MTU WA MPIRA: Tunawachukua kina Kamwe ila kuna tatizo

Yanga imefanya uamuzi mgumu mapema wiki hii. Uamuzi wa kuwapa kazi vijana wawili kwenye kitengo chake cha habari.

Ni Ally Kamwe na Priva Shayo. Ni vijana machachari katika soka la kisasa. Wanaufahamu vyema mchezo wa soka hasa katika kuchambua kimbinu na kiufundi.

Tuachane na huyu Priva ambaye atakuwa meneja wa mitandao ya Yanga. Huyu kazi yake haina shida sana. Inahitaji ubunifu na umakini tu.

Turudi kwa Kamwe. Huyu ameteuliwa kuwa ofisa habari wa Yanga. Ni kijana mmoja shupavu. Amekuwepo kwenye tasnia ya habari kwa miaka 10 sasa. Anaifahamu kazi yake vyema.

Kamwe anasifika kwa kusema ukweli hasa katika uchambuzi wa soka. Penye nyeupe husema nyeupe na nyeusi vivyo hivyo. Hii ndio tofauti ya Kamwe na wengine.

Hii imemjengea mvuto mkubwa katika tasnia ya michezo. Hii ndio imemfanya awe mkubwa mpaka Yanga ikaamua kumwajiri. Inavutia sana.

Lakini pamoja na wasifu mkubwa wa Kamwe, huko anakokwenda kufanya kazi kumeharibika sana. Hakumpi nafasi ya kuonyesha kile alichokuwa akifanya pale Azam TV.

Huku kwenye usemaji na uofisa habari kuliharibiwa siku nyingi na mtu mmoja wa kuitwa Haji Manara. Alitengeneza aina ya usemaji ambayo sasa inaonekana ndio njia sahihi.

Usemaji wa kusifia kupitiliza na kutosema ukweli. Huwezi kuwa msemaji ama ofisa habari sasa na ukazungumza uhalisia wa soka. Labda nyuma ya kamera. Mbele ya kamera unapaswa kusifia tu.

Mbele ya kamera unapaswa kueleza kuwa Yanga itaifunga hata Barcelona au Manchester City ikija kwa Mkapa. Unatakiwa kusifia tu hata kama moyoni mwako unafahamu siyo kweli. Hii ndio ‘standard’ aliyoweka Manara.

Hii ndio sababu majuzi tu nimemsikia Kamwe akisema Yanga ni kubwa kuliko Al Hilal ya Sudan. Nikacheka sana. Kamwe anafahamu hilo sio kweli, lakini analazimika kusema hivyo kwa sasa maana anaowasemea hawapendi kusikia ukweli.

Laiti Kamwe angekuwa Azam TV asingezungumza hivyo. Anafahamu fika Yanga imeachwa mbali na Al Hilal kwenye kila kitu. Lakini je watu wa Yanga wanataka kusikia hivyo? Hapana. Manara aliiaminisha jamii kuwa unapoisemea timu yako unapaswa kusifia tu.

Hii ndio sababu hata Ahmed Ally huwa anaishi kwa kusifia tu pale Simba. Ndicho alichokuta ofisini. Anasifia hata kama sio ukweli. Ndio ofisi aliyokuta.

Akiwa Azam TV, Ahmed angesema kweli. Lakini je kwa sasa watu wa Simba wanataka kusikia hilo? Hapana. Wameishi miaka mingi na msemaji wa kusifia kila kitu. Ukiwaambia ukweli nani atakusikiliza?

Mbali na kusifia, kingine kinachofanywa na wasemaji wa sasa ni kulalamika kuwa wameonewa. Hata ikitokea Simba na Yanga zimefungwa inabidi uwaaminishe mashabiki kuwa mmeonewa. Inashangaza sana.

Hiki ndicho alichofanya Manara kwa miaka mingi. Alichukua televisheni na kuita waandishi wa Habari kuonyesha namna ‘walivyoonewa’. Alifanya hivyo mara kwa mara. Ndio namna alivyoweka ngazi kwenye usemaji wengine wanafuata nyayo tu.

Hivyo hata hawa kina Ally Kamwe sitarajii makubwa sana kutoka kwao.

Nasubiri kuona wakisifia zaidi taasisi yao na kuacha kusema ukweli. Unadhani wanakosea? Hapana, ndio ofisi zao zinawataka hivyo kwa sasa. Hawana namna. Inabidi wacheze na kuimba na mfumo walioukuta katika klabu hizo. Kila la heri kwao!