MTU WA MPIRA: Robertinho atachagua pepo yake mwenyewe

NCHI ilipatwa na mshtuko mkubwa mwanzoni mwa wiki wakati Simba ikicheza dhidi ya Mbeya City pale kwa Mkapa. Ulikuwa ni mshtuko mkubwa.

Mashabiki waliokuwa uwanjani walipigwa na butwaa. Ndani ya dakika 33 tu, kocha mpya wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertino’ alimtoa staa wa timu, Clatous Chama kwa sababu za kiufundi na kumpa nafasi Pape Sakho.

Mshtuko ulikuwa mkubwa zaidi kwani pia alitoka John Bocco aliyekuwa ameumia na kuingia Kibu Denis.

Hadi Chama anatoka alikuwa ndiye ametoa pasi iliyozaa bao la kwanza la Simba. Ni jambo ambalo amezoea kulifanya kila siku.

Swali kubwa na mshtuko wa mashabiki ulikuwa kwanini Chama anatolewa katika dakika zile. Ni ajabu na kweli.

Chama ndiye staa wa timu. Ni mchezaji ambaye hata wenzake wote wanakiri kuwa ni wa daraja la tofauti. Anajua halafu anajua tena.

Siku zote Simba imekuwa ikicheza kumzunguka Chama. Huyu ndiye anayeamua washambulie vipi na katika wakati gani. Anamiliki mpira, anafungua timu, anaanzisha mashambulizi, anapiga pasi za mabao na kufunga pia.

Haijalishi ameanza mechi vipi lakini siku zote Chama ndiye ufunguo wa Simba. Kuna namna wachezaji wengine wanakuwa huru uwanjani Chama akiwepo.

Wataalamu wa soka huwa wanasema mchezaji mahiri hata asipocheza vizuri kwa dakika nyingi, anahitaji dakika chache tu uwanjani kubadilisha kila kitu.

Hii ndio sababu wachezaji tegemeo kwenye timu huwa hawatolewi kirahisi. Akili yao inaweza kuamua mechi muda wowote.

Kama unakumbuka katika fainali za Kombe la Dunia, Kylian Mbappe hakucheza vyema kwa dakika 60 dhidi ya Argentina, lakini kwa dakika chache tu alibadilisha upepo wa mchezo husika.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Neymar dhidi ya Croatia. Alizurura kwa muda mwingi wa mchezo, lakini alibadili upepo kwenye dakika za nyongeza na kufunga bao maridadi.

Ndivyo wachezaji mahiri huaminiwa. Lakini huyu kocha mpya wa Simba anamtoa staa timu yake ndani ya nusu saa ya kwanza. Inashangaza sana.

Nini kilitokea baada ya hapo. Ni kweli Simba walipata mabao mengine mawili, lakini timu ilipoteza balansi.

Simba ikapoteza umiliki wa mpira mbele ya Mbeya City pungufu. Wakaanza kuutafuta kwa tochi. Wakawa wanashambuliwa kama nyuki walioona maua mazuri.

Kocha Juma Mgunda akasimama kumuuliza Saido Ntibazonkiza kwanini Mbeya City wanacheza zaidi wakati wako pungufu? Lakini hakuna kilichobadilika. Mechi ilimalizika mashabiki wa Simba wakiwa wameshika roho mkononi.

Pamoja na ushindi, lakini mashabiki hawakuwa na furaha. Wamezoea kuona Simba ikicheza vizuri dhidi ya mpinzani yeyote na kushinda.

Walitarajia kushinda mabao mengi zaidi hasa baada ya Mbeya City kuwa pungufu. Wanakumbuka namna walivyoshinda 5-0 dhidi ya Mtibwa Sugar pungufu na kuidhalilisha Tanzania Prisons kwa mabao 7-1 baada ya kuwa pungufu.

Hawa ndio mashabiki wa Simba. Wanataka timu yao ishinde lakini pia icheze vizuri. Kipindi cha nyuma wamewahi kufukuza makocha kama Dylan Kerry, Joseph Omog na wengineo kwa sababu timu ilikuwa haichezi vizuri japo wanashinda.

Hivyo Robertino anatakiwa kuchagua pepo yake. Kwanza lazima atambue umuhimu wa Chama kwenye timu yake. Huyu ni kipenzi cha Wanasimba. Wakati huu timu ikielekea katika mashindano ya kimataifa ni vyema kocha huyu awe amefahamu namna vyema ya kumtumia Chama.

Hizo mechi za hatua ya makundi zinamtegemea sana Chama. Kule soka linachezwa kwa uzoefu na akili kubwa kama ya Chama.

Haya mambo ya kumng’ang’ania Kibu Denis na kumuweka Chama benchi yanaweza kumponza mapema.

Yanaweza kufanya kazi yake iwe ngumu zaidi pale Simba kuliko namna anavyofikiria.