Nassor Idrissa: Waamuzi nchini bado safari ndefu

SAFARI ya Azam FC kwenye Ligi Kuu Bara imekuwa ya milima na mabonde kutokana na timu hiyo kupitia nyakati tofauti zinazoacha historia kubwa katika soka.

Kuna kipindi ambacho Azam FC imekuwa ikikutana na nyakati ngumu lakini wakati mwingine imekuwa ikipitia nyakati za raha ambazo kila klabu ya soka inapenda kupita.

Nassor Idrissa ‘Father’ anaweza kuwa miongoni mwa watu wachache ambao wamekuwa sehemu ya Azam FC tangu ilipokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) sasa Championship hadi leo hii na ni moja kati ya timu tatu kubwa za soka hapa nchini.

Kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Azam FC pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Katika mahojiano yake maalum na Mwanaspoti yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Father anakiri kwamba kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, maisha ya soka la Tanzania yanapiga hatua kubwa na yanabadilika sio tu kwa Azam FC pekee bali nchi nzima kiujumla.

Dalili kubwa ambayo Father anaitaja kama kiashirio cha maendeleo ya soka la Tanzania ni kupanda kwa thamani na hadhi ya ligi hiyo.


LIGI INA HADHI

Kigogo huyo anasema ligi ya kipindi hiki imekuwa ya tofauti ukilinganisha na ile ya nyuma kimaendeleo, ushindani na maboresho mbalimbali.

“Ligi sasa ipo juu imebadilika na imepata maendeleo makubwa. Ukiangalia jezi kila timu kwa kila msimu kuna jezi husika tofauti na zamani timu zilikuwa hazina jezi maalum.

“Ukiangalia viwanja tunavyo, vimeboreshwa lakini ule wa zamani waliochezea kama kina Mohamed Mbwana ungekuwa sasa ungefungiwa hata miaka 10 lakini ligi imekua na inavutia ndio maana hata wachezaji kutoka mataifa mbalimbali wanavutiwa kuja kucheza,” anasema.


WAAMUZI BADO

Pamoja na kuimarika kwa ligi na soka kwa ujumla nchini, lakini Father anakiri kwamba eneo la waamuzi bado halijaonyesha ufanisi mkubwa na linahitajika kuimarishwa ili liendane na kasi ya mafanikio ya soka.

Anasema hakuna sababu ya waamuzi kutoka nchi jirani za Burundi na Zambia kuchezesha mechi kubwa za mashindano Afrika na dunia kiujumla huku wa hapa nchini wakishindwa kufanya hivyo.

“Eneo la waamuzi linahitaji kufanyiwa maboresho makubwa. Niseme tu eneo la waamuzi bado sana. Hadhi ya maendeleo tuliyonayo kwenye ligi na mpira wetu haviendani na viwango vya waamuzi wetu, japo ni eneo gumu inabidi lifanyiwe mabadiliko makubwa ndio maana nchi za wenzetu wanahangaika na teknolojia (VAR) na kadhalika,” anasema Father na kuongeza:

“Kama tunaweza kutoa wachezaji kwenda hata Ulaya kwa nini waamuzi wetu hawaendi? Hili eneo tumefeli. Wanachotakiwa waamuzi wetu kufanya ni kutafsiri sheria kama zinavyosema. Kama wana mapenzi na timu yoyote waache ili kuboresha viwango vya waamuzi katika ligi yetu.”


WAPANIA UBINGWA, MAKUNDI CAF

Anafunguka na kusema mwaka huu wamepania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ambao hawajautwaa muda mrefu tangu walipobeba ndoo hiyo mara moja tu mwaka 2014.

“Azam hatukuwahi kuwa na lengo lingine lolote katika ligi hii zaidi ya kuwa mabingwa. Ni kazi ambayo tunaipigania kwa miaka yote hiyo na ndio maana msimu huu tumewekeza sana kwenye kikosi kwa sababu hatuwezi kupata matokeo mazuri kama hatujawekeza katika eneo hili.”

