NIONAVYO: Bundesliga ni darasa tosha

BAYERN Munich ya Ujerumani ambao ni mabingwa wa Ligi kuu ya taifa hilo imemfungashia virago kocha wake raia wa Ujerumani, Thomas Tuchell, tayari kwa kuachana naye au kusitisha uhusiano naye, kama wanavyosema wao, ifikapo majira ya joto au mwisho wa msimu.

Makubaliano haya ya kusitisha uhusiano kiungwana yametokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo katika Ligi Kuu ya Bundesliga.

Huenda msimu huu Bundesliga ikapata bingwa mpya mapema baada ya mwongo na ushee japo Bayern ina ‘uchawi’ wake kama ilivyoonyesha msimu uliopita ilipolidaka taji lililokuwa likiwaniwa na mahasimu wao, klabu ya Dortmund.

Muulize mtu yeyote mtaani, anafahamu nini kuhusu Bundesliga, atakutajia Bayern Munich ambayo imekuwa ikitwaa ubingwa karibu kila msimu. Bundesliga haina mabadiliko makubwa msimu kwa msimu kama ilivyo kwenye ligi zingine mfano ni England na Hispania. Pamoja na kuwa na baadhi ya klabu znazoitwa kubwa katika EPL na La Liga bado kunakuwa na mabadiliko mengi uwanjani na hata kwenye akaunti benki karibu kila msimu.

Bundesliga, haina nafasi ya mabadiliko makubwa kwa sababu karibu kila kitu kimegongelewa kwenye mawe, hii ni pamoja na umiliki na udhamini wa klabu na ligi yenyewe.

Wakati pesa kutoka Marekani na Ghuba yamekuwa yakimiminika kama mvua katika ligi nyingi za Ulaya, Ligi Kuu ya Ujerumani ina kanuni zinazodhibiti sana mtaji unaoingia kwenye ligi yenyewe na hata klabu.

Ni kanuni hizi zinazochangia kwa kiasi fulani kutokuwepo na mabadiliko makubwa kisoka na hata kifedha katika Bundesliga.

Mei mwaka jana kulikuwa na kampeni kubwa iliyoongozwa na uongozi wa Ligi Kuu ya Ujerumani (DFL) kutaka mabadiliko ili kuruhusu uwekezaji wa mabilioni ya Euro katika Bundesliga ikiwa ni pamoja na kuunda chombo cha kunadi haki za televisheni yaani DFL Media.

Upande wa pili kulikuwa na kampeni kubwa ya kuzuia jambo hilo ikiendeshwa na baadhi ya klabu, wanachama na mashabiki wa soka. Wakati upande wa kwanza ukiliona jambo hilo kama mwanya wa kuiwezesha Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza kuwa katika mstari mmoja wa kiushindani na ligi nyingine za Ulaya upande wa pili uliogopa wawekezaji kuingia na kulazimisha ligi au klabu kuendeshwa wanavyotaka wao, kinyume na utaratibu ambao Wajerumani wameuzoea.

Wanaogopa mabadiliko. Matokeo yake waliopinga wazo wakaibuka kidedea kwa kushindikana kupatikana theluthi mbili ya kura za klabu hivyo 36 katika Mkutano Mkuu maalum wa Ligi Kuu (DFL).

Hatimaye, Desemba mwaka jana ikiwa ni miezi sita baada ya jaribio la kwanza kushindikana, mkutano mkuu wa klabu ukafanikiwa kupata theluthi mbili, japo kwa wembamba wa kura na kufungua milango kwa wawekezaji.

Pamoja na jambo hilo kupitishwa, bado kuna upinzani mkubwa miongoni mwa mashabiki wakiona kama uwekezaji wa Euro 1 Bilioni katika chombo cha Televisheni cha Ligi Kuu, DFL Media, unaokwenda kufanywa na kampuni za kigeni zilizoomba tenda hiyo utawafanya mashabiki wa soka wa Ujerumani kuwa watumwa wa utamaduni wa kigeni.

Mfano wanasema, msukumo wa kuonyeshwa mechi nyingi kwenye televisheni unaweza kulazimisha kuwepo michezo ya kuanza mapema mchana (lunch time kick off) utaratibu ambao wao hawakuuzoea. Pia wanajenga hoja, kanuni yao ya 50+1 inaweza kukiukwa. Kanuni ya 50+1 inataka mashabiki au wanachama kuwa na kura nyingi za maamuzi katika kila chombo kinachoundwa kushughulika na soka.

Upinzani huu unaendelea, kila mara mabango yanaonekana viwanjani, kiasi cha kuwatishia wawekezaji. Kampuni ya uwekezaji ya Blackstone kutoka Marekani wameeleza dhamira yao ya kujiondoa kwenye tenda hiyo, kwani mambo yanakwenda taratibu huku uungwaji mkono na mashabiki ukiwa unatia  Jambo zuri kwa Bundesliga na mfumo wa klabu wa Ujerumani kwa jumla, ni vitu vingi vinatabirika kwa kanuni na hata upinzani unaoonekana si wa kuanzisha kanuni mpya bali wa mashabiki kuhakikisha misingi ya kanuni zilizopo inalindwa.

