MZEE WA UPUPU: Kwanini Azam FC haianzii raundi ya awali CAF?

RAUNDI ya awali ya mashindano ya klabu barani Afrika, ilianza Ijumaa iliyopita, Septemba 9, 2022. Timu tatu za Tanzania ambazo zilicheza wikendi, zimeanzia raundi ya awali, kasoro timu moja tu, Azam FC!

Simba na Yanga zimeanzia raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa na Geita Gold imeanzia raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho.

Azam FC kuanzia raundi ya kwanza ni fumbo lililowatatiza wengi, tangu Agosti 7 mwaka huu, pale CAF ilipotoa rasmi tamko kwamba Azam FC haitoanzia raundi ya awali.

Wengi walitegemea kuona Simba ikianzia raundi ambayo Azam FC itaanzia, kutokana na mafanikio ya hivi karibuni kwenye mashindano ya Afrika, lakini imekuwa tofauti.

Wapo wanaosema Azam FC imefaidika na mafanikio ya Simba, lakini hawasemi kwa nini iwe Azam FC na siyo Simba yenyewe. Kwenye hilo, kuna wanaosema Simba isingeweza kufaidika kwa sababu inashiriki Ligi ya Mabingwa. Kama ni hivyo, kwanini iwe Azam FC na siyo Geita Gold ambayo inashiriki mashindano sawa na Azam FC?

Kwa sababu kuna baadhi ya nchi zimetoa timu mbili za kuanzia raundi ya kwanza, kama Tunisia na Algeria. Nchi ya bingwa mtetezi, Morocco, imetoa timu moja tu kuanzia raundi ya kwanza. Ufuatao ni ufafanizi wa kina juu ya sababu ambazo zinaifanya Azam FC kutoanzia raundi ya awali.

CAF ina wanachama 56, kati yao 54 ni wanachama kamili na wawili ni wanachama vivuli, ambao ni Zanzibar na Re Union.

Wanachama hawa hutakiwa kutoa timu zitakazoshiriki mashindano mawili ya klabu yanayoandaliwa na CAF, yaani Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Kwa hiyo kila shindano hutarajia washiriki 56 kutoka wanachama wale 56. Lakini pia kuna wanachama 12 ambao hupewa nafasi mbili kwenye kila shindano, ikiwemo Tanzania.

Hii ina maana kwamba kuna ongezeko la klabu 12 kwenye kila shindano, hivyo kufanya klabu 68. Kwa hiyo CAF hutarajia jumla ya klabu 68 kwenye kila shindano lake, kila msimu.

Lakini kutokana na sababu mbalimbali, haijawahi kutokea hivyo hata msimu mmoja. Msimu huu kwa mfano, kwenye Ligi ya Mabingwa kuna timu 58 zinazoshiriki, kutoka nchi 46. Na kwenye Kombe la Shirikisho kuna klabu 50 kutoka nchi 39.

Hizi timu 50 za kwenye Kombe la Shirikisho zikiingia kwenye mtoano, baada ya raundi moja zitabaki timu 25 ambazo haziwezi tena kuingia kwenye mtoano kwa sababu hazigawanyiki kwa mbili.

Kwa hiyo CAF ikishapata idadi kamili ya timu zitakazoshiriki, huangalia utaratibu utakaoepusha kubaki na idadi ya timu ambazo hazigawanyiki kwa mbili. Hufanya ukokotoaji na kuzichagua baadhi ya timu kuanzia raundi ya kwanza na zilizobaki kuanzia raundi ya awali.

Kwa msimu huu, ukokotoaji wake ukaja na majibu kwamba kati ya timu 50 za kwenye Kombe la Shirikisho, timu 14 zianzie raundi ya kwanza na 36 zilizobaki zianzie raundi ya awali.

Hizi timu 14 zilichaguliwa kutokana na viwango vyao, au ufanisi wao kwenye mashindano ya CAF kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kwa mfano, klabu namba moja kwa ufanisi ni Al Ahly ya Misri, lakini haishiriki Kombe la Shirikisho.

Katika klabu zinazoshiriki Kombe la Shirikisho, namba moja ni RS Berkane, ambayo ni namba sita kwa ujumla Afrika.

Azam FC imeanzia raundi ya kwanza kwa sababu ni miongoni mwa klabu 14 vyenye ufanisi bora kwenye mashindano ya CAF Kati ya klabu 50 zinavyoshiriki Kombe la Shirikisho msimu huu. Hii ni kutokana na matokeo yake ndani ya miaka mitano iliyopita ilipokuwa ikishiriki michuano hiyo ya Kombe la Shrikisho.

Katika kipindi hicho, Azam FC imecheza mechi nane, imeshinda tatu, sare moja na imepoteza mechi nne. Haya ni matokeo bora juu ya timu 36 zote zilizoanzia raundi ya awali. Wapo wanaoamini kwamba Azam FC ilifaidika na ufanisi wa Simba kwenye mashindano ya Afrika, la hasha.

Hakuna klabu yoyote ambayo hufaidika na klabu nyingine kwenye mchakato wa kuanzia raundi ya kwanza...hapo kila timu hujibeba yenyewe.

Sehemu pekee ambayo klabu inaweza kufaidika na mafanikio ya klabu nyingine ni kwenye kupata nafasi ya kushiriki, kwa sababu mafanikio ya timu moja huipatia nchi nafasi nne.

Lakini ukishaipata hiyo nafasi, kinachofuatia hapo ni kujibeba wewe mwenyewe. Azam FC ilijibeba wenyewe kwa matokeo yake ambayo imekuwa ikiyapata.