Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MJUAJI: Mgogoro wa Yanga ni bifu la Tambwe Leya na Sunday Manara

MJUAJI: Mgogoro wa Yanga ni bifu la Tambwe Leya na Sunday Manara

KWANZA napenda kuwaomba radhi wasomaji wa safu hii kwa kosa la kuandika mgawanyiko wa Yanga uliwafanya wachezaji kujiunga na Mseto ya Morogoro. Ukweli ni kwamba walijiunga na Nyota Afrika ya Morogoro na baadaye Pan Africa.

Baada ya hilo, ningependa leo kuwapa zaidi juu ya mgogoro wa Yanga na mambo yalivyokuwa kuanzia 1975 na kumbukizi hizi zitakuwa katika mfululizo wenye kusisimua.


MWALIKO WA KENYA

Aprili Mosi, 1975 Yanga ilipata mwaliko kwenda kucheza mechi za kirafiki nchini Kenya katika miji ya Nairobi na Mombasa. Chama cha Soka cha Kenya (KFF sasa FKF) kiliandikia timu hiyo ikiwa ni Mabingwa wa soka la Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Yanga ilipangiwa kucheza na Abaluya (sasa AFC Leopards), Gor Mahia za Nairobi na Champion na Mwenge za Mombasa. Michezo hiyo pia iliaminika ingeipa maandalizi ya kucheza mchezo wa Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) dhidi ya Enugu Rangers ya Nigeria.


TAMBWE AMKATA MANARA

Katika hali ambayo haikutarajiwa, Kocha wa Yanga, raia wa Zaire (sasa DR Congo), Tambwe Leya alilikata jina la mchezaji mashuhuri wa timu hiyo, Sunday Manara ‘Computer’.

Mshambuliaji huyo alikuwa ni mchezaji tegemeo wa Yanga na timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Sunday aliitwa ‘Computer’ kutokana na uwezo wake hata kabla kifaa hicho hakijafika nchini na kutumiwa au kufahamika kwa watu wengi. Baada ya Tambwe kulikata jina la Sunday, viongozi wa Yanga akiwemo meneja wa timu, Shiraz Shariff walikutana ili kujadiliana siku moja kabla ya safari ya Kenya.

Kocha Tambwe alimzuia Sunday asiende kwa madai ya kutohudhuria mazoezi takribani wiki moja. Inadaiwa mchezaji huyo tegemeo alimuomba kocha wake wiki moja ya mapumziko, lakini hakukubaliwa naye kuamua kuchukua mapumziko hayo bila ruhusa.

Baada ya wiki moja kuisha, mchezaji huyo aliporudi mazoezini kocha wake alimshusha hadi kikosi B cha Yanga. Sunday alifanya mazoezi na kikosi hicho cha pili kwa wiki moja na kumuomba radhi kocha mbele ya wachezaji wenzake wa kikosi cha kwanza.

Wachezaji walio-tajwa kwenda ni Patrick Nyaga, Juma Pondamali ‘Mensah’, Juma Shabani, Leodegar Tenga na Omary Kapera ‘Mwamba’.

Wengine ni Selemani Jongo, Boi Idd ‘Wickens’, Mohamed Mkweche, Mohamed Rishard ‘Adolf’, Jellah Mtagwa na Nondo. Pia, walikuwemo kina Juma Matokeo, Muhaji Muki, Ahmad Omary, Gibson Sembuli na Moshi Hussein ‘Dayani.


MASHABIKI HOFU TUPU

Baada ya kikosi cha kwenda Kenya kutangazwa, mashabiki na wanachama wa Yanga wakaingiwa na wasiwasi kuhusu hatima ya mchezaji huyo tegemeo.

Mwenyekiti wa klabu, Mangara Tabu alisema walikuwa na wasiwasi kwa kuwa katika michezo ya kirafiki dhidi ya Breweries ya Kenya na Cosmo iliyofanyika nchini, Sunday hakuwemo.


APINDUA MEZA

Pamoja na jitihada za Kocha Tambwe kumzuia Manara asiwemo kwenye safari, lakini alimchemka. Mchezaji huyo alikuwemo. Hatimaye, meneja Shirazi alijitokeza na kusema hakuna mchezaji wa Yanga atakayekosekana kati ya waliotajwa pamoja na Manara.


MGOGORO HOTELINI

Hilo la Manara likaisha, timu ikaenda Kenya na kurudi salama. Ikiwa katika maandalizi ya mchezo wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Enugu Rangers, Yanga ilishindwa kuanza mazoezi baada ya kuzuiwa kuweka kambi hotelini - Bahari Beach nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Viongozi wa hoteli waligoma kuwapokea wachezaji kwa sababu ya deni la Baraza la Michezo (BMT) la Sh400, 000.

Ufafanuzi kidogo. Tangu nchi ipate uhuru serikali ndio iliyokuwa ikizihudumia timu zinazowakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa kupitia BMT. Hivyo Baraza hilo lilikuwa limelimbikiza kiasi hicho cha deni na kuifanya hoteli kugoma kuipokea Yanga kwa sababu ya kuhofia kuongeza deni.


MGOGORO HADI STARS

Wakati hali ikiwa tete katika suala la hoteli, Kocha Tambwe aliingia tena kwenye utata mwingine na Kocha wa Taifa Stars, Carl Berhard Trauttman.

Tambwe aliwagomea wachezaji Manara, Gibson Sembuli, Juma Matokeo, Muhaji Muki na Ahmad kujiunga na timu ya taifa hadi Yanga itakapomaliza michezo miwili dhidi ya Enugu Rangers.

Nini kiliendelea? Usikose wiki ijayo. Tuwasiliane kwa 0713 900017.