Ni kanuni hizo zinazoifanya Bayern iwe na msuli dhidi ya wengine kwa sababu nguvu yake inaanzia kwa mashabiki wake na misingi waliyoiweka wanachama kwa miaka mingi.

Hilo haliwezi kubadilika ghafla kama ujio wa matajiri wa kiarabu pale Man City ulivyobadilisha utawala wa jiji la Manchester na soka la England kwa jumla. Kwa mashabiki wa Ujerumani fedha ni muhimu lakini si zaidi ya soka wao.

Changamoto za Bundesliga zinatokana na kanuni za Bundesliga pia. Kanuni ya 50+1 inayowapa wanachama kuwa na maamuzi katika kila uwekezaji na utawala wa klabu inaweza kuwa na kikwazo kwa wawekeaji wanaotaka kuona fedha yao ikiongezeka thamani baada ya kuwekezwa kwenye ligi hiyo inayosifika kwenye viwango vya ufundi. Matokeo yake ni, klabu za Ujerumani zinapata wakati mgumu kushindana na timu kama Arsenal, Manchester United, Manchester City, Liverpool na hata Newcastle United ambayo imeingia kwenye ligi ya fedha England. Fedha zinazoingia Ujerumani lazima itakumbana na urasimu wa kikanuni na mazoea ya kiutamaduni. Kwa ufupi Bundesliga haijawa tayari kwa uwekezaji wa kigeni.

Hapa Tanzania, kama ilivyo katika mambo mengi hutangulia halafu sheria na kanuni huja baadaye. Watu watatafuta ardhi popote wakae na kujenga kisha serikali itakuja kurasimisha au hata kuwaondoa.

Utaratibu wa soka la nchini hauko tofauti na utamaduni mwingine mpana. Sheria ya uwekezaji katika soka hasa katika klabu ya umma haina miaka 10 tangu imekuwepo.  Kwa mujibu wa sheria hiyo, klabu zinaweza kumilikiwa kwa asilimia mpaka 49 na mitaji binafsi huku asilimia 51 na wanachama wa klabu hizo.

Sheria yetu ilitungwa kuweza kutoa nafasi kwa wafadhili tuliowazoea, hasa katika klabu za Yanga na Simba, sasa kuitwa wawekezaji. Ukiangalia kwa miwani mikubwa, ni utaratibu haujaeleweka au wanachama hawajajengewa uwezo wa kujua wajibu na haki zao. Ukiangalia orodha ya klabu za Ligi Kuu, ni klabu tatu za Yanga, Simba na Coastal Union zinazopenya sifa ya kuitwa klabu za wanachama.

Lakini ukiangalia wanachama waliopo na namna mambo yanavyokwenda utagundua klabu zina wanachama wanaokaa pembeni kushangilia timu inaposhinda na kupiga kelele timu inapofanya vibaya. Sidhani kama kuna wanachama wengi wanaofuatilia masuala ya uendeshaji wa klabu yakiwemo masuala ya fedha na ufadhili.

Wawekezaji ndio wameachiwa mzigo wa kutafuta wawekezaji,kuendesha klabu na kuamua lolote ili mradi timu inashinda.

Si wanachama wengi ambao leo wakiulizwa klabu yao ina wadhamini wangapi wanaweza kuwajua. Kinachoonekana kwenye jezi za wachezaji ndicho wanachokitambua. Hawajui mikataba imeingiwa lini, inakwisha lini na ina maana gani kwa klabu yao. Wanachotaka ni ushindi si kingine. Siku timu ikipoteza mchezo utasikia tunataka timu yetu.

Ni mtihani mkubwa sana pale hatima ya klabu inapoachwa mikononi mwa mwekezaji wa sasa. Yaani mwekezaji wa sasa ndiye atafute udhamini wa klabu, pia kuwatafuta wawekezaji wengine ili asaidiane kuipeleka klabu mbele.

Menejimenti za klabu zinatakiwa kuwajibika kwa uongozi uliowekwa na wanachama ambao ndio wanamiliki asilimia 51 ya klabu. Viongozi wa klabu za umma wanatakiwa kuwajibika kwanza kwa wanachama waliowachagua kabla ya Bodi za klabu ambayo ni chombo cha pamoja cha uendeshaji wa klabu.

Wawakilishi wa klabu kwenye bodi ya uendeshaji ni muhimu wakaonekana kujua na kuwakilisha matakwa na masilahi ya wanachama.

Kama tulivyoona katika Ligi ya Ujerumani, kanuni zilizopo na uelewa wa mashabiki na wanachama wa klabu hata shirikisho ni muhimu sana kuelekeza katika kuamua mustakabali wa klabu na soka kwa jumla. Taasisi, kanuni na wanachama wao wanatakiwa kuelewa na kuzingatia kanuni na taratibu zinazowekwa kuwaongoza na sio kienyeji tu.


Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.