NIONAVYO: Katisha miaka 58 Miura yupo Uwanjani

Muktasari:
- Kwa wale wa kizazi cha sasa, maarufu kama Gen Z, ni wazi ukiwauliza kama wamewahi kuona tukio la Zidane akionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa beki wa Italia, Marco Materazzi kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2006, wengi hawatakuwa na kumbukumbu hiyo, labda kwa msaada wa teknolojia.
LEO tukiwauliza wasomaji wetu ni wangapi walimwona Zinedine Zidane akichezea timu ya taifa ya Ufaransa na kuchukua Kombe la Dunia dhidi ya Brazil mwaka 1998, tutashangaa.
Kwa wale wa kizazi cha sasa, maarufu kama Gen Z, ni wazi ukiwauliza kama wamewahi kuona tukio la Zidane akionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa beki wa Italia, Marco Materazzi kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2006, wengi hawatakuwa na kumbukumbu hiyo, labda kwa msaada wa teknolojia.
Ni muda mrefu sasa tangu Zidane, aliyezaliwa mwaka 1972, astaafu kucheza soka la kulipwa.
Kama ulikuwa unapata taabu kuvuta kumbukumbu ya Zidane, sasa utapata taabu zaidi kuvuta kumbukumbu ya mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi ya Zidane wakitofautiana kwa miaka mitano.

Kama moja ya maajabu yanayoishi, mchezaji huyo bado anacheza soka la kulipwa akiwa naumri wa miaka 58.
Ni Miura Kazuyoshi au King Miura kama anavyojulikana kwa jina la utani.
Ni mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Japan aliyecheza katika klabu ya Atletico Suzuka akiwepo kwa mkopo kutoka Yokohama FC.
Miura alizaliwa Februari 26, 1967. Kutokana na uwezo na mapenzi yake kwenye soka, alipiga safari yake ya kwanza kutafuta nafasi ya kucheza soka la kulipwa huko Brazil akiwa na umri wa miaka 15 na alichezea klabu kadhaa zikiwemo Santos na Palmeiras.
Aliporejea kwao Japan, alikuwa ni nyota mkubwa kwenye ligi mpya ya kulipwa,J-League.
Haishangazi alikuwa mchezaji wa kwanza kutangazwa kama mchezaji bora wa bara la Asia kwa mwaka 1992.

Miura alikuwa mshambuliaji bora wa Japan katika mtoano wa Kwenda Kombe la Dunia mwaka 1998 akiwa mfungaji wao bora lakini katika hali ya utata, jina lake halikuwemo miongoni mwa waliosafiri Kwenda Paris na timu ya taifa.
Safari ya soka kwa Miura ilimpeleka pia Bara la Ulaya akichezea klabu kadhaa huko Italia, Ureno na Croatia. Aliwahi pia kucheza kwa majaribio AFC Bournemouth ya England.
Unavyosoma makala hii sasa, Miura yuko kibaruani uwanjani au safarini na timu yake ya Suzuka anayoitumikia kwa mkopo.
Miura anaizidi klabu yake hiyo iliyoanzishwa mwaka 1980 kwa miaka 13 na akimzidi kocha wake Park Kang Jo kwa idadi hiyo ya miaka.
Kang ni kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Korea Kusini aliyezaliwa Japan. Pamoja na kuvunja rekodi zote hizo na kushinda karibu kila kitu, Miura haonyeshi dalili za kutundika daruga.

Rekodi za King Miura ni za kushangaza katika ulimwengu wa soka. Umri wake, unamwezesha kupambana na mabeki ambao wanastahili kuwa wajukuu wake, lakini yeye bado yupo.
Ni rekodi za kushangaza kwani kitaalam wacheza soka ya kulipwa hutegemewa kustaafu katika umri kama wa miaka 30 hivi.
Wachezaji waliozaliwa Miura akiwa anacheza soka, wengi tayari wamestaafu. Inategemewa kuwa wachezaji kadri wanavyokua na uwezo wao wa kucheza hupungua. Majeraha nayo kwa kiasi kikubwa husababisha hata baadhi ya wachezaji kustaafu kabla ya umri wao.
Katika Ligi Kuu England (EPL) wastani wa wachezaji kustaafu ni miaka 35. Hata hivyo, ni asilimia 17 tu wanaocheza hadi umri wa miaka 35. Wachezaji huwa katika kiwango chao cha juu kwenye umri kati ya miaka 25 hadi 27.
Baadhi ya sababu za wachezaji kama Miura, Roger Miller, Buffon,Ryan Giggs, Iniesta na wengine kwenda misimu mingi uwanjani zaidi ya kawaida ni pamoja na mazoezi, tiba nzuri, lishe nzuri, muda mzuri wa kupumzika, mtazamo imara kuhusu mchezo wenyewe na zaidi ya yote ni nidhamu.

Hapa kwetu ni vigumu kukutana na wachezaji waliokwenda umri huu, japo Madaraka Seleman ‘Mzee wa Kiminyio’ anatajwa kucheza akiwa na zaidi ya miaka 43 akiwa ndiye anayeshikilia rekodi.
(ingawa kulikuwa na mtazamo wachezaji wa kiafrika huzaliwa zaidi ya mara moja).
Pamoja na kukosa huduma nzuri za tiba, lishe na nyingine, tatizo la kutokuwepo kwa ligi za kulipwa za chini zinazoweza kuwavutia wachezaji wenye umri mkubwa huchangia wachezaji wetu kustaafu mapema.
Si wachezaji wengi wenye uimara kichwani (strong mentality) wa kukubali kutoka kwenye timu ya ligi kuu inayomlipa Sh5 milioni kwa mwezi na kukubali kucheza Daraja la chini linalomlipa laki 5.
Wachezaji wengi wana mtazamo wa kupanda juu, kufika kilele cha uwezo na kisha kuacha kucheza.

Kwa Miura ana miongo mitano anacheza soka yupo. Tangu miaka ya 1980 hadi 2025 yupo. Pamoja na utimamu wa mwili na afya aliyojaliwa na Mwenyezi Mungu, nidhamu na mapenzi kwa mchezo wenyewe ndivyo vimemfanya Miura yupo. Wakati wachezaji wengi waliozaliwa miaka ya 1990 wamestaafu na wa 2000 wanafikiria kustaafu King Miura bado yupo.
Mwandishi wa Makala haya ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kutuma maoni yako kupitia namba yake hapo juu.