Prime
Mnguto: CAF imetuacha na makovu Coastal Union

Muktasari:
- Katika sehemu hii ya pili na ya mwisho, Mnguto anaendelea kufafanua mambo mbalimbali ikiwamo yanayompa faraja kubwa kwenye utawala wake ndani ya bodi ya ligi na Ligi Kuu Bara kutambulika namba nne kwa ubora Afrika.
JANA ilikuwa sehemu ya kwanza ya mahojiano ya Mwanaspoti na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Steven Mnguto na alizungumzia mambo mbalimbali ya uongozi wake ndani ya bodi hiyo, ishu za waamuzi, masuala ya rushwa na mengine mengi.
Katika sehemu hii ya pili na ya mwisho, Mnguto anaendelea kufafanua mambo mbalimbali ikiwamo yanayompa faraja kubwa kwenye utawala wake ndani ya bodi ya ligi na Ligi Kuu Bara kutambulika namba nne kwa ubora Afrika.
"Kwanza ligi yetu kuwa bora ni kama naacha alama, lakini hawa watu niliowaamini kufanya nao kazi, wamekuwa bora na kuleta matokeo bora.
"Zamani ilikuwa tukipangwa na timu za nje lazima hofu iwepo, ila sasa hivi hatujali, tuko vizuri. Hata wao wakipangwa na Yanga wanajua safari imeishia hapo. Au na Simba wanajua mtihani ni mgumu.
"Hayo ni mambo ya kufurahisha sana kwa sababu tumeondoa ufalme wa Waarabu kuogopwa, ingawa siyo kwa asilimia zote, hiyo ni hatua kubwa."

SURA YA UONGOZI WA BODI
Anasema kwenye Bodi ya Ligi Kuu Bara uongozi ni imara na mambo yanaendeshwa kisasa na hadi inapata hati safi kila mwaka kutokana na hesabu zao kuwa vizuri.
"Uongozi wa sasa umenyooka, utaona mtendaji mkuu ana watu wake, hata upande wa masoko na habari. Kila eneo limenyooka na kutulia kiukweli.
"Ndiyo maana unaona bodi iko vizuri, sidhani kama kuna changamoto yoyote kwenye utendaji, mahesabu yetu yanakaa vizuri, tunapata hati safi kila mwaka, tunajitahidi haki za wachezaji na wafanyakazi wetu ziko vizuri."
YEYE NI COASTAL UNION DAMU
Wengi wanadhani kila shabiki wa soka nchini ni ama awe Yanga au Simba. Hata hivyo, kwa Mnguto ni tofauti na anasema hajawahi kushabikia timu nyingine zaidi ya Coastal Union.
"Hutakuja kuona nashabikia timu nyingine. Coastal naipenda kutoka moyoni. Zaidi ya hiyo labda iwe inawakilisha nchi. Licha ya kuwa bado Coastal inapata shida kwenye kupata wadhamini, lakini hatupoi kiasi hicho, tunajitahidi kufuatilia baadhi ya vitu.
HAJAITUPA KIUONGOZI
Anasema licha ya kukaa pembeni kiuongozi baada ya kufanyika uchaguzi Desemba mwaka 2024, lakini bado yuko karibu na uongozi kama mshauri.
"Bado niko karibu na uongozi katika nafasi ya ushauri. Ingawa wapo wanaokupenda na wanaokuchukia, unaposhari kitu kizuri wapo wanaosema unawaingilia wenzio.
"Hata hivyo, mara nyingi huwa natoa ushauri kwa mwenyekiti wangu kumweleza kile ninayoyaona na huwa anayapokea na kuyafanyia kazi."
AMEWAACHIA BASI
Akiwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo anasema walipata udhamini uliowapa basi kwa ajili ya timu. Hii ni baada ya uongozi uliokuwepoo kuondoka kwa kushindwa kuipandisha timu Ligi Kuu Bara.
"Nilianza nikiwa makamu mwenyekiti, sikuwa napenda sana uongozi ila niliombwa baada ya kufungwa na Mbagala Market mabao saba.
"Sisi watu wa Tanga ni wastaarabu sana, kwa hiyo walivyoona mambo yanaenda kombo wakaachia ngazi ndipo uongozi wangu ulipoanzia na tukapandisha timu.
"Baada ya kuipandisha timu Ligi Kuu Bara, tukapata basi kwa udhamini wa Tanga Cement. Ni basi aina ya Coaster ndilo gari la kwanza wakati huo mimi nikiwa makamu.
"Hadi naondoka, tumeshapata basi jipya na kiwanja ambacho siku za mbele tutajengea kiwanja cha mazoezi na mashindano, pia mabweni ya wachezaji."

