Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Tusisubiri mtu afe uwanjani

Nionavyo Pict

Muktasari:

  • Kwa muda mrefu tabia za wahuni michezoni zilichangia kubebeshwa lawama na faini kwa klabu na chama cha mpira cha England, FA. Baadhi ya nchi na mamlaka za michezo ziliruhusu idadi ndogo ya tiketi kuuzwa kwa mashabiki wa Uingereza kwenye matukio makubwa kwani ilihofiwa fujo zitatokea kama ilivyokuwa kawaida yao.

HAKUNA kitu kilichochafua taswira ya mpira wa Uingereza katika karne iliyopita zaidi ya vitendo vya wahuni viwanjani au kwa lugha yao wanawaita hooligans. Hooligans hawa walifanya vurugu ndani na nje ya Uingereza. Kila ziliposafiri klabu za Uingereza na hata timu ya taifa, hooligans walikuwapo na walikuwa tayari kuwafanyia fujo mashabiki wa timu pinzani, kuharibu miundombinu na kuharibu matukio husika.

Kwa muda mrefu tabia za wahuni michezoni zilichangia kubebeshwa lawama na faini kwa klabu na chama cha mpira cha England, FA. Baadhi ya nchi na mamlaka za michezo ziliruhusu idadi ndogo ya tiketi kuuzwa kwa mashabiki wa Uingereza kwenye matukio makubwa kwani ilihofiwa fujo zitatokea kama ilivyokuwa kawaida yao.

Madhara ya vitendo vya wahuni ni pamoja na kuharibu matukio, kuharibu miundombinu kama ya viwanja na barabara, kujeruhi raia na walinzi wa usalama na wakati mwingine kusababisha vifo. Mwaka 1964 lilitokea tukio la kusikitisha lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 300 baada ya fujo zilizoanza pale refarii alipolikataa bao la kusawazisha la wenyeji Peru dhidi ya Argentina kwenye mashindano ya kufuzu ushiriki wa Michezo ya Olimpiki. Huo ni mfano tu kati ya matukio mengi yaliyogharimu maisha kutokana na vurugu za viwanjani.

Kuwapo kwa kamera viwanjani, tiketi kuuzwa kwa mashabiki waliokaa kwenye viti vyenye namba, mafunzo maalum kwa polisi na upigaji marufuku kuingia viwanjani kwa hooligans waliotambulika, kulisaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na vitendo hivyo.

P 01

Matukio ya siku ya Jumapili kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika uliozikutanisha timu za Simba SC na CS Sfaxien ya Tunisia ulinirudisha kwenye enzi za utawala wa hooligans katika soka la Uingereza. Sitaki kueleza kwa undani kilichotokea uwanjani, yametolewa matamko mbalimbali na wahusika mbalimbali kuanzia kwa waziri anayehusika na michezo na kuongoza wizara inayomiliki uwanja, Jeshi la Polisi na klabu ya Simba. Kwa ufupi vilifanyika vitendo vya kihuni na vya kutia hasara rasilimali za nchi. Hakuna utetezi wowote unaoweza kuhalalisha vitendo vya mashabiki kuharibu miundombinu ya Uwanja wa Taifa wa Benjamin William Mkapa.

Matukio ya vurugu yalifuatia matokeo ya mchezo kati ya timu hizo mbili. Waliokuwa wanapinga matokeo walikuwa ni wageni mbao kwa kweli walikuwa wachache na wangeweza kudhibitiwa na polisi na wahudumu wa uwanja. Unajiuliza mashabiki wa kwetu badala ya kukaa pembeni na kusherehekea ushindi, wanakuwa wa kwanza kung'oa viti. Walitaka na walipata nini mashabiki hawa? Wageni wanakuja kwako wanazozana na hawajakugusa, halafu wewe unaamua kung'oa samani za nyumba yako.

P 02

Wageni wakishaondoka unaingia gharama ya kurekebisha samani ulizoharibu mwenyewe.

Nimewahi kuandika huko nyuma kuhusu fahari tuliyo nayo kama taifa kuwa na miundombinu mizuri ya kimichezo kiasi cha kutoenda kuazima viwanja kwa majirani zetu.

