MJUAJI: Yanga noma, iliichapa Brazil 3-1

Kikosi cha Yanga 1974

TIMU ya taifa ya Brazili iliwasili nchini Jumanne ya Mei 8, 1973. Timu hiyo ilipokewa na mashabiki wengi wa soka katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam (DIA).

Mchezo kati ya timu hiyo ya taifa ya Vijana ya Brazil ulikuwa uchezwe Mei 9 katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) lakini ulihairishwa.

Katibu Mwenyezi wa Young Africans (Yanga), Mshindo Mkeyenge alisema sababu za kuahirishwa kwa mchezo huo ni uchovu wa safari wa wachezaji wa timu hiyo, kwani ilitua Jumanne.

Kati ya watu mashuhuri waliojitokeza uwanja wa ndege kuipokea timu hiyo, pia alikuwapo Mwenyekiti wa Yanga, Mangara Tabu Mangara.

Taarifa ya kusitisha ni, basi la wachezaji wa timu hiyo ya Brazil lilipokuwa likitoka uwanja wa ndege lilipata ajali kwa kugongana na gari lingine katika barabara, njiapanda iendayo uwanja wa ndege, hata hivyo, hakuna aliyeumia kwenye ajali hiyo.


SABA TISHIO

Kwa mujibu wa Meneja timu ya Brazil, Antonio Zaccur timu hiyo ya vijana ilikuwa na wachezaji saba ambao walikuwa wakitegemewa kuliwakilisha taifa hilo katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1974 kule Munich, Ujerumani Magharibi.

Wachezaji hao ni Ze Luiz, Laeocio ambaye ni kapteni, Wagner, Ivan, Feitosa, Chico na Sergio.

Alipouzungumzia mchezo wao dhidi ya Yanga, Zaccur alisema walipokuwa katika ziara nchini Uganda walipata sifa za wachezaji wa Yanga.

Alisema anajua anakutana na timu kali na yenye wachezaji wazuri wenye uwezo wa hali ya juu lakini timu yake ingefanya kila juhudi ili iibuke na ushindi.


ILIPIGA MTU 13-0

Timu hiyo ya vijana ya Brazil iliikuwa katika ziara ndefu barani Afrika na Uarabuni na tayari ilikuwa imecheza michezo 10 bila ya kupoteza hata mmoja.

Ilipokuwa Abu Dhabi ilicheza michezo sita na kushinda yote. Katika mchezo wake mmoja iliifunga timu mabao 13-0.

Ilipoenda Sudan ilitoka sare 1-1 na timu ya taifa ya nchi hiyo, ikaifunga El Hilal ya huko bao 1-0. Ilipokuwa Uganda ilitoka sare 1-1 na timu ya taifa ya nchi hiyo.


KOCHA YANGA ATAMBA

Wakati huo Yanga ilikuwa inanolewa na Kocha Mromania, Professa Victor Stansculescu ambaye alisema mechi hiyo ingekuwa ngumu na kuahidi angeibuka na ushindi.

Kikosi cha Yanga kilikuwa kinaundwa na wachezaji wafuatao.

Elias Michael, Muhidin Fadhil, Selemani Said, Boi Idd ‘Wickens’ na Kilambo Athuman. Wengine ni Hassan Gobbos, Adam Juma, Leonard Chitete, Omar Kapera, Abdulrahaman Juma, Kitwana Manara, Sunday Manara, Maulid Dilunga na Gilbert Mahinya.


MCHEZO WENYEWE

Yanga iliichakaza timu hiyo ya vijana ya Brazil kwa mabao 3-1 katika mchezo mkali wa kirafiki ambao uliwavutia mashabiki waliojitokeza Uwanja wa Taifa.


Katika mchezo huo, maelfu ya watazamaji kutoka sehemu mbalimbali za mji wa Dar es Salaam na vitongoji vyake walijitokeza, mabao yote ya Yanga yalifungwa katika kipindi cha kwanza.

Mashabiki walianza kuingia uwanjani saa nne asubuhi ili kuwahi nafasi ya kuweza kuuona mchezo huo vizuri.


YANGA MAPEMA TU

Katika dakika ya pili tu, Yanga iliandika bao lililofungwa na Leonard Chitete aliyepokea pasi kutoka kwa Abdulrahamani Juma. Yanga ilikuwa ya moto, dakika moja baadaye iliandika bao la pili. Safari hii tena pasi ilitoka kwa Abdulrahamani Juma ambaye aliwapunguza mabeki wawili wa Timu ya Brazil na kumpasi Maulid Dilunga aliyeukwamisha wavuni.


DHARAU ZAWAPONZA

Wachezaji wa Brazil walionekana kuanza mchezo huo kwa kucheza kwa dharau na kujiamini walikuwa kama wamepigwa na mshangao kwa kilichotokea.

Walishangazwa na kiwango kilichoonye shwa na wachezaji wa Yanga.

Hawak utegemea kufungwa mabao hayo mawili ya haraka kwa muda mfupi sana. Kabla hawajajiuliza vizuri wakajikuta wakipigwa bao la tatu.

Kona iliyopigwa na Abdulrahamani Juma ilimpa nafasi Chitete kufunga bao la tatu. Kabla ya kufunga bao hilo, mpira huo ulimkuta Mbrazili, Wegner na akashindwa kuuokoa vizuri na kuanguka miguuni mwa Chitete aliyefumua shuti kali lililojaa kimiani na kumshinda kipa Luiz Carlos.


NGOMA NGUMU

Kipindi cha kwanza, mchezo ulitawaliwa na Yanga na kuwapa wakati mgumu washambuliaji wa Brazil kina Ivan, Chiko, Mario, Feitosa na Sergio kuipenya ngome ya Yanga.

Ngome hiyo iliundwa na wachezaji mahiri kina Ali Yussuf, Kilambo Athuman, Omar Kapera na Hassan Gobbos.

Kipindi cha pili, Brazil iliingia kwa kasi na kutokana na maelekezo ya Kocha Jose de Souza na kusababisha hatari nyingi katika lango la Yanga.

Kipa wa Yanga, Fadhil Muhidin alifanya kazi ya ziada kuokoa michomo ya hatari katika kipindi hiki. Mara nne kipa huyo alipangua hatari ya mipira iliyopigwa na kichwa na Laercio, Chico na Ivan ambayo yangeweza kuzaa matunda kwa Wabrazili hao.

Bao la kufutia machozi lilifungwa na Amnaldo ambaye alipiga shuti kali la chinichini lililojaa kimiani na Muhidini kushindwa kuliona.

Yanga ndio iliyokuwa timu pekee kuifunga timu hiyo ya Brazil katika ziara yake hiyo. Kwa furaha mashabiki wa Yanga waliingia uwanjani na kuwabeba wachezaji wao juu ya mabega yao.

Gazeti la Uhuru iliifanya habari ya hii kuwa kubwa (lead story) kwa kuiweka ukurasa wa mbele.

Iliandika kwa maneno makubwa na meusi Yanga 3 Brazil 1 na kuambatanisha na picha ya mchezo huo.