NIONAVYO: Wimbi jipya-kubahatisha michezo kuliko kucheza
Muktasari:
- Alikuwa na kalamu na karatasi mkononi akifuatilia michezo iliyokuwa inafuata jioni hiyo.
‘Kuishi kwingi ni kuona mengi.’ Waswahili walisema. Juzi baada ya mchezo wa CAF wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kati ya Yanga dhidi ya Al Hilal ya Sudan, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar Es Salaam, dada mmoja anayefanya kazi saluni ya kunyolea nywele alionekana kuwa bize sana.
Alikuwa na kalamu na karatasi mkononi akifuatilia michezo iliyokuwa inafuata jioni hiyo.
Nilimchokoza kujua inakuwaje ana mapenzi na timu za kutoka nje ya Tanzania na ambazo si wengi wamewahi kuzisikia.
Majibu yake yalinishangaza; alisema yeye timu hazijui na wala soka hapendi kihivyo, ila betting, michezo ya kubahatisha, ndiyo inamlazimisha kufuatilia kwa karibu.
Kutokana na yeye, nikajua namna vijana wengi na hata watu wazima walivyokamatwa na michezo ya kubahatisha huku wengi wakiifanya njia yao rasmi ya kujiingizia kipato na wengine wakiwa wamepata uraibu kutokana na ubashiri.
Kwa haraka nikaona tuna uwezekano mkubwa wa kuwa na wachezaji wengi wa michezo ya kubahatisha kuliko wanamichezo.
Nahisi hatari inayokuja iwapo wanamichezo nao wataingia kwenye michezo ya kubahatisha.
Kamari, upatu, michezo ya kubahatisha, bahati nasibu, kubeti na majina mengine mengi ambayo mwishowe yanarudi kwenye maana moja kuwa ni michezo ya kubahatisha kwa njia ya kubashiri matokeo na matukio.
Kumbukumbu za maandishi zinaonyesha kamari ikichezwa katika China ya zamani karibu miaka 4,000 iliyopita
Kutokana na utandawazi uliochagizwa na kubadilika kwa teknolojia, kamari inachezwa kisasa ikiwa pia imevuka mipaka ya ardhi, anga na bahari.
Sasa kamari inachezwa na mtu bila kwenda kwenye nyumba za kamari maarufu kama Cassino, ambazo waitaliano walizianzisha miaka 400 iliyopita.
Wanaocheza hawahitaji kufahamiana tena. Kila mtu anacheza kwa wakati wake kutoka kwenye kompyuta yake au kwenye simu ya kiganjani mwake.
Kamari ya asili ilitabiri mambo mengi ya kiroho na asili mfano matendo ya miungu kama kunyesha kwa mvua, kuchomoza kwa jua, magonjwa, vifo, kuandama kwa mwezi, kuonekana kwa nyota na mengine mengi, lakini ubashiri wa matokeo na matukio ya michezo umechukua umaarufu kuliko ubashiri wa matukio mengine kwa sasa.
Kampuni kubwa na watu binafsi wamewekeza pesa nyingi katika kutangaza masoko na kuibua teknolojia mpya za kuendesha biashara za ubashiri hasa kuhusu matokeo na matukio katika michezo.
Kama ilivyo kamari kwa jumla wake, ubashiri katika michezo umeanza miaka mingi iliyopita, mfano katika dola ya kirumi huko Roma inasemekana ubashiri ulifanyika katika mashindano ya farasi.
Inasemekana ubashiri kwenye michezo ulifanyika pia kwenye michezo ya asili ya Olimpiki ya wayunani au wagiriki.
Shirika la IMARC linalojihusisha na utafiti wa masoko na biashara linaeleza thamani halisi ya uwekezaji katika sekta hii kwenya soka duniani ni takribani Dola za Kimarekani 3.2 bilioni na inategemewa kufikia hadi Dola 4bilioni ifikapo mwaka 2028. Katika michezo, bado kamari imekuwa ni rafiki wa mashaka kwa wanamichezo na michezo.
Pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na kampuni hizi za kubeti, kamari haijawahi kuwa rafiki wa kuaminika wa michezo.
Huko nyuma, michezo ya farasi ilikuwa maarufu zaidi katika kamari, tulisikia kashfa za waendesha farasi au wamiliki wa farasi kushiriki katika kupanga matokeo kutokana na ushawishi wa wacheza kamari.
Matokeo ya michezo huwa hatarini kuvurugwa pale wahusika wa michezo kama wachezaji, waamuzi makocha na wadau wengine wakijihusisha katika michezo ya kubashiri bila kufuata maadili.
Michezo hii ya kubashiri ina taswira tofauti kwa wanamichezo.
Vyama mbalimbali vya michezo ikiwemo shirikisho la soka ulimwenguni, FIFA, linapinga vikali wanamichezo ikiwemo makocha,waamuzi na benchi la ufundi kujihusisha katika michezo hiyo.
Hii inatokana na uwezo wa wahusika hao kuamua dira ya mchezo au matokeo ya mwisho ya mchezo. Hivyo basi, FIFA imeunda sheria kali endapo itachunguzwa na kubainika mhusika kati ya hao waliotajwa amejihusisha na michezo ya kamari moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Njia ya moja kwa moja inahusisha mchezaji au mwamuzi kuweka pesa mwenyewe kwenye mchezo wa ubashiri.
Njia isiyo ya moja kwa moja ni pale mtu ambae si moja wa wahusika waliolezwa hapo juu akishiriki kwenye kamari kwa pesa ya mhusika kati ya hao waliokatazwa na FIFA na kisha kugawana faida na mhusika akivujisha taarifa nyeti inayoweza kutumika katika michezo hii ya kubashiri.
Kutokana na sheria za maadili za FIFA, mtuhumiwa akigundulika wazi kushiriki katika michezo ya kamari anaweza kupigwa faini na kuzuiwa kushiriki katika shughuli zozote za mpira wa miguu kwa kipindi kirefu.
Hukumu inaweza kutofautiana ukubwa kutokana na maelezo ya upande wa utetezi.
Wanasoka mbalimbali wamekumbana na sheria hii akiwemo aliyekuwa mshambuliaji wa klabu ya Liverpool na timu ya taifa ya uingereza Daniel Sturridge, beki wa Newcastle na timu ya taifa ya uingereza Kieran Trippier, na hivi karibuni kabisa mshambuliaji wa klabu ya Brentford Ivan Toney.
Baadhi ya athari za kucheza kamari kwa wanamichezo ni pamoja na kupata msongo, urahibu na hasara za kifedha ikiwemo madeni na hata kufilisika.
Hapa kwetu, michezo ya kubahatisha imetamalaki kama ilivyo kwingine duniani na labda niseme kuliko ilivyo katika nchi nyingi za Bara la Afrika.
Kampuni za michezo hii zinazidi kuongezeka kila uchwao na matangazo ya biashara ya kampuni ziko hewani katika kila radio, televisheni, magazeti na mabango barabarani.
Katika nchi ambayo wengi wa wanamichezo wanaweza kuchukuliwa kama watu wasio na ajira kutokana na kupata ujira mdogo au uchezaji wao kuwa wa ridhaa hali hii inaweza kuwa hatari kwa wachezaji binafsi na maendeleo ya michezo kwa jumla.
Nionavyo mimi, elimu, tahadhari na hata adhabu kwa wanamichezo na taasisi za michezo kuhusu suala zima la michezo ya kubashiri haijatolewa kwa kiasi cha kutosha.
Wakati muafaka wa kuelimisha wanamichezo kuhusu madhara ya michezo ya kubashiri ni sasa, vinginevyo juhudi zote za kusukuma mbele michezo zinaweza kuishia bure kufumba na kufumbua.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.