NJE YA BONGO: Shafii aanza kulipwa Uturuki

HATIMAYE mchezaji kinda wa Kitanzania, Shafii Omary Lumambo amepewa mkataba wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa ikiwa ni kipindi kifupi tu tangu ajiunge na akademi ya Tuzlaspor inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Uturuki maarufu kama TFF First League.

Kinda ambaye anafanya balaa kwenye ligi ya vijana nchini humo kwa kutoa asisti tano na kupachika mabao mawili, ni zao la taasisi ya African Youth Empowerment (AYE) ambayo imejikita katika kuvumbua na kuendeleza vipaji kwa kuvitafutia fursa zilizopo kulingana na mtandao walionao.

Shafii amesaini mkataba wa miaka miwili na wababe hao wanaopambania nafasi ya kupanda daraja, akiongea na Nje ya Bongo, kinda huyo alisema hiyo ni nafasi ambayo alikuwa akiipambania tangu alipotua nchini humo.

“Kusaini mkataba wangu wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa ni jambo kubwa sana kwangu pamoja na familia yangu, sasa nimekuwa mchezaji wa kulipwa kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa AYE ambao waliniona kuwa ninaweza na kunitafutia fursa ya kupigania ndoto zangu,” alisema kinda huyo na kuongeza;

“Najua kuwa bado ninasafari ndefu kwa sababu kusaini ni jambo moja, nachotakiwa ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili nipige hatua zaidi, natamani kucheza kwenye ligi na timu kubwa zaidi Ulaya.”

Kocha wa Tuzlaspor, Bekirrtegun ambaye aliwahi kutamba akiwa na Fenerbahce ya nchini humo, amemuongelea kinda huyo kwa kusema ni mchezaji mzuri ambaye anatakiwa kuendelea kukuzwa vyema ili klabu hiyo inafuaike naye kwa miaka michache ijayo.

“Hatuwezi kuharakisha kuanza kumtumia kwenye kikosi cha kwanza, ni mchezaji mzuri ambaye anahitaji muda ili kuendelea kukua zaidi kisoka, nimekuwa nikivutiwa naye na ndio maana nimekuwa nikimpa nafasi ya kufanya mazoezi na kikosi changu cha kwanza,” alisema kocha huyo.

Licha ya kuwa mdogo kiumri, Shafii (18) amekuwa akitumika kwenye kikosi cha umri wa miaka 19 na kuwa mchezaji wa kutumainiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya African Youth Empowerment, Muyimba Gerald akiongelea hatua ya kijana wao, alisema ni fahari kwao na hiyo wamepokea kama chachu ya kuendelea kujitoa zaidi kuhakikisha wanasaidia vijana wengi zaidi wa Kitanzania.

“Shafii ni kijana mwenye nidhamu kubwa na ndio maana amaweza kupiga hatua kwa haraka sana mbali na kipaji alichonacho, binafsi nilitegemea hilo na nilimweleza kabla hajaondoka kuwa wewe ni Mbwana Samatta ajaye kwenye nchi yetu, kama taasisi tuna furaha sana na tunaamini kuwa tutawapata wachezaji wengine wenye vipaji vikubwa kwa ajili ya kuwasaidia,” alisema.

Muyimba alidokeza mwakani, 2024 watakuwa na mchakato wa kutafuta vipaji huku wakitegemea kuwa na kundi kubwa zaidi la mawakala kutoka Ulaya kwa ajili ya zoezi hilo, pia watakuwa na ujenzi rasmi wa kituo chao.