Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MWAKYEMBE: Bondia asiyesahau 'mauzauza' safari nzito ya ngumi

Mwakyembe Pict

Muktasari:

  • Emmanuel Mtewele ndio majina yake halisi yanayopatikana katika vyeti vya kuzaliwa, ila mashabiki wa ngumi za kulipwa nchini wanamtambua kama Emmanuel Mwakyembe ambaye ni mmoja kati ya madalali wa viazi kutoka Mbeya sokoni hapo.

JINA la Mwakyembe sio geni kwa wenyeji wa Soko la Mabibo, Dar es Salaam ambalo ni maarufu kama Mahakama ya Ndizi, lakini ni geni kama utakuwa mgeni katika soko hilo.

Emmanuel Mtewele ndio majina yake halisi yanayopatikana katika vyeti vya kuzaliwa, ila mashabiki wa ngumi za kulipwa nchini wanamtambua kama Emmanuel Mwakyembe ambaye ni mmoja kati ya madalali wa viazi kutoka Mbeya sokoni hapo.

Kwa mujibu wa mtandao wa Boxrec ambao ndio unahusika kuhifadhi takwimu za mabondia duniani unaonyesha bondia huyo alianza kucheza ngumi za kulipwa 2018 ambapo pambano lake lilimalizika kwa sare dhidi ya Mudy Pesa likichezwa kwa raundi sita pekee.

Rekodi zinaonyesha bondia huyo amepigana mapambano 15 kabla ya leo, Jumatano, kupanda ulingoni nchini Russia katika pambano la kwanza la kimataifa nje ya mipaka ya Tanzania dhidi ya Tigran Ulzayan wa Russia.

MW 03

Bondia huyo ameshinda mapambano 12 kati ya hayo matatu akishinda kwa Knockout, akipigwa moja huku akitoka sare katika mapambano mawili.

Mwakyembe kwa sasa ni bondia wa nne kati ya mabondia 115 bora wa uzani wa Light nchini wakati duniani akiwa wa 153 katika mabondia 2496 ambaye amepewa asilimia 25 za kushinda kwa Knockout huku akiwa na hadhi ya nyota mbili sasa kwa mujibu wa Boxrec.

Mwanaspoti lilipiga stori mbili tatu na bondia huyo ambaye amezungumzia mikasa mizito aliyowahi kukutana nayo ikiwemo kutelekezwa wakati anaenda mjini kutafuta maisha.

Mwakyembe anasimulia kuwa safari yake kuja Dar kutafuta ugali ilitokana na namna alivyowasiliana na jamaa yake aliyemtangulia darasa moja shule kuwa maisha Dar yanawezekana kwa kumpa ramani ya namna vijana wanavyoyaendesha kupitia Soko la Mabibo.

MW 01

Hali hiyo ikampa mzuka Mwakyembe kutaka kuja mjini kuungana na jamaa yake kutafuta riziki, lakini bahati mbaya alipofika Mlandizi, Pwani akiwa kwenye basi jamaa alimzimia simu, yaani hadi anafika katika ilipokuwa stendi ya mabasi Ubungo, mwenyeji wake alikuwa hapatikani hewani.

Kutokana na mwenyeji wake kuingia mitini na yeye akiwa mgeni jijini humo akalazimika kubaki stendi ya Ubungo kuendelea kutafuta msaada kabla ya kuunganishwa na mtu mwingine anayemtaja kwa jina Henry ambaye alikubali kumsaidia na kumfundisha kufanya biashara katika soko hilo.


SWALI: Sasa ilikuwaje ukaingia kwenye ngumi?

JIBU: "Daah! Sababu kubwa ilikuwa kukataa unyonge unajua wakati nafanya biashara pale Mabibo nilikuwa na mteja maalumu ambaye alikuwa ananipigia simu na kuagiza mahitaji yake. Nilichokuwa nafanya ni kumnunulia yeye akija analipia nampa mzigo wake.

MW 05

"Nakumbuka kuna siku alinipigia simu nimchukulie mahitaji, sasa wakati anafika kulikuwa na jamaa tupo naye kwenye shughuli za kutafuta alipoona gari akaimbilia. Nikawa namueleza kwamba huyo ni mteja wangu tushamalizana kwenye simu.

"Jamaa akachukia kwa kuona kama nimemkatalia riziki yake sasa yule mteja alivyoondoka yule jamaa akaja kunikunja akitaka nimpe buku moja (Sh1,000) kutokana na kwamba jamaa alikuwa anacheza ngumi na nilishapewa faili lake, nikatoa kwa unyonge.

"Lakini jamaa alivyoona nimechukia na sina cha kumfanya alinifuata tena na kunichania shati langu ambalo nakumbuka lilikuwa jipya kabisa. Binafsi niliumia ila sikuwa na cha kufanya maana jamaa alikuwa anajua ngumi na mimi sijui.

"Baada ya tukio hilo kuna rafiki yangu mmoja alinifuata kuniambia atanipeleka sehemu nifanye mazoezi ya ngumi ili niweze kujilinda. Akanipeleka kwenye gym ya mzee moja mstaafu wa jeshi ilikuwa Mabibo Jeshini.

"Hapo ndiyo safari yangu ya ngumi ilipoanzia kwa sababu niliweza kujifunza msingi wa ngumi na mtu aliyekuwa ananifundisha akagundua uwezo na kipaji changu katika ngumi akanikazania niendelee.

"Lakini sababu kubwa ilikuwa kwamba kuna mtu aliniletea unyonge kwenye kazi kwa kunionea ila nilivyofika huko nikashauriwa kuendelea na hadi leo hii nimefikia hapa.

