Moto wa Fei Toto hauzimiki Bara

Muktasari:
- Mfano ni gwiji anayeishi (The Living Legend), John Bocco ambaye amefunga mabao 156 ya Ligi Kuu Bara huu ukiwa ni misimu wake wa 17 katika ligi hiyo, sasa akiitumikia JKT Tanzania baada ya kufanya makubwa akiwa na Azam FC na Simba SC.
KUNA rekodi zilizoandikwa na wanasoka nchini, ambazo kizazi chochote (Gen Z) kinaweza kikasisimka na kutamani kuwafahamu zaidi malegendari hao na zikatumika kama chachu ya kujituma kwa bidii.
Mfano ni gwiji anayeishi (The Living Legend), John Bocco ambaye amefunga mabao 156 ya Ligi Kuu Bara huu ukiwa ni misimu wake wa 17 katika ligi hiyo, sasa akiitumikia JKT Tanzania baada ya kufanya makubwa akiwa na Azam FC na Simba SC.
Bocco alivunja rekodi ya mabao ya Ligi Kuu iliyokuwa ikishikiliwa kwa miaka mingi na mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyefunga mabao 153 katika misimu 13.
Wengine ni gwiji wa Yanga, Edibily Lunyamila, mchezaji pekee aliyefunga hat-trick mbili katika mechi moja ya Ligi Kuu Bara wakati alipofunga mabao sita timu yake ikiichakaza RTC Kagera kwa mabao 8-0 mwaka 1998.

Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’, ni mchezaji pekee ambaye hadi leo amefunga hat-trick katika mechi ya Dabi ya Kariakoo wakati Simba ikiichakaza Yanga 6-0 mwaka 1977.
Sunday Manara ‘Computer’, Haruna Moshi ‘Boban’, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’, ni baadhi ya wanasoka wakongwewenye majina mazito, yanachokifanya kizazi cha Gen z kuzisoma taarifa zao.
Nyuma yao wapo wakali kibao, lakini huwezi kuchukulia poa yupo kazi nzuri inayofanywa na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye anaanza kuandika rekodi zake kibabe.

Fei Toto ni kizazi cha Gen Z kuna mastaa wa zamani wakati wanacheza alikuwa bado hajazaliwa ila amezikuta simulizi kuwahusu zilizofanya kumpa chachu ya kupambana kuweka heshima itakayokuja kusimuliwa na vizazi vingine.
Mwanaspoti limekusanya data za Fei Toto, jinsi staa huyo alivyoanza mdogomdogo kuandika rekodi na moto wake ukiendelea kuwaka zaidi Bara.
Tangu awali, usajili wake ndani ya kikosi cha Yanga ulikuwa na utata baada ya kutambulishwa Singida United ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars mchana na jioni kutambulishwa Yanga ambayo alianza kuitumikia katika msimu wa 2018/19.

Hakuwa bora zaidi katika eneo la kufunga kutokana na kutumika kama kiungo mkabaji hadi hapo Nasreddine Nabi alipoamua kumbadilisha nafasi akimtumia zaidi kama kiungo mshambuliaji.
Safari ya kuja Tanzania Bara ilianza baada ya kung’ara na JKU ya Zanzibar aliyobeba nayo taji la Ligi Kuu ya visiwani humo kwa misimu miwili mfululizo 2016-2017 na 2017-2018.
Pia kung’ara katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2018 akiwa na jezi namba 3 enzi hizo, ndio iliyoivutia Singida United na kufikia hatua ya kuzungumza naye, kisha kumpa mkataba wa miaka mitatu asubuhi na kumvusha Bahari ya Hindi kuja Bara.

Hata hivyo, saa chache baadaye siku hiyo hiyo, mida ya jioni akaibukia Jangwani. Yanga ilipindua meza, baada ya kumalizana na mabosi wa JKU waliokuwa na mkataba naye na kumpa dili la miaka minne kabla ya kuuongeza tena.
Baada ya kuonyesha ubora wake ndani ya kikosi cha Yanga kwa misimu miwili mfululizo, kiungo huyo aliyejaliwa kipaji alianzisha mgomo wa kuikacha Yanga ikielezwa alishamalizana mapema na Azam FC.
Mwanaspoti linakukusanyia data zake katika misimu saba aliyocheza Ligi ya Bara kwa maana ya mabao, mechi, dakika na asisti (angalia majedwali).

MWENYEWE ATIA NENO
Fei ambaye msimu huu tayari ana asisti tisa akiongoza katika kutoa pasi zilizozaa mabao katika Ligi Kuu Bara hadi kufikia nusu ya msimu, ameliambia Mwanaspoti kuwa anatamani kuandika rekodi yake mwenyewe kwenye ligi na hana ushindani wa kufikia rekodi ya staa yeyote.
“Nafasi yangu kucheza uwanjani inabadilika kulingana na mechi au kocha anataka kunitumia eneo gani kwa wakati huo kwani naweza kucheza kama mshambuliaji wa mwisho, namba kumi na kiungo mkabaji hivyo siwezi kusema nataka kufikia rekodi ya fulani zaidi nataka kuandika rekodi yangu mwenyewe. Kwa sasa nina furaha kwa kuvunja rekodi yangu ya asisti.”