MECHI ZA CAF ZAACHA MAKOVU
Coastal Union msimu huu ilipata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuondolewa hatua ya awali na Bravos do Maquis ya Angola.
Katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa wa Tundavala mjini Lubango, Angola, Coastal ilichapwa mabao 3-0, kabla ya kurudiana Azam Complex, Chamazi na kutoka suluhu na Mnguto anasema mechi hizo ziliwaachia maumivu makubwa na madeni, ingawa wanajipanga tena msimu huu.
"Tulipopangwa kucheza kimataifa ilitupa faraja japokuwa ilihitaji pesa nyingi, ila tulijitahidi sana kwani tulipata michango mbalimbali.
"Ila tuwe wa wazi, imetuachia makovu na madeni yaliyotufanya turudi chini, lakini tunajipanga kuwa bora msimu ujao na tumewaachia hilo jukumu uongozi mpya."
UONGOZI ULIVYO
Uongozi wa Coastal Union kwa sasa unaongozwa na mwenyekiti ambaye ni Muhsin Ramadhan Hassan na makamu mwenyekiti Dr Fungo Ally Fungo, wajumbe wa kamati ya utendaji pamoja na wajumbe saba na awali kabla uya uchaguzi uliofanyika Desemba mwaka jana, Mnguto aliamua kukaa pembeni ili kumpisha mwingine ajaribu.
"Coastal Union ulivyo uongozi wake tunachaguana, hakuna haya mambo ya uchaguzi ambayo nimeyaona miaka ya hivi karibuni.
"Kwa hiyo ilipokaa sana na kufanikiwa kwa kiasi, nikaona bado sijafika mwisho lakini kwa nini mwingine asijaribu.
"Tukakubaliana na wanaoniunga mkono, twende kwa njia hii na uchaguzi ufanyike ili tuone wengine. Bahati nzuri mwenyekiti wa sasa ni aliyekuwa makamu wangu. Pia kizuri ni, tunabadilisha katiba ambayo inasema mwenyekiti anakwenda kugombea na mwenza."
KARIA NDANI YA COASTAL UNION
Inafahamika kwa wengi Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) ni shabiki wa Coastal Union kama ilivyo kwa Mnguto ambaye awali ameeleza ndiyo timu iliyoko moyoni mwake.
Hata hivyo wengi wamekuwa wakiona klabu hiyo ikifanya vibaya licha ya kuwa na viongozi hao wakubwa kwenye oska la Tanzania.
Mnguto anasema sio kama wengi wanavyofikiria, na wao wapo kwa ajili ya kuziongoza timu zote kwa haki na hawawezi kuipendelea moja ikiwamo Coastal wanaoishabikia.
"Haikuwa rahisi viongozi wote wakubwa kuwa wadau wa Coastal, ikifanya vizuri wanasema kwa sababu ya uwepo wetu. Wengine wanasema rais yupo ndani na timu inataka kushuka daraja.
"Sisi tulikuwa tunaonyesha uadilifu wetu kwa sababu tumekuja pale ili kuziongoza timu zote ziweze kupata haki sawa na sio kuipendelea Coastal.
"Ikionewa lazima niseme jamani kuna kitu hakiko sawa. Watu wanapata tabu kuandaa hizi timu na kuna wakati hadi waandishi wanasema hakuna klabu inayoonewa kama hii yetu na tupo.
"Ikija kesi ya Coastal huwa nakaa pembeni namwachia makamu aongoze kikao, hata kama imebabuka kihalali ni sawa kanuni ichukue mkondo wake."
KUMBE COASTAL INA UWANJA
Anamshukuru Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu kwa kuwapa eneo walilopanga kujenga uwanja kwa ajili ya mazoezi na anakiri licha ya mambo kuwa mengi ila wanataka kuweka nguvu zao huko ili kutokuendelea kutumia Uwanja wa Mkwakwani kwa mazoezi.
"Tunamshukuru Mheshimiwa Ummy Mwalimu. Alitusaidia kupata kiwanja. Kuna wakati kabisa tuliamua kukishughulikia ila tukajikuta tuna mambo mengi.
"Kuna mtu ameahidi nyasi na mbegu tayari tumeshazipata, kilichobaki ni sisi kuweka nguvu katika kusafisha na tuliwahi kuufanyia hivyo lakini unakuta haufanyiwi kitu chochote na majani yanaota. Ila tutapatengeneza kiwe kiwanja kizuri cha mazoezi.
"Mkwakwani tutapaacha kwa sababu hairuhusiwi kiwanja cha mechi kufanyiwa mazoezi."
KANUNI KUZIBANA TIMU LIGI KUU
Kutokana na mambo yaliyotokea kabla ya tarehe ya mchezo wa Ligi Kuu Bara wa Kariakoo Derby wa Yanga na Simba, ikiwamo Wanamsimbazi kuzuiwa kuingia Uwanja wa Benjamin Mkapa kufanya mazoezi ya mwisho kwa mujibu wa kanuni, Mnguto amegusia hilo huku akiweka wazi Bodi ya Ligi Kuu itaboresha kanuni ili kuzibana klabu ziwe na viwanja vya mazoezi.
"Kilichotokea ishu ya Yanga na Simba, tutaboresha kanuni zetu zaidi, kuanzia msimu ujao kutakuwa na kanuni, kila timu iwe na uwanja wa mazoezi, kama huna basi usahau kucheza ligi.
Pia Mnguto ametoa wito kwa klabu zote kuwazingatia vijana kwani ndio watakaokuza soka la nchi hii kwani yeye sio muumini wa kusajili wachezaji kutoka nje.
"Ninachojaribu kushauri timu ni kukuza vijana. Hawa ndio watakaokuza soka letu, mimi ni muhanga wa kusajili wachezaji wa nje.
"Najaribu kuwashauri viongozi wangu kuhusu wachezaji wa nje kwa sababu cha kwanza hatupati watu sahihi, cha pili ni gharama kubwa, hivyo ni bora tukawakuze wa kwetu.
Hata hivyo, anakiri uwepo wa nyota wa kigeni ndio waliosaidia kukuza soka letu na hadi kufikia kuwa namba nne Afrika lakini bado kuna umuhimu kwa wazawa ili wapate muda wa kucheza.
"Ila wachezaji wa kigeni ndiyo wametusaidia kukuza soka letu lakini kuna muda wanaweza kucheza wazawa hawa wakakaa benchi."

