Mudy Pesa: Bondia muuza vijora afunguka alivyoona maluweluwe ulingoni

Muktasari:
- Mudy Pesa anakiri wazi yeye ni miongoni mwa mabondia ambao hawakuwahi kupita kucheza ngumi za ridhaa kutokana na historia yake ilivyo katika mchezo lakini hadi sasa ameonyesha kipaji chake kwa wadau wa mchezo huo.
UKISIKILIZA tamko la serikali lililotolewa wikiendi iliyopita na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’ kuwa asiruhusiwe kucheza ngumi za kulipwa bondia yeyoye kama hajacheza ngumi za ridhaa basi bondia Mohamed Rashid maarufu kama Mudy Pesa angehusika.
Mudy Pesa anakiri wazi yeye ni miongoni mwa mabondia ambao hawakuwahi kupita kucheza ngumi za ridhaa kutokana na historia yake ilivyo katika mchezo lakini hadi sasa ameonyesha kipaji chake kwa wadau wa mchezo huo.
Lakini kama unamkuta Kariakoo, jijini Dar es Salaam akipambana na wateja wake wa vijora, kamwe huwezi amini kama ni bondia wa ngumi za kulipwa.
Bondia huyo aliyeanza kupigana mwaka 2017, alichezea kichapo kizito katika pambano lake kwanza na Abdul Omari lakini haikumkata ndoto zake za kuendelea kubakia kucheza mchezo huo.
Mpaka sasa Mudy Pesa kijana wa mitaa ya Manzese, jijini Dar ameshapanda ulingoni katika mapambano 18, akishinda 10, kati ya hayo saba kwa Knockout na manne akipoteza na ametoka sare manne.
Bondia huyo katika rekodi yake hajawahi kupigwa kwa Knockout na kwa sasa amekuwa bondia wa tisa kati ya 51 bora Tanzania wa uzani wa super feather wakati duniani akishikilia namba 414 kati ya 1746 huku akiwa na hadhi ya nyota moja.
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Mudy Pesa ameeleza sababu za yeye kuingia katika mchezo wa ngumi za kulipwa ilhali ikiwa hajawahi kucheza ngumi za ridhaa lakini bado anaonyesha kiwango kizuri.
“Hakuna mtu ambaye alinivutia kuingia kucheza ngumi isipokuwa ni mimi mwenyewe ndiyo nimeupenda mchezo kutoka moyoni na wala hakuna mtu kwenye familia yetu alicheza ngumi isipokuwa ni mimi ambaye nacheza kwa mapenzi yangu.”

Ulianza kupigana mwaka gani?
Nimeanza mwaka 2018 na hadi sasa nimepigana mapambano 18 na sijawahi kucheza pambano lolote la ubingwa isipokuwa nilipata nafasi ya kupigana Dubai mara moja.
Safari yako ya Dubai ilikuaje?
Kwanza safari ilitokana na rekodi yangu kuwa nzuri, ndiyo maana walinitafuta kwa ajili ya kwenda kupigana, nilikwenda na kuonyesha kiwango kizuri ambacho kila mtu alikifurahia, sikuonyesha unyonge.
Unajua mwanzo nilikuwa najua safari za ndege zilikuwa za mipango lakini nilichokuja kugundua juhudi binafsi ndiyo zinasababisha mtu aweze kufika mbali tofauti na nilivyokuwa naamini mwanzoni.
Kitu kikubwa ni kufanya mazoezi maana hata gym yangu ni uswahilini na kuna baadhi ya mabondia waliondoka kwetu kwa sababu hatuwezi kwenda kupigana nje ila hata walipoenda sehem nyengine hawakufanikiwa.

Kitu gani kikubwa ulikutana nacho safari ya Dubai?
Nakumbuka wakati tunaenda tulivyofika uwanja ndege hapa Dar maana tulikuwa kama watatu, nilidharauliwa na mdada wa ukaguzi kwa kunitaa bishoo, naenda kuharibiwa sura.
Unajua hakuamini kabisa kama mimi bondia tofauti na wenzangu maana alisema sifanani na wapiganaji zaidi ya kuwa ‘brother man’ na nitaenda kuumizwa uso.
Lakini nilimwambia naenda kupambana na nirudi nitakupitia hapahapa kuniona nitakavyokuwa yaani kama nilivyoenda kwa sababu nimejiandaa vya kutosha kuweza kupigana na nilivyorudi nilimkuta tena nikamwambia narudi na wala sina kovu lolote usoni.
Kingine ni kuona mabondia wengi wakipigwa kwa Knockout isipokuwa mimi na wengine watatu tuliopigwa kwa pointi.

