NIONAVYO: Miaka minne kazini, Motsepe amethibitisha ameweza

Muktasari:
- Haishangazi wengi kutokuamini, kwani hata nyumbani kwao Afrika Kusini hakuwa ameonyesha nia anaweza kuchukua kazi ya kushughulika na siasa na maendeleo ya soka kuwa kazi yake kuu.
ALIPOTANGAZA nia yake ya kuwania kiti cha urais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wengi walimwona kama mtu aliyekuwa anapima kina cha maji tu. Ukiondoa umiliki wake wa klabu ya Mamelodi Sundown, Dr Patrice Motsepe hakuwa mtu aliyetarajiwa kuingia kwenye siasa za moja kwa moja za soka.
Haishangazi wengi kutokuamini, kwani hata nyumbani kwao Afrika Kusini hakuwa ameonyesha nia anaweza kuchukua kazi ya kushughulika na siasa na maendeleo ya soka kuwa kazi yake kuu.
Yawezekana maono yake na mafanikio aliyoyapata na Mamelodi yalichangia kumshawishi kuna jambo anaweza kulifanya kwa ajili ya soka la Afrika. Sundown ambayo familia ya Motsepe ilitwaa umiliki wake tangu mwaka 2003, ilianza kutoa changamoto kwa klabu kongwe za Afrika ya Kusini za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates katika kuwania ubingwa na tuzo mbalimbali Afrika Kusini.

Mafaniko hayo hayakuishia nyumbani tu, hata katika mashindano ya Afrika, Sundowns ilianza kutoa changamoto kwa timu za Afrika ya Kaskazini kama Al Ahly, Zamalek, Wydad Cassablanca, Esperance na nyinginezo na hivyo kuifanya kuwa klabu ya kwanza katika ukanda wa kusini (Cosafa) kutishia ufalme wa klabu hizo.
Ikitumia wachezaji kutoka Afrika ya Kusini na nchi za jirani, Sundown pia ilileta wachezaji kutoka nje ya Afrika hasa Amerika ya Kusini.
Dr Motsepe alimrithi Ahmad Ahmad wa Madagascar aliyemng’oa Issa Hayatou wa Cameroon mwaka 2017.
Wakati katika miaka yake minne Ahmad Ahmad alionekana kupwaya katika viatu vya Issa Hayatou, miaka minne ya Motsepe imekuwa na vitu vya mafanikio vinavyoonekana japo bado ni mapema kumlinganisha na Hayati Issa Hayatou aliyekalia kiti cha rais wa CAF kwa miaka 29.

Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 yaliyofanyika Ivory Coast yaliweka rekodi kama mashindano ya CAF yaliyotazamwa katika nchi zaidi ya 100 na mashabiki zaidi ya bilioni 1.5 kote duniani.
Hii inaonyesha namna gani soka la Afrika lilivyokuza chapa yake na hivyo kuvutia wawekezaji. Haishangazi malipo ya fedha na bonasi za mashindano mbalimbali yameongezeka maradufu.
Maombi ya mataifa mbalimbali kuandaa mashindano ya CAF kwa sasa ni mengi kwani wenyeji wa mashindano wanapata motisha kutokana na kupanda kwa umaarufu wa mashindano hayo na fedha zinazotoka CAF. Ni mara chache sana kusikia shindano fulani la CAF limeshindikana kufanyika kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

Kwa mara ya kwanza, Afrika iliingiza timu kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia Qatar 2022 ambayo ni Morocco. Haya ni mafanikio makubwa na chanzo cha matumaini Afrika haikuwa mbali kucheza fainali za Kombe la Dunia kama ambavyo zimekuwa zikifanya timu za Ulaya na Amerika.
Miundombinu ya kuchezea soka pia imeimarika katika mataifa mbalimbali. CAF kwa kushirikiana na FIFA zimekuwa zikitoa msukumo kwa viwanja kuwa katika viwango vinavyokubalika kwa kuchezea na kurushwa katika runinga.
Uzoefu wa Dr Motsepe kama mfanyabiashara na mmiliki wa klabu utakuwa umechangia pakubwa katika kufikia mafanikio haya. Hata katika uwanda wa siasa za soka, kipindi cha miaka minne ya Motsepe hakikuwa na migogoro mingi ya kutishia mashindano kuchezwa.

Katika Mkutano Mkuu maalum wa CAF uliofanyika Cairo, Misri, Jumatano ya wiki hii, Dr Motsepe amepewa ridhaa ya kuliongoza soka la Afrika kwa miaka mingine minne.
Hata hivyo, anakabiliwa na changamoto za kuupeleka soka mbele kwa kuhakikisha kuna miradi ya kutosha ya maendeleo ya soka la vijana na wanawake, miundombinu bora, uwekezaji zaidi katika mashindano mbalimbali na nyanja za kiufundi, tiba na lishe kwa wanamichezo.
Kwa mafanikio na utengamano uliokuwa CAF katika miaka minne ya Dr Motsepe, kuna dalili zote soka la Afrika litapiga hatua kubwa. Kuna dalili imani aliyopewa ya kupita bila kupingwa haitakuwa kitu cha kujutia bali cha kujivunia siku za usoni.
Kwa waliokuwa wanafuatilia mkutano maalum wa CAF bila shaka walimwona nyota wa zamani wa soka na Rais wa Shirikisho la Soka la Cameoon, Samwel Eto’o akichaguliwa katika kamati ya utendaji ya CAF.

Hii inatokea baada ya Eto’o na Cameroon kuwa kwenye mgogoro na CAF kiasi cha nchi hiyo kulipeleka shirikisho hilo katika mahakama ya usuluhishi wa migogoro ya michezo.
Kitendo cha Eto’o kupewa kiti cha mbele wiki moja baada ya uamuzi ulioipa ushindi Cameroon dhidi ya CAF, ni kitendo kinachoonyesha utayari wa CAF na Motsepe kufanya kazi na wasiokubaliana naye huku akiheshimu michakato ya sheria. Huu ni mtazamo chanya kwa mtu aliyedhamiria kuleta utengamano katika familia ya soka.
Mwandishi wa Makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).Unaweza kutuma maoni yako kupitia namba yake hapo juu.