Ndemla: Basena alitaka niache soka nirudi shule

'HAKUNA kukata tamaa' Hakuna kufeli'. Kauli hizi zinaenda sambamba na maisha ya soka ya kiungo fundi wa mpira anayekipiga Singida Big Stars, Said Hamis Ndemla na anasema kama sio Haruna Moshi 'Boban', Mwinyi Kazimoto na Uhuru Suleiman, angegeuka kuwa mtazamaji na shabiki wa timu fulani.
Kwa nini? Anasema baada ya kupandishwa timu ya wakubwa mwaka 2013 kwenye kikosi cha Simba, alikutana na kikwazo kutoka kwa Kocha Mganda, Moses Basena, hata hivyo hakukata tamaa.
Mwanaspoti lilifanya naye mahojiano na mbali na sakata hilo, anasimulia mengine mengi kuhusu maisha yake ya soka na alivyohusishwa na Yanga na dili lilivyokuwa, ingawa ukizungumza naye ni mkimya lakini anayejibu bila papara na anasikiliza kwa umakini.
KWA NINI NI MKIMYA?
"Nina aibu iliyopitiliza hasa kwa watu nisiowazoea, ndio maana sipendi kuongea mbele ya kundi la watu wala kukaa eneo hilo, ila sasa ukinikuta napiga stori na jamaa zangu huwezi amini kama ni mimi nje na hapo utanikuta ninachezea simu mara nyingi na sina stori na mtu.
"Ndio maana kwangu inakuwa ngumu kufanya mahojiano na watu, sasa wengi wananiona kama nina kiburi, kupitia mahojiano haya wafahamu hivyo, mimi siyo muongeaji kabisa, sikumbuki ni lini nilifanya mahojiano na kwenye televisheni ndio siwezi kabisa."
Ugeni wa Mwanaspoti aliukaribisha kwa ukarimu sehemu anapokaa panapoitwa Karakana Sokoni mkoani Singida; "Naheshimu sana wewe kufunga safari kutoka Dar es Salaam hadi Singida, ndio maana najilazimisha kuzungumza ili mradi uone nimethamini hilo."
ATAKIWA ARUDI SHULE
Ndemla si mwongeaji sana na kwa kumtazama tu unapata jibu, anaanza kwa kusimulia namna Kocha Basena alivyokuwa akimkatisha tamaa na kumtaka arudi shule kutokana na umri wake ulikuwa chini ya miaka 20 na hakuwa akimpa moyo wa kucheza soka.
"Ulikuwa ni ushauri mzuri, lakini akili yangu tayari ilishazama kwenye soka. Ilinipa wakati mgumu sana kila nilipoenda mazoezini. Aliniambia wewe bado kijana mdogo rudi shule.
"Hata hivyo, sikukata tamaa na alikuwa akinifuatilia pia ninavyocheza. Hata hivyo, kuna kaka zangu, walikuwa wananipa moyo wa nini napaswa kufanya ili kocha aniamini. Haruna Moshi 'Boban', Uhuru Seleman na Mwinyi Kazimoto walinisaidia sana. Hii ilisaidia sana na kuna siku kocha aliniita na kuniambia una kipaji kikubwa, pambana. Ilikuwa siku nzuri sana kwangu," anasema Ndemla.
BABA AMWINUA KISOKA
Ndemla ambaye pia kwa mwonekano ni mpole anamkumbuka marehemu baba yake ndiye aliyechangia yeye kupenda soka.
Bado ni pigo kubwa sana kwake kumpoteza na anakiri kama kuna mambo akiyakumbuka na kumuumiza ni kifo chake kwani ndiye aliyechangia pakubwa kumwinua kisoka.
"Kifo cha baba yangu mzazi ambaye alinisapoti sana kwenye mpira ndicho kimeacha kovu la maumivu moyoni, nilitamani aonje matunda yangu, afurahie akiniona nacheza. Alinipeleka shule ya soka ya Makongo ili kuhakikisha ndoto yangu inatimia, kiukweli sipendi kusimulia hilo," anasema.
MAMA ANAMTIA MOYO
Anamtaja mama yake mzazi anayeitwa Blandina, namna anavyojitahidi kumtia moyo licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara, ndiye anayemsisitiza pia asikate tamaa na kama riziki ipo anaamini itafika.