Umepigana mara ngapi mapambano Derby?
“Mapambano yenye upinzani mkali niliyocheza hadi sasa manne, nilicheza na Waziri Rosta wa Dartown, nilicheza na Man Chuga, upinzani ulikuwa mkali, Emmanuel Mwakyembe ambaye ndiye nilitishwa kutokana ubora wa Mwakyembe ikaisha kwa sare.
Kuna nyengine nilicheza na mtu anaitwa Omary Zinga huyu ndiye alihamishia ugomvi mtaani kabla ya pambano.
Baada ya kusaini kuna siku akanizuia njiani akitaka tupigane kwa madai nilikuwa nachonga sana lakini kwa bahati nzuri tuliamuliwa maana sikuwa na mpango wa kupigana mtaani.
Ulishawahi kupigwa ngumi ukatamani kuacha?
Nakumbuka niliwahi kupigwa ngumi ambayo siku hiyo raundi nne niliona kama elfu moja, niliona maluweluwe, nilikutana na mtu mkali halafu halikuwa pambano langu maana aliyetakiwa kupigana naye alipata majeraha ndiyo nikapewa nafasi yake.
Kiukweli hilo pambano ndiyo lilinifanya niumize sana kichwa nilivyorudi nyumbani, nilipigana bure halafu nimeumia mbaya zaidi mke wangu alikuwa hapendi kabisa nicheze michezo hii, alinisema sana.
Unajua niliwaza mengi sana, nilitamani niache kabisa mambo ya kupigana ila nilisema itafika wakati nitapiga mtu kama nilivyopigwa mimi.

Sasa hivi mke bado hapendi upigane?
Hapana kwa sababu mwanzo hakuona faida yake lakini sasa hivi anaona mambo ninayofanya kupitia ngumi hivyo yeye ndiyo amekuwa sapoti yangu ya kwanza kabisa na anaupenda mchezo.
Kifupi familia yangu kuanzia baba, mama na mke wangu wote hawana pingamizi la mimi kupigana isipokuwa wameniomba niwe makini maana ulingoni lolote baya linaweza kutokea.
Kwa nini unaitwa Mudy Pesa?
Kiukweli watu wengi wanaita hilo jina lakini hawajui kama sina pesa na sijawahi kumili pesa ila wananiita tu Mudy Pesa ingawa nikiuulizwa kwa nini naitwa hivyo ikiwa sina pesa huwa namueleza ukweli.
Hilo jina limetokana mzee wangu wakati anadai urithi wa baba yake aliyefariki dunia, baadhi ya ndugu walitaka kumdhulumu na baba yake pia hakuwa na pesa sasa kutokana na hilo akawa analia akisema anataka pesa ya baba.
Sasa ile pesa ya baba ndiyo ikazaa jina la pesa ya baba na mimi nipozaliwa ndiyo nikawa naitwa Mudy Pesa hadi nimefikia umri huu ingawa baba yangu anaitwa Rashid siyo pesa.
Ngumi zimekuwa zikihusishwa na ushirikina kwako ipoje?
Kitu cha kwanza ambacho naamini huwa ni mazoezi ingawa wengi hupenda kwenda kwa waganga kwa ajili ya kujihami.
Wewe ulishawahi kwenda kujihami?
Sijawahi kwenda kwa mganga isipokuwa ninapokuwa na mapambano mara nyingi naenda kwa mashkhe kwa ajili ya kupata visomo vya madua yasinikute mabaya kwa sababu juu ya ulingo kuna kuwa na mambo mengi mabaya.
Sijawahi kuona chochote ila tunaona wenzetu wanavyokutana na matukio mabaya, namwomba Mungu sana aniepushe maana wengine ndiyo kama hivyo wanakufa.
Nje ya ngumi unafanya shughuli gani?
Nafanya biashara, mwanzoni nilikuwa Manzese nauza mtumba ila sasa nipo Kariakoo nauza vijora ndiyo imekuwa biashara yangu kubwa.