Laiti mashabiki hawa wangejua kadhia wanayopata majirani zetu kwa kusafiri kilometa nyingi mbali na nyumbani ili kucheza mchezo wa nyumbani kwenye viwanja vinavyokubalika na CAF au FIFA, wasingethubutu kufanya yale. Siyo siri, majirani zetu wa Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya na Msumbiji wamekuwa na wakati mgumu wakati wa michezo yao ya kimataifa kwa sababu ya kutokuwa na miundombinu yenye hadhi inayokubalika.

P 03

Kuwa na miundombinu mizuri na kuwa na mazigira rafiki ni vitu viwili tofauti. Fujo za viwanjani na hata nje ya uwanja zinaweza kushusha hadhi ya nchi kiasi cha kuzuiwa kuingiza mashabiki au hata kuzuiwa kuwa wenyeji wa mashindano mbalimbali.

Tanzania kwa kushirikiana na majirani zake wa Kenya na Uganda imepewa uenyeji wa mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027. Kwa matukio ya namna hii tunawakaribisha au tunawafukuza wageni? Vipi wabaya wetu wakijenga agenda ya siri dhidi ya uenyeji wetu tutakuwa na la kujijitetea?

Pamoja na kwamba vitendo vya namna hii viliwahi kutokea huko nyuma lakini taswira ya Uwanja wa Mkapa na ya mashabiki wetu kwa muda mrefu imekuwa ya kusifiwa kiasi cha kupokea matukio makubwa kama lile la ufunguzi wa African Football League lililovutia vyombo vya habari vya kimataifa na kuhudhuriwa na wageni wengi mashuhuri akiwamo Rais wa Fifa, Giani Infantino. Taswira ya uwanja na mashabiki wetu ikififia, haitakuwa kazi rahisi kuisafisha.

P 04

Vitendo vya kihuni tumeviona katika baadhi ya mataifa na kwa kweli katika safu hii tumekuwa tukiiomba CAF kuingilia kati. Hata hivyo, utakuwa ni ujinga kuiga vitendo visivyo vya kistaarabu kama kuwasha moto viwanjani, kupiga mafataki, kuwamulika wachezaji na mionzi mikali machoni na hata kuwashambulia waamuzi. Huo ni ushamba na utatugharimu na kuzigharimu timu zetu zitakapoadhibiwa au kulazimika kucheza bila ya mashabiki uwanjani.

Kuelekea mashindano makubwa yajayo, serikali imeandaa bajeti kubwa ya miundombinu ya michezo. Sidhani kama itakuwa ni busara kutumia fedha ambazo zingesaidia huduma za afya, elimu, maji na kadhalika kujenga miundombinu hii iwapo watumiaji wake wanaanza utamaduni wa uharibifu.

Shirikisho la mpira wa miguu na jeshi la polisi nao pia wajitathimini kutokana na vitendo vilivyotokea kwenye mchezo huo. Pamoja na kuwapo kwa polisi na wahudumu wa uwanjani (stewards), bado mashabiki wachache na wachezaji wa timu ya CS Sfaxien waliweza kuanzisha na kufanya zogo ambalo limetugharimu. Najiuliza kama tumejiandaa vya kutosha kuhakikisha matukio yanayohatarisha usalama viwanjani yanadhibitiwa vilivyo. Mamlaka husika zilenge kuwadhibiti mashabiki mmoja mmoja wenye tabia za kihuni kwa kuwazuia kuingia uwanjani na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria. Wakati mwingine adhabu za jumla kama klabu kutozwa faini zimekuwa hazina tija sana.

P 05
P 05

Viwanja vipya na vya zamani vielekezwe kwenye kuwa na mashabiki waliokaa na tiketi zinazowatambulisha.

Elimu ya mara kwa mara itolewe kwa mashabiki kuhusu kuwa wastaarabu muda wote huku kila shabiki akiwa mlinzi wa mwenzake.

Hatua kali za makusudi zikichukuliwa dhidi ya wote wanaojihusisha na vitendo vya kihuni uwanjani tunaweza kudhibiti tatizo likiwa bado changa. Tudhibiti kabla vitendo hivi havijagharimu maisha. Tusipoziba ufa tutajenga ukuta.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.