MW 04

SWALI: Rekodi zinaonyesha ulianza kupigana 2018 nini kimekuchelewesha (kutoboa)?

JIBU: "Kwanza kabisa nilianza ngumi mwaka 2014 hadi 2015 nacheza ngumi za ridhaa kabla ya kuingia kwenye ngumi za kulipwa ambazo nilianza mwaka 2016, lakini kwa bahati mbaya na changamoto za viongozi wa ngumi mapambano mengi ambayo nilicheza hayakuwekwa kwenye Boxrec.

"2018 ndiyo yalianza kuingia baada ya kuwa kwa kocha Maneno maana yeye ndio alinipambania na huwa namshukuru sana maana hata hiyo sare na Mudy Pesa haikuwa sahihi kwa sababu nilimpiga isipokuwa yeye alikuwa anabebwa na mapambano aliyokuwa ananizidi.


SWALI: Ulishawahi kupigwa ngumi ukatamani kuacha kabisa?

JIBU: "Mmh hapana, sijawahi kupigwa ngumi na kutamani kabisa kuacha roho hiyo sina kabisa. Nimepigwa ila siyo hadi kufikiria kuacha ngumi, hapana kwa kweli.


SWALI: Pambano gani kwako lilikuwa gumu na hutakuja kulisahau?

JIBU: "Nadhani pambano langu na bondia kutoka Kenya anaitwa Nicolaus Mwangi kwa sababu mpinzani alikuwa bora sana kunizidi halafu alikuwa anatokea Dubai anapoishi.

"Lakini namshukuru Mungu niliweza kumpiga maana hakuamini na alichokutana nacho kutokana namna nilivyompiga, ingawa mwanzoni mwalimu wangu alihofia kwa kuwa kuna wakati mazoezini nilikuwa sitokei ila tulivyopewa muda mambo yalibadilika kwa sababu tulijiandaa vyema.

"Kiukweli pambano na Mwangi ndilo lilinipeleka mjini na kuongeza thamani yangu kwa kile nilichokionyesha, aliandaa Mo Dewji.

MW 01

SWALI: Una uhusiano wowote wa kifamilia na aliyekuwa Waziri (wa Michezo), Dk (Harrison) Mwakyembe?

JIBU: "Sina uhakika na hilo lakini hili jina nimelichukua kwa babu yangu kwa kupewa wakati nipo mdogo na kuhusu Dk Harrison Mwakyembe ni ukoo mkubwa sana na umesambaa.

"Nakumbuka kuna kipindi Dk Mwakyembe wakati ule yupo kwenye wizara michezo alinitafuta, ila bahati mbaya alipitia kwa viongozi wa ngumi hawakumpa namba yangu  ingawa kocha wangu alinihakikishia nitapigiwa simu na Dk Mwakyembe, ila haikutokea.

"Binafsi bado ndoto hiyo nipo nayo ya kuomba nikutane naye kwa sababu ameshakuwa kiongozi mkubwa na huenda tukawa na udugu kupitia familia za koo zetu Mbeya.


SWALI: Siku hizi mabondia nasikia kuna imani potofu za kishirikina, wewe ulishaenda au kufanyiwa kwenye mapambano yako?

JIBU: "Naweza kukuambia kwamba nimeshakutana na hali hiyo siyo chini ya mara moja kwa sababu kuna wakati nilikuwa na pambano na bondia mmoja naomba nisimtaje jina tulifanya maandalizi ya pambano yote vizuri.

"Nakumbuka siku ya kupima uzito baada kumaliza  nilishikwa na tumbo la kuharisha ikawa kila baada ya robo saa naenda chooni na mwanzo nilihisi ni mchafuko wa tumbo.

"Lakini ile hali iliendelea hadi siku ya pambano tunatoka kambini kwetu na mashabiki hadi Uwanja wa Ndani wa Taifa hali ya kuharisha inaendelea. Basi kuna bondia mwenzangu wa gym moja akaenda kunitafutia jivu nile maana aliniambia ni dawa.

"Kiukweli haikuweza kusaidia ilifika kipindi hadi mashabiki wangu wakahisi naogopa pambano maana ilikuwa kila muda naelekea chooni, wakati wote mke wangu ananiangalia kila nikienda chooni hadi hali ya kujiamini ilipotea kabisa.

"Lakini mke wangu kutokana na ile hali akaniomba tusali maana yeye ni mtu wa maombi, basi tukafanya sala ya maombi na Mungu akaleta rehema yake tumbo lilikata muda mchache kabla ya kupanda ulingoni.

"Sasa tulivyoitwa kwenda ulingoni mpinzani wangu alikuja kinyumenyume halafu watu wake wakaangusha hirizi chini ya ulingo, lakini nashukuru nilimpiga kwa Knockout ya raundi sita ingawa jamaa tangu nilivyompiga akawa anasumbuliwa na macho hadi sasa haoni.

"Promota alinipigia simu kuniomba kuniambia kama nimechanjia mikono niende nikamnasue, lakini ukweli sijawahi fanya hivyo na nilimwambia hata promota ingawa haikuwa nzuri kwa ndugu yangu.

"Lakini kuna bondia mwingine nilicheza naye alienda hadi Bagamoyo kwa mganga akazika na mbuzi ili anipige japo kuwa siyo sawa kuweka matokeo yake, baadaye nilikuja kuambiwa na jamaa zake kile ambacho walichokifanya sasa ukweli hayo mambo watu wanafanya ingawa naamini zaidi kwenye dua na mazoezi."