SAKATA LA LAWI
Anasema sakata la mchezaji huyo kutakiwa na Simba na kusalia Coastal, hilo limeisha.
Lawi alikuwa akitakiwa na Simba na tayari ilikuwa imelipa pesa za usajili kabla ya beki huyo wa kati kwenda kuajaribu bahati katika klabu ya K.A.A Gent ya Ligi Kuu ya Ubelgiji na alifanya hadi vipimo vya afya kabla ya kurejea kwa wanamangushi kukipiga msimu huu na anasema kama itatokea klabu inamhitaji watamuuza.
"Hili lilishapata ufumbuzi, kwa sababu Lameck (Lawi) anacheza, tulishindwa kuwapa Simba kwa sababu walishindwa kufikia makubaliano.
"Akihitajika sehemu tutamuuza, ila kuhusu Simba ni watu waelewa sana tulishafikia makubaliano tukamaliza kila kitu na tukawa sawa, kwa sababu huwezi kuzuia kuhitajika kwa mchezaji."

NI NGUMU KUZUIA WACHEZAJI KUUZWA
Anasema Coastal ni klabu inayotengeneza wachezaji na wanapohitajika na klabu nyingine wanawauza kama ilivyotokea kwa Bakari Mwamnyeto kwenda Yanga, Abdul Hamisi Suleiman 'Sopu' aliyetua Azam FC na wengineo.
"Sisi tunatengeneza wachezaji na kuuza. Imelazimika kuwa biashara yetu kwani huwezi kuizuia Azam, Simba na Yanga kumchukua mchezaji watakayemtaka wakija kugonga mlangoni kwako.
"Timu kubwa usipozifungulia mlango, basi watauvunja tu, hivyo hakuna haja ya kufika huko kote, unawauliza tu wanamtaka nani, unakaa nao mezani na kufanya makubaliano na kuweka wazi kiwango chetu."

MWAMNYETO AWAPA UDHAMINI
Katika usajili wa dirisha kubwa msimu wa 2020-2021, Yanga ilimsajili Mwamnyeto na hapa Mnguto anaelezea dili hilo lilivyokuwa baada ya Simba nao kumhitaji.
"Mchezaji wa kwanza kutupatia pesa ni Bakari Mwamnyeto, alitakiwa na Simba na Yanga, wote walinijia, nikawaambia jamani, hatuwezi kumzuia ila naomba tukubaliane kitu kimoja.
"Wewe si una GSM na mwingine MO, mimi nataka 150 milioni za usajili, Simba wakasema inategemea na bosi mwenyewe, Yanga wakakubali, tuliona ni udhamini lakini kama tumemtoa bure.
"Kwa sababu tulikuwa hatuna udhamini, kwa hiyo kitu kilichokuwa rahisi kwetu ni hicho, baada ya hapo ndio tukawa tunapata wafadhili."
SOPU, AKPAN WAIPA COASTAL 200 MIL
"Tukamuuza Sopu (Abdul Hamisi Suleiman) kwenda Azam (msimu wa 2022-2023) tukapata Sh100 milioni, mwaka huo tulitengeneza hela nyingi maana Simba ilimchua Victor Akpan kwa bei hiyo, tukamaliza kwa faida ya Sh200 milioni.
"Hata sasa atakayetokea kumtaka Lawi aje mezani tuzungumze biashara ili mambo yaweze kwenda vizuri," anamaliza Mnguto.