Mziki wa Afcon 2021, Cheki walichofanya mastaa EPL

YAOUNDE, CAMEROON. FAINALI za Afcon 2021 zinazidi kunoga huko Cameroon baada ya mechi kupigwa kwenye kila kundi huku mashabiki wakishuhudia uhaba mkubwa wa mabao.

Mechi za kwanza kwenye michuano hiyo Cameroon walikipiga na Burkina Faso, huku mashabiki walishuhudia vipute vya kibabe kabisa Morocco dhidi ya Ghana, Nigeria dhidi ya Misri ambapo Kelechi Iheanacho alimtesa Mohamed Salah, huku Tunisia ilianza na mechi ya kibabe dhidi ya Mali.

Klabu za Ligi Kuu England zinafuatilia kwa karibu fainali hizo kutokana na kuwa na mastaa wao kibao. Hiki hapa walichofanya mastaa hao wa Ligi Kuu England katika mechi za kwanza za michuano ya Afcon 2021.


Arsenal

Thomas Partey alianza kwenye mechi ya Ghana kuchapwa 1-0 na Morocco Jumatatu iliyopita, kabla ya kufanyiwa mabadiliko wakati Pierre-Emerick Aubameyang alikosa mechi ya Gabon iliposhinda 1-0 dhidi ya Comoro kutokana na kuwa na maambukizi ya Uviko -19. Jumanne, Mohamed Elneny alicheza kwa dakika zote 90, Misri ilipochapwa 1-0 na Nigeria na Nicolas Pepe alianzia benchi wakati Ivory Coast iliposhinda 1-0 dhidi ya Equatorial Guinea, Jumatano iliyopita na kuingizwa dakika ya 71.


Aston Villa

Bertrand Traore alikuwa nahodha wa Burkina Faso ilipochapwa 2-1 na Cameroon kwenye mechi ya kwanza ya michuano hiyo Jumapili iliyopita, lakini alitoa asisti ya bao la kwanza kabla ya kutolewa dakika ya 86. Jumanne, Trezeguet alianza kwenye kikosi cha Misri dhidi ya Nigeria na kucheza kwa dakika 58 katika mchezo huo wa kipigo cha bao 1-0 kwa timu yake maarufu kama Mafarao.


Brentford

Frank Onyeka alishuhudia timu yake ya Nigeria ikishinda mechi yake ya kwanza ya Kundi D dhidi ya Misri, licha ya kiungo huyo alikuwa benchi na hakutumika kwenye mechi hiyo ya Jumanne iliyopita.


Brighton

Ulrick Eneme Ella aliingia dakika 66 kuisaidia Gabon kupata ushindi wake wa kwanza kwenye Kundi C, ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Comoros, Jumatatu iliyopita. Staa mwingine wa Brighton, Yves Bissouma alikuwa benchi wakali Mali ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tunisia kwenye mechi ya Kundi F na aliingia dakika 59 katika mechi ambayo ilichezwa kwa dakika 89.


Burnley

Maxwel Cornet alianzishwa kwenye kikosi cha Ivory Coast katika mechi yao ya kwanza ya Kundi E dhidi ya Equatorial Guinea, Jumatano iliyopita na alicheza kwa dakika 71 kwenye ushindi wa bao 1-0.


Chelsea

Kipa, Edouard Mendy alikosa mechi ya kwanza ya Senegal kwenye Kundi B dhidi ya Zimbabwe, Jumatatu iliyopita kutokana na kuugua Uviko-19, huku akiwa na matumaini ya kutumika kwenye mechi zijazo.


Crystal Palace

Jumatatu, Cheikhou Kouyate alicheza dakika zote 90 wakati Senegal ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zimbabwe, wakati Jordan Ayew alicheza kwa dakika 86 kwenye kikosi cha Ghana kilipochapwa 1-0 na Morocco, mechi zote zikiwa za Kombe B. Kwingineko, Wilfried Zaha aliingia dakika 71 kuchukua nafasi ya staa wa Burnley, Maxwell Cornet wakati Ivory Coast ilipoichapa 1-0 Equatorial Guinea Jumatano iliyopita kwenye mechi ya kwanza ya Kundi E.