"Mama kila wakati ananitia moyo. Mke wangu pia na rafiki yangu Wayne Abbas, kama nina jambo linaniumiza huwa ni rahisi kuwaambia. Mimi si mwongeaji sana na kukueleza jambo langui nie nimekuzoea na kukuamini," anasema kiuyngo huyo ambaye alionyesha huzuni hasa akisimulia kifo cha baba yake.
HAKUNA KUKATA TAMAA
Japokuwa hapendi kuweka wazi vitu vyake binafsi, anasema hawezi kukufuru vitu alivyovipata kwa sehemu kupitia soka, ila analidai na anaamini litakuja kumlipa akiendelea kupambana bila kukata tamaa.
"Kuna wakati mchezaji anaweza kukaa benchi siyo kwamba hana uwezo ama kiwango chake kimeisha, kuna wakati upepo wake unakuwa mzuri na wakati mwingine mbaya, ndio maana nasema ukifika wakati wangu wa kucheza nitafanya makubwa."
KIKOSI B
"Japokuwa walitangulia kupandishwa kina Jonas Mkude, Christopher Edward na wengine, mimi nikafuatia mwaka uliofuata, Simba wakati ule ilitengeneza timu ya vijana nzuri sana, ambayo wengi walitamani tufike mbali.
"Ingawa kwa asilimia kubwa kikosi hicho, kilitawanyika kwangu mimi bado naamini tuna uwezo mkubwa wa kufanya mengi kwenye soka, kikubwa ni kutokukata tamaa."
MAWAKALA WANAZINGUA
Anasema kinachowakwamisha wachezaji wazawa kutoka nje ni kukosa mawakala wa kutengeneza dili zao, hivyo wanajikuta wakikwama kutimiza ndoto zao.
"Nimewahi kwenda kufanya majaribio Sweden klabu ya AFC Eskilstuna ya mjini Eskilstuna, nilifaulu lakini yapo mambo yaliyofanya nisicheze timu hiyo, makocha waliokuwa wananiangalia mazoezini na wachezaji walisema nina kipaji kikubwa," anasema na kuishia hapo na kushindwa kueleza yote aliyopitia huko; "Si kila kitu mchezaji anaweza akazungumza."
Hata hivyo, huku akiongea kwa upole kuhusu wazawa kusemwa mitandaoni anasema; "Kuna wakati naona mengi kwenye mitandao ya kijamii kuona wazawa hatupambani, ila sio kila kitu kinachoandikwa unatakiwa kukijibu, mengine unayaacha yaende tu, binafsi nikipata wakala mzuri nipo tayari kwenda nje."
MAKOCHA WAMBEBA
Anawataja Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu ndiye aliyeona kipaji chake wakati akiichezea timu ya mtaani ya Mesina na ilikuwa mechi ya kirafiki dhidi ya Simba B na hapo ndio ukawa mwanzo wake wa kutua Simba.
"Aliyekiona kipaji changu kwa mara ya kwanza ni Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, tulicheza mechi ya kirafiki nikiwa na timu yangu ya mtaani ya Mesina dhidi ya Simba B Uwanja wa Kinesi, baada ya mechi akaniita akasema nipe namba yako nitakupigia ili uchezee Simba B, ilikuwa mwaka 2012, kisha akafanya hivyo nikasaini."
Anawataja pia makocha Jamuhuri Kiwelu, Abdala Kibadeni na Seleman Matola ndio waliomtambulisha kwenye ramani ya soka na hasa Ligi Kuu na sasa anajulikana na Watanzania.
Anakiri walimjenga kutokukata tamaa na kukabiliana na kila aina ya changamoto za soka, kuhakikisha kipaji changu hakiendi na maji.
Kwa upande wa makocha wa kigeni, Goran Kopunovic na Dylan Kerry anasema wanafuatilia kipaji chake hadi sasa.
"Ni makocha ninaowasiliana nao hadi sasa, muda mwingi wananitia moyo, hivyo napata nguvu nikiamini nikipata wakati wa kucheza kwa zamu yangu nitafanya kitu kikubwa."
KUONDOKA SIMBA FRESHI TU
"Simba imenilea hadi kufahamika na watu wengi, nimetembea nchi mbalimbali, zipo hatua za kimaendeleo ingawa siwezi kuzitaja nilizozifanya nikiwa na timu hiyo, imenipa ujasiri wa kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Pia anazungumza nyakati zake alipoacha na Simba; "Nilijua kuna siku nitaondoka, hakuna mchezaji anaweza akaishi milele kwenye timu moja, maisha yetu ni ya kuzunguka kesho hapa, keshokutwa kwingine, kuna wakati ninaweza nikarejea tena."
