Namungo vs Simba, Ilibaki kidogo tu mtu aumie!

MASHABIKI wa soka wa mkoani Lindi walipata burudani ya aina yake wakati wa Sikukuu ya Eid El Fitri kutokana na soka tamu lililopigwa kwenye Uwanja wa Ilulu, wakati wenyeji Namungo walipoialika Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Timu hizo zilishindwa kutambiana kwa kutoka sare ya mabao 2-2, huku mashabiki wa Simba wakipumua baada ya timu yao kunusurika kipigo mbele ya wenyeji wao walioitangulia mara mbili kufunga bao kabla ya wekundu hao kuchomoa.
Wekundu wa Msimbazi walilazimika kufanya ‘comeback’ mbele ya Namungo iliyofunga bao la tatu kupitia Obrey Chirwa, lakini mwamuzi Omary Mdoe kutoka Tanga na wasaidizi wake walitafsiri kwamba mfungaji alicheza madhambi kabla ya kufunga.
Katika mchezo huu, licha ya sare, Simba kwa muda mrefu ilipeleka mashambulizi langoni kwa Namungo ila umaliziaji ulikuwa changamoto, ingawa kocha Pablo Franco alifanya mabadiliko kadhaa katika kikosi kilichocheza na Yanga wiki iliyopita.
Mwanaspoti kama kawaida yake linakuletea tathmini ya mchezo ulivyokuwa kwa dakika 90.
SIMBA ILIPOTEA HAPA
Katika kipindi cha kwanza Simba ilianza kwa kufanya mashambulizi mara kwa mara langoni kwa Namungo.
Uwepo wa Meddie Kagere pekee kwenye eneo la ushambuliaji ulionyesha kuwapa nafasi kubwa mabeki wa Namungo, Frank Magingi na Hamis Halifa kumkaba kwa urahisi.
Mipango ya kocha Pablo ilionekana kukwama kwani mpaka dakika tano za kipindi cha kwanza zinamalizika walikuwa hawajapata bao la kuongoza.
Simba iliingia ikionyesha inataka bao la mapema, lakini mipango yao ilikuwa inaishia kwenye miguu ya Magingi - kitasa cha Namungo kilichokuwa kinacheza kwa kutumia nguvu nyingi.
Namungo ilikuwa inafanya mashambulizi ya kushtukiza na hilo lilijibu mapema tu dakika ya saba baada ya kupata bao la kuongoza.
Bao hilo lilipatikana baada ya Haruna Shamte kupiga faulo na kupanguliwa na kipa wa Simba, Aishi Manula kisha Shiza Kichuya alipiga kona iliyounganishwa wavuni kwa kichwa na Jacob Massawe.
NAMUNGO ILIBETI VIZURI
Katika hali ya kushangaza Namungo nao ni kama Simba tu kwenye eneo la ushambuliaji kwani ilimuanzisha David Molinga.
Molinga alipoanzishwa alikuwa na ubora wa kukaa na mipira na kuwafanya mabeki wa Simba, Joash Onyango na Henock Inonga kutembea naye muda wote.
Upande mwigine benchi la ufundi la Namungo lilimuweka pembeni mshambuliaji wao matata, Reliants Lusajo hali ambayo mwanzoni ilionekana kama vile lilikosea.
Hata hivyo, kadri dakika zilivyokuwa zinakwenda Lusajo alionekana kumuweka bize beki wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomari Kapombe aliokuwa anakutana nao kwa vipindi tofauti.
CHIRWA ATIBUA REKODI SIMBA
Mabadiliko ya kutolewa Molinga na kuingia Obrey Chirwa yalionekana kuwa na tija kwani dakika ya 54 aliifungia bao la pili timu ya Namungo.
Chirwa alifunga bao hilo kwa kichwa akiwa katikati ya mabeki wa Simba, Onyango na Tshabalala na mpira kwenda moja kwa moja wavuni.
Bao hilo lilitokana na krosi ya Lusajo ambaye alikuwa anacheza kama winga na alionyesha ubora baada ya kuchonga krosi iliyozaa bao.
Mabao hayo mawili yaliifanya Simba kuvunjiwa rekodi yake baada ya kuruhusu kufungwa mara mbili katika mchezo mmoja.
KICHUYA BADO YUMO
Winga Kichuya kadri siku zinavyozidi kwenda anazidi kuonyesha ubora na kwenye mechi mbili za Simba na Yanga amehusika katika mabao yaliyofungwa na Namungo.
Kichuya katika mchezo wao na Simba ndiye aliyetoa pasi ya bao la kwanza baada ya kupiga kona iliyozaa bao baada ya Massawe kuunganisha kwa kichwa.
Kwenye mchezo huo pia alikuwa na ubora wa kukimbia na mipira na kumpa wakati mgumu Tshabalala ambaye alikuwa hapandi mara kwa mara kupeleka mashambulizi mbele kama ilivyo katika michezo mingi anayocheza.
Kichuya alipotolewa katika dakika ya 77 na kuingia Ibrahim Mkoko mabadiliko hayo yalionyesha kuwepo kwa kitu kilichopungua upande wa Namungo.
SIMBA ILIPWAYA KIMTINDO
Kukosekana kwa Benard Morrison na Chris Mugalu kulionyesha kuwepo kwa upungufu kwenye kikosi cha Simba.
Wawili hao walikuwa kwenye mechi zilizopita mpaka za mashindano ya kimataifa, lakini kwenye mchezo wao na Namungo hawakuwepo kutokana na sababu mbalimbali.
Kocha Pablo alilazimika kumtumia Kagere kwenye eneo la ushambuliaji na baadaye alimuingiza John Bocco aliyetoka kwenye majeraha, lakini hakuwa na msaada wowote.
BATO YA VIUNGO USIPIME
Kwenye eneo la kiungo ambalo ndilo mhimili mkubwa wa timu inapocheza kulikuwa na bato la aina yake, huku upande wa Namungo wakicheza Massawe, Khamis Khalifa ‘Nyenye’ na Abdulaziz Makame ‘Bui’ na upande wa Simba walicheza Jonas Mkude, Mzamiru na Rally Bwalya.
Mkude upande wa Simba na Masawe upande wa Namungo walikuwa wanacheza kiungo cha chini wakisaidia kukaba hali iliyowafanya wasionekane mara nyingi kwenye upande wa kupiga pasi za mwisho.
Makame na Mzamiru walikuwa wanaenda sambamba kuhakikisha kila mmoja anaifanya kazi yake vizuri huku akihakikisha timu haipotezi.
Katika dakika ya 61 Mzamiru alitoka na kuingia Ousmane Sakho kuweka wepesi wa kutengeneza mashambulizi, lakini aligonga mwamba.
Matokeo ya juzi yaliifanya Namungo kufikisha pointi 30 baada ya mechi 22 ikibaki katika nafasi ya tatu, huku Simba ikifikisha 42 kutokana na michezo 21, ikipunguza pengo la pointi kutoka 13 hadi 12 wakati ligi ikiwa inaelekea ukingoni.