NIONAVYO: Serikali isaidie ligi, klabu Zanzibar

Muktasari:
- Timu ya taifa ya Zanzibar au Zanzibar Heroes iliibuka mabingwa kwa kuwafunga wageni wao Burkina Fasso kwa magoli 2-1 katika mechi ya fainali. Timu nyingine zilizoshiriki ni Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) na Kenya (Harambee Stars).
MASHINDANO ya Kombe la Mapinduzi kwa mwaka 2025 yalifanyika kwa mafanikio makubwa kisiwani Pemba. Tofauti na miaka ya hivi karibuni ambako klabu kutoka ndani na nje ya Tanzania zilichuana, mwaka huu mashindano yalishirikisha timu za Taifa.
Timu ya taifa ya Zanzibar au Zanzibar Heroes iliibuka mabingwa kwa kuwafunga wageni wao Burkina Fasso kwa magoli 2-1 katika mechi ya fainali. Timu nyingine zilizoshiriki ni Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) na Kenya (Harambee Stars). Waalikwa wengine yaani Uganda na Burundi walijitoa katika dakika za mwisho.
Kufuatia ubingwa wa Zanzibar Heroes, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi aliandaa dhifa kwa heshima ya timu hiyo. Ukiachia mbali sherehe hiyo, Rais Mwinyi alikabidhi kitita cha shilingi milioni 50 kwa timu hiyo, hizi zikiwa ni mbali na milioni 70 walizopata kutoka kwa waandaaji.
Rais Hussein Mwinyi alikwenda mbele zaidi na kuahidi kuwaunganisha wachezaji wa timu ya Taifa na mawakala wa klabu za Uturuki ili waweze kucheza katika Ligi Kuu ya Turkiye huko Ulaya. Hii ni habari njema na kwa kweli ilionyesha namna gani serikali ya Mapinduzi inachukulia kwa uzito maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu unaopendwa sana visiwani Zanzibar.

Mchango wa Zanzibar katika maendeleo ya mpira wa Tanzania na hata nje ya Tanzania ni mkubwa. Wachezaji wengi kutoka Zanzibar wanacheza na kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Tanzania na wengine sasa wanacheza nje ya Tanzania. Wataalam wa ufundi kama makocha, waamuzi na madaktari wa tiba za michezo kutoka Zanzibar wamefanya vizuri katika viwango vya taifa mpaka viwango vya FIFA.
Kwa tunaofuatilia kwa karibu historia na maendeleo ya mpira wa miguu wa Zanzibar, hatukushangazwa na kufanya vizuri kwa Zanzibar Heroes. Zanzibar inaweza kufanya vema zaidi kama Rais mwinyi ataamua kuendelea na dhamira yake nzuri kwa kuweka mifumo mizuri itakayowezesha maendeleo endelevu ya mchezo huo.

Timu ya taifa ya Zanzibar inafanya vizuri wakati ni muda mrefu umepita tangu ishiriki mashindano yoyote rasmi. Kumbuka huko nyuma timu ilicheza kila mwaka kwenye mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Challenge) ambayo bahati mbaya kwa miaka ya hivi karibuni yamekuwa hayafanyiki. Zanzibar ilianzisha chama cha mpira mwaka 1926 ikiwa ni takribani miaka 20 kabla ya kuundwa kwa chama cha soka Tanzania bara. Tunaweza kusema Zanzibar ni kitovu cha mpira wa miguu kwa ukanda huu.

Zanzibar ni mwanachama mshiriki (Associate Member) wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika yaani CAF. Kwa hadhi hiyo, Zanzibar inaweza tu kushiriki mashindano ya klabu Afrika yaani Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho. Hii ni nafasi muhimu sana inayoweza kuutangaza mpira wa Zanzibar na pia kuwapa nafasi vijana wa Zanzibar kuonekana katika nyanja za kimataifa. Kwa bahati mbaya klabu za Zanzibar zimekuwa zinashiriki kwa kusuasua katika mashindano haya ya CAF. Baadhi ya sababu zinazotolewa kwa kutofanya vizuri kwa klabu za Zanzibar ni ukosefu wa fedha na changamoto ndogo katika ligi ya Zanzibar.
Hata hivyo, uzoefu wa ushiriki wa timu ya Malindi FC kwenye mashindano ya Kombe la Washindi mwaka 1994 ni Ushahidi kwamba zikipata maandalizi makini, timu za Zanzibar zinaweza kufanya vizuri na hata kufikia kushawishi CAF kuongeza idadi ya timu.

Litakuwa jambo jema sasa serikali ya Mapinduzi, pamoja na kuwekeza katika miundombinu ya mpira wa miguu, iwekeze katika Ligi Kuu ya Zanzibar ili kuweka mazingira ya kuvutia uwekezaji katika ligi hiyo.

Klabu za Zanzibar zinazoshiriki mashindano ya Afrika zipewe msaada mkubwa katika ushiriki wao ikiwa ni pamoja na kupata wawekezaji na pia kulipiwa sehemu ya gharama za ushiriki mfano usafiri. Iinakuwa jambo linalotia unyonge kuona timu za Zanzibar zinafikia makubaliano ya kucheza michezo yao ya nyumbani na ugenini katika viwanja vya ugenini…