kuna timu mbili ambazo zinamilikiwa na Jiji kutoka katika mikoa mbalimbali.

Timu hizo ni KMC ambayo ipo Dar es Salaam pamoja na Mbeya City iliyopo pale Mbeya.

Katika msimamo KMC wao wamefunga mabao 31, wakati Mbeya City (14), jumla yake 45, kwa maana hiyo timu hizo mbili zimewazidi mabao mawili washambuliaji hao wa Simba.

Kutokana na ukali wa ufungaji mabao ambao washambuliaji hao wa Simba wameonyesha msimu huu halitakuwa jambo la kushangaza kufikia idadi hiyo na kuwapita kutokana na hali ya Mbeya City msimu huu kusuasua.


Dube na Azam nzima hawaoni ndani

Straika wa Azam, Prince Dube ndiyo kinara wa ufungaji katika ligi akiweka kambani mabao 12.

Mabao hayo 12, ambayo amefunga Dube ukijumlisha na 28 ambayo wamefunga wachezaji wengine wa kikosi hicho maana yake hawaoni ndani kwa mastraika hao watano wa Simba.

Ndio, Dube ni mnyama hatari katika kutupia mabao, lakini tatizo hana pacha ya kutosha kumpa sapoti ya kushindana na wakali hao wa Simba.

Mwanaspoti limeongea na Dube na anasema kasi ya ufungaji ya Kagere inamfanya yeye kuwa bora na kuendelea kujindaa vya kutosha katika kila mechi.

“Natamani kufanya vizuri msimu huu kuisaidia timu yangu ya Azam kufikia malengo yake na jambo hilo linachangiwa na ukali ambao unaonyeshwa na washambuliaji wengine kama Kagere,” anasema Dube.


Timu 17+1

Wakali hao watano wamezifunika timu nyingine zote 17 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara kwa mabao au unaweza kusema wamewafunika hadi nyota wenzao zaidi ya 20 wa Simba walionao kikosi kimoja, ambao hao wengine kwa ujumla wao wameifungia timu hiyo ya Msimbazi mabao 15 tu. Ukiacha Yanga (mabao 41) na Azam (40), timu nyingine zote zilizobaki zimefunga mabao kuanzia 31, na kushuka chini.


Wasikie hawa

Kagere anasema kikubwa ambacho amejiwekea ni kufikisha idadi ya mabao 22, ambayo alimaliza nayo msimu uliopita na baada ya hapo ataweka malengo mengine ya matamanio.

“Malengo ya matamanio ni pamoja na kufikisha mabao 23, ambayo nilifunga msimu wangu wa kwanza lakini natamani kufanya yote haya ili kuisaidia timu yangu kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara nyingine msimu huu,” anasema Kagere.

Kocha wa Simba, Didier Gomes da Rosa anasema makali yanayoonyeshwa na safu yake ya ushambuliaji ni ushirikiano ambao unapatikana kutoka kwa wachezaji wengine pia.

“Ukali huo wa kufunga ambao washambuliaji wangu wameonyesha unaturahisishia kupata matokeo katika kila mechi na kufanya vizuri kwenye mashindano yote ambayo tunashiriki msimu huu,” anasema kocha huyo Mfaransa.