Kuhusu ushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, anasema: “Kocha wetu mpya (Mfaransa Denis Lavagne) pia anatupa matumaini makubwa sana kwa kuwa ana uzoefu mkubwa kacheza fainali kubwa ya mashindano haya ya Afrika, anajua joto la kukaa kwenye kile kiti akitafuta ushindi na haya ndio matumaini yetu.

“Kwa hiyo tuna nia ya dhati sana, lengo tufike hatua ya makundi ile mizunguko minne na tumeshazungumza na kocha analifanyia kazi na tuna imani naye.”


KIPAUMBELE NI VIJANA

Anasema eneo la vijana ndilo wanalipa kipaumbele na hawalifanyii mchezo kabisa kwa kuwa ndio zao la timu yao.

“Eneo la vijana ni eneo tulilolikazia sana kwa sababu ni eneo ambalo ni rahisi kupata vipaji vya hali ya juu. Lakini sio kazi rahisi kuskauti hao vijana wenye vipaji. Mfano kile kipindi cha nyuma kulikuwa na mashindano kama Copa Coca Cola ambayo yalitusaidia kuwapata vijana waliochujwa kutoka ngazi ya kata hadi taifa hivyo tuliwapata waliobora zaidi,” anasema Father.

“Kipindi hicho tulipata vijana wenye vipaji vikubwa na hata timu ya U-23 ya timu ya taifa tuna vijana kama saba, lakini tuna vijana ambao ni hazina kwa taifa na wametokea kwetu kama Tepsi Evance, Zuberi Foba, Pascal Msindo hao ni wapya achilia mbali wale wa zamani kina Lusajo, Kachwele, Yahya Zaiyd, Shabani Chilunda, Jaku, Metacha Mnata, Ramadhan Kabwili na wengine ambao sijawataja ni mazao yetu.”


HAWAWABANII MASTAA

Anasema mchezaji waliyemlea na kumkuza kimpira hawamzuii kuondoka na akihitaji kurudi wanampokea

“Asili ya mpira ipo hivi, mtu atakaa na pale anapohitaji kupata changamoto mpya unampa nafasi ya kwenda kupata mbele ya safari kwa ajili ya maendeleo yake na hata ya klabu, kwa mfano Novatus (Dismas) kwa sasa yupo Ubelgiji anasaidia taifa na sisi tunafaidika yeye kuwepo pale,” anasema Father na kuongeza:

“Ndio maana hata siku moja hamjawahi kusikia tunawasema vibaya wachezaji tuliowalea kwa sababu maendeleo tuliyonayo yametokana na wao hata Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ni moja ya vijana waliomwaga jasho lao hapa Azam.

“Pia hatuna historia ya mchezaji kuondoka na kusema anatudai au tumemnyang’anya kitu au sisi kusema tunamdai yote ni kwa sababu tunatambua thamani yao na umuhimu wao kwetu.”


MASTAA 12 WA KIGENI SAFI TU

Anasema kitendo cha kuruhusu wachezaji wa kigeni kwa idadi hiyo ina manufaa makubwa sana.

“Kitendo cha kuruhusu wachezaji 12 wa kigeni ni safi sana, ina manufaa makubwa maana mpira una ushindani wa wazi, mpira ni biashara kubwa sana sasa wachezaji wetu wana nafasi ndogo ya kutoka nje kupata uzoeefu hivyo wa nje kuja hapa ndio inatupa uzoefu wa kupambana nao,” anasema na kusisitiza wageni hawawanyimi nafasi wazawa ambao ni zaidi ya 500 kwenye Ligi Kuu.


KOCHA ANATAKA MIKANDA

Father hakutaka kuishia kati anasema kocha wao mpya hahitaji kumtuma mtu kwenda kuangalia wapinzani wake wa kimataifa anachohitaji ni mikanda ya video ya wapinzani.

“Kocha kasema hana haja ya kwenda anachohitaji ni mikanda ya hizo mechi zao na tumejipanga vyema kupata hiyo mikanda yao japo sio kazi nyepesi.”