Everton

Alex Iwobi alianzia benchi kwenye kikosi cha Nigeria katika mechi ya kwanza ya Kundi D dhidi ya Misri, Jumanne iliyopita, lakini aliingia kwenye dakika za majeruhi kama sehemu ya ujanja ujanja wa kupoteza muda.


Leicester City

Nampalys Mendy alikosa mechi ya Senegal ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zimbabwe, Jumatatu iliyopita kutokana na kuwa na Uviko-19, lakini Daniel Amartey alicheza kwa dakika zote 90 Ghana ilipochapwa 1-0 na Morocco kwenye kwenye mechi ya kwanza ya Kundi C siku hiyo hiyo. Mastaa Wilfred Ndidi na Kelechi Iheanacho walianza kwenye kikosi cha Nigeria kiliposhinda 1-0 dhidi ya Misri, Jumanne iliyopita, ambapo Ndidi alimaliza mechi yote na Iheanacho, aliyefunga bao kwenye mechi hiyo alicheza kwa dakika 80.


Liverpool

Katika Kundi B, Sadio Mane alicheza kwa dakika zote na kufunga penalti ya dakika 97 wakati Senegal iliposhinda 1-0 dhidi ya Zimbabwe, wakati Naby Keita alikuwa nahodha wa Guinea na kucheza dakika zote 90 wakati waliposhusha kipigo cha bao 1-0 kwa Malawi, Jumatatu iliyopita. Mohamed Salah alikuwa nahodha wa Misri na alicheza mechi yote na kushindwa kuikoa timu yake kuepuka kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Nigeria, Jumanne.


Man City

Riyad Mahrez alikuwa nahodha wa Algeria kwenye mechi yao ya kwanza ya Kundi E dhidi ya Sierra Leone Jumanne iliyopita na kucheza dakika zote 90 kwenye sare ya 0-0.


Man United

Eric Bailly alianza na kucheza dakika zote wakati Ivory Coast ilipoanza michuano kwa kushinda kwenye Kundi E ilipoiababua Equatorial Guinea bao 1-0, Jumatano iliyopita. Wakati Hannibal Mejbri alianza na kucheza dakika 45 za kipindi cha kwanza wakati Tunisia ilipokumbana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mali katika Kundi F, Jumatano iliyopita.


Southampton

Moussa Djenepo alianza na kucheza dakika 81 wakati Mali ilipoichapa Tunisia 1-0 katika mechi ya kwanza ya Kundi F, Jumatano iliyopita na alionyeshwa kadi ya njano kwenye dakika ya 33 tu ya mchezo.


Watford

Ismaila Sarr hakucheza kutokana na kuwa majeruhi chama lake la Senegal liliposhinda dhidi ya Zimbabwe kwenye mechi ya kwanza ya Kundi B Jumatatu iliyopita na ameondoka kwenye kikosi hicho kwenda Hispania kupata matibabu.

Wakali wengine Adam Masina na Imran Louza waliitumikia Morocco kwenye mechi ya kwanza ya Kundi C dhidi ya Ghana. Masina alicheza kwa dakika 90 na alionyeshwa kadi ya njano, wakati Louza alicheza dakika 78.

William Troost-Ekong alikuwa nahodha wa Nigeria katika mechi yao ya kwanza ya Kundi D dhidi ya Misri na alicheza dakika zote, Super Eagles iliposhinda 1-0.


West Ham

Said Benrahma aliachwa kwenye benchi wakati Algeria ilipocheza mechi yao ya kwanza ya Kundi E dhidi ya Sierra Leone na aliingizwa dakika 83, lakini alishindwa kuisaidia timu yake kushinda baada ya kutoka sare ya 0-0.


Wolves

Romain Saiss alikuwa nahodha wa Morocco na kucheza dakika zote wakati taifa walipoichapa Ghana 1-0 Jumatatu iliyopita, wakati staa mwingine wa Wolves fainali za Afcon 2021, Willy Bolly hakutumika pale Ivory Coast ilipoichapa Equatorial Guinea 1-0 Jumatano iliyopita.