Nkane Kinda anayetikisa TPL

KAMA kuna ndoto anaitamani itimie winga wa Biashara United, Denis Nkane (18), ni kuona anapata nafasi ya kuitumikia timu ya Taifa ‘Taifa Stars kabla ya kupata nafasi ya kukipiga nje.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Nkane anafunguka namna anavyotamani kuandika rekodi ya kuwepo kwenye kumbukumbu za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa mchezaji mwenye mchango Stars.

Anasema hayo baada ya Watanzania kuanza kumtupia jicho, alipofunga bao dhidi ya Djibouti mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika, kwamba anatamani kutuzwa nyumbani kisha nje.

“Wengi wamenijua baada ya kuifungia timu yangu bao dhidi ya Djibouti na hiyo imetokana na ugeni wangu kwenye ligi, kwani nimepandishwa dirisha dogo kutoka kikosi B na kocha Francis Baraza, mwaka jana, kabla hajatimkia Kagera Sugar,” anasema.

Kabla ya kufunga bao akianzia benchi, anasema kocha alikuwa anamuelekeza kitu cha kufanya mbele ya mabeki wa Djibouti na alifanikiwa kutekeleza maelekezo hayo

“Baada ya kuingia kipindi cha pili nilijua nitafunga, kwani tayari nilielewa maeneo ya kupenya baada ya kocha kuniibia siri hiyo.”

WINGA FUNDI

Kuhusu mshambuliaji wa pembeni anayemhusudu anamtaja aliyekuwa winga wa Simba, Luis Miquissone namna alivyokuwa anapenda aina ya upambanaji wake anaoamini ndio umempa nguvu kuitumikia klabu kubwa Afrika, Al Ahly ya Misri.

“Miquissone alikuwa na kipaji cha aina yake. Hakuishia hapo alionyesha bidii ya kukifanya kipaji chake kiwe bora. Nilijifunza kitu kutoka kwake, ila kwa upande wa mabeki ninamkubali sana Pascal Wawa ni mtulivu na humpiti kirahisi,” anasema.


KUBWA YA KWANZA

Nkane anasema mara ya kwanza kushika pesa kubwa ilikuwa Sh80, 000 aliyoipata akiwa na timu ya Market United ya Njombe ikiwa Daraja la Kwanza. “Pesa hiyo nilipata mwaka 2018. Ilinipa nguvu ya kupambana hadi hapa nilipo leo, ambapo kwa sehemu naona soka limenipa mwanga wa maisha yangu ya baadae,” anasema.

Nje na hilo, anasema soka limempa watu wapya ambao wanaendelea kuifanya akili yake ikue na kuwaza makubwa kwenye kazi hiyo.


SHUKRANI KWA BARAZA

Kinda huyo anamshukuru kocha Baraza ambaye kwa sasa yupo Kagera Sugar kumwamini na kumpandisha timu ya wakubwa, ambako anaona kipaji chake kitazidi kuonekana.

“Hakuna wakati mgumu ambao niliupata mbele ya kocha Baraza kama mechi ya mzunguko wa pili (wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita) ambayo tuliwafunga nyumbani (Kagera Sugar), alinifundisha nikajikuta namwadhibu (Baraza) maana alihitaji sana matokeo na sisi kocha wetu Odhiambo alihitaji tufunge ili tumalize nafasi ya nne.”


KOCHA, NAHODHA WAMZUNGUMZIA

Nahodha wa timu hiyo, Abdulmajid Mangalo anakitazama mbali kipaji cha Nkane na kumshauri kujikita katika bidii na nidhamu kwani ndivyo vitakavyomsaidia kufika mbali.

“Kocha Baraza alikiona kipaji chake, naamini akizingatia anayoelekezwa na makocha milango ya kutoboa kwake ipo wazi, kubwa zaidi ni nidhamu,” anasema Mangalo.

Kocha Baraza aliyempandisha toka kikosi B, anasema alikiona kipaji cha Nkane akifanya mazoezi na timu ya mtaani akamchukua na kumuendeleza.

“Wakati nafika Musoma nilimkuta anacheza timu ya maveterani kwa nidhamu ya hali ya juu. Alikuwa anajituma sana kwenye mazoezi nikamchukua ili nimuongezee ujuzi na kujiamini,” anasema Baraza.

“Mechi ya ligi ya kwanza niliyompanga ni dhidi ya Simba, nilitumia mfumo wa mabeki watatu, aliwasumbua sana Chikwende na Gadiel Michael hadi kipindi cha pili walimuingiza Tshabalala.”

Anasema Nkane alikuwa anacheza winga, lakini alimbadilisha kucheza beki wa pembeni, kutokana na kimo chake.

“Ninamuona mbali kutokana na bidii yake na nidhamu. Ipo siku atakuwa lulu mbele ya timu zinazopendwa na wachezaji wengi Tanzania,” anasema.