ATUA MTIBWA
Anasema baada ya kutua Mtibwa Sugar, aliishi vizuri na kuamini hakuna jambo linaloshindikana kwenye soka, akitofautisha na mashabiki ambao tafsiri zao mchezaji anapotoka klabu kubwa wanaona ndio mwisho wake. Anaamini kipaji ndio kinakupa heshima na kutakiwa na timu nyingine na ndio maana sasa yupo Singida Big Stars na maisha yanaenda na maisha ya aliko sasa hayana tofauti na kwengine kwani kila kitu wanakipata cha mahitaji yao ya msingi;
"Kuna mastaa wengi kila mmoja na maisha yake, ila tunapokutana kambini na mazoezini tunapiga stori za kazi.
"Uwepo wa mastaa wenye viwango kwangu inanisaidia muda mwingi kujiweka tayari ili nikiambiwa nicheze niwe tayari kuyafanya majukumu kwa ukamilifu."
KUHUSISHWA NA YANGA
Ndemla wakati yupo Simba alihusishwa na Yanga mara kadhaa, kwa upande wake anasema hakuwahi kukaa meza moja na viongozi wa timu hiyo wala kumpigia simu ya kuhitaji huduma yake.
"Nilikuwa naona taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii, wengine wakiniambia nimelemaa Simba sioni fursa za pesa kwa Yanga, ila ukweli ni huu, na sijawahi kuzungumza Yanga hata wao wanalijua hilo," anasema.
Anasema uvumi huo ulianza baada ya kucheza dabi ya kwanza, ambayo Yanga ilitangulia kuongoza mabao matatu kipindi cha kwanza na Simba ikarejesha yote kipindi cha pili.
"Nakumbuka tuliingia kipindi cha pili na mwanangu Willium Lucian 'Gallas' tulikichafua pale kati, hapo nikaanza kusikia mara naenda Yanga ila haikuwa hivyo, hiyo mechi ilinitambulisha kwa jamii," anasema.
CHUJI, MWINYI NI MOTO
Anasema alikuwa anapenda aina ya uchezaji wa Athuman Idd 'Chuji' na Kazimoto, ambao aliwaambia kabisa jinsi walivyomchochea apende zaidi soka.
"Ni kaka zangu ambao nisipocheza wananiuliza nina shida gani, nikicheza nikifanya vizuri wananipongeza, nikifanya vibaya wananiambia nirekebishe.
"Walikuwepo wengi waliokuwa wanafanya vizuri wakati huo, ila hao jamaa muda mwingi wakiwa uwanjani walikuwa na vitu vipya, vilivyokuwa vinavutia kuwatazama, pia walinifanya nisipende sana mitandao ya kijamii nisimamie zaidi na kazi zangu."
Nje na hilo, anasema kwa namna walivyoishi maisha yao, yalimfunza kuchukulia umaarufu tofauti na kazi siyo kitu anachokipa umuhimu.
"Ingawa unanisaidia kurahisisha kupata huduma mbalimbali mfano nikienda hospitali napata huduma kwa wakati."
AJIBU MTU POA SANA
Ndemla ni swahiba na Ibrahim Ajibu aliyecheza naye Simba na sasa wamekutana SBS, anashangazwa na namna jamii inamchukulia kama nunda, wakati ni mtu poa na mwenye huruma dhidi ya wengine.
"Ajibu ni mcheshi, ana utu ila walivyoamua kumchukulia anaamua kuwapa picha wanayoitaka, ukibahatika kukutana naye mkapiga stori utamjua kwa upande wa pili.
"Siyo mtu wa kujali kuzungumzwa vibaya, huwa anaamini kama hayupo hivyo hasumbuki na wale wanaompachika tabia za kila aina, mtu anayefikiri maisha ya baadaye, kama akiamua siku aamue kuyaonyesha maisha yake upande mwingine atabadilisha upepo," anasema.
Anaulizwa na vipi inavyosemekana ni mvivu wa mazoezi, anajibu; "Siyo mvivu soka ni kazi yake, kila mchezaji akiamua kufunguka yake nadhani mtajua upande wake wa pili, ndio maana si kila jambo la kulijibu."