Prime
Tumetoka mbali na Sir David Beckham, mbali sana

Muktasari:
- Wakati ule Beckham akiwa katika ubora wake Waingereza walikuwa wakikufuru kila wiki juu yake. walituingiza katika dunia yake na kila siku tukaamka na David Beckham na kulala na David Beckam. Ilitushangaza sana kwa baadhi ya mambo ambayo Waingereza walikuwa wanatuambia katika kumtangaza David Beckham.
BLASPHEMY. Neno la Kiingereza ambalo kwa Kiswahili linamaanisha kukufuru. Sijui kwanini Wazungu wenyewe walianzisha neno hili wakati wakijua kwamba wanaongoza kukufuru. David Beckham wiki iliyopita amepewa cheo cha sir. Tumetoka naye mbali.
Wakati ule Beckham akiwa katika ubora wake Waingereza walikuwa wakikufuru kila wiki juu yake. walituingiza katika dunia yake na kila siku tukaamka na David Beckham na kulala na David Beckam. Ilitushangaza sana kwa baadhi ya mambo ambayo Waingereza walikuwa wanatuambia katika kumtangaza David Beckham.
Waingereza bwana! Kuna wakati walimuweka hadi katika msalaba wakidai kwamba ni yesu aliyepaa kuwakomboa. Waingereza walifanya mambo mengi ambayo yalikuwa kama kufuru ilimradi tu wamuweke juu David Beckham.
Miaka imesogea na kuna vijana wengi wa kizazi kipya hawajui Beckham alikuwa nani. Alikuwa mwanasoka mahiri, ndiyo, lakini sio zaidi ya Zinedine Zidane wala Ronaldo de Lima. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza duniani tulishuhudia kitu kinachoitwa ‘branding’ kwa mwanasoka.

‘Branding’ ni kutengenezwa kuwa mkubwa pengine kuliko ulivyo. Waingereza wakiwa wanatumia vyombo vya habari kama BBC, Reuters, SkySports na vinginevyo wakatufundisha namna ya kumtengeneza mtu kuwa mkubwa pengine kuliko alivyo.
Kama walivyoisambaza Ligi Kuu England katika kila kona ya dunia, ndivyo ambavyo walifanikiwa kumsambaza Beckham kama mtu mahiri zaidi katika soka duniani. Kumbuka kwamba alikuwa anaishi katika dunia moja na Zidane aliyewapa Ufaransa ubingwa wa dunia pale Paris. Kumbuka alikuwa anaishi katika dunia moja na Ronaldo de Lima ambaye aliwapa ubingwa wa dunia Brazil pale Yokohama.
Achana na wanasoka. Beckham alitengenezwa kuwa mkubwa kuliko wachezaji wa NBA. Akatengenezwa kuwa mkubwa kuliko madereva wa Formula One, akatengenezwa kuwa mkubwa kuliko Tiger Woods, akatengenezwa kuwa mkubwa kuliko mabondia wa uzito wa juu kina Lennox Lewis.

Kilichoongeza utamu katika kila kitu ni Beckham pia kumuoa Posh Spice. Victoria Adams. Wakatengenezwa kuwa kama mfalme na malkia. Na waliilazimisha dunia yote iwaone hivyo. Beckham alikuwa anafuatiliwa anapoamka hadi anapolala.
Kudhihirisha hilo ni kwamba hata jumba ambalo Beckham alikuwa anaishi pale Uingereza, Hertfordshire, lilijulikana kama Beckingham Palace wakilinganisha na makazi ambayo alikuwa anaishi Malkia Elizabeth II wakati huo, Buckingham Palace.
Baadaye Waingereza wakadai kwamba ingependeza kama sura ya Beckham ingekaa katika noti yao ya pauni. Tulisikia mengi wakati ule tatizo ni kwamba mengi tuliyasikia katika redio na kuyaona katika televisheni. Kama ingekuwa ni katika zama hizi za mitandao nadhani Beckham ndiye angekuwa mwanamichezo mwenye wafuasi wengi zaidi mitandaoni kuliko mwingine yeyote yule.

Leo Beckham ana wafuasi milioni 88 katika mtandao wa Instagram wakati Cristiano Ronaldo ana wafuasi milioni 658 huku hasimu wake Lionel Messi akiwa na wafuasi milioni 505. Ingekuwa tofauti kama Beckham yule wa Waingereza angekuwa katika nyakati hizi. Si ajabu angekuwa anashindana na Instagram yenyewe kwa wafuasi.
Waingereza walitufanyia mambo ya ajabu kwa Beckham. Mtu mmoja tu ambaye hakukubaliana na Waingereza alikuwa Sir Alex Ferguson. Alipenda mchezaji abaki kuwa mchezaji. Hakupenda Beckham alivyokuwa. Alikuwa kama mcheza filamu badala ya kubaki kuwa mcheza soka.
Mwishowe alimfukuza katika timu yake kwa mshangao wa wengi. Akamuuza kwenda Real Madrid. Na bado akiwa kule huku akicheza timu moja na Zidane na Ronaldo de Lima, bado Waingereza walihamishia kambi katika viwanja vya mazoezi vya Real Madrid, Valdebebas, kwa ajili ya kufuatilia maisha yake.

Baadaye Beckham akaenda zake Marekani na huko wakafuatilia maisha yake mpaka alipostaafu soka akiwa miongoni mwa wanamichezo wenye noti nyingi duniani. Katikati hapo alijaribu kufufua jina lake kwa kwenda Ufaransa na Italia, lakini hakuwa Beckham yule tena. Kuanzia hapo ndipo jina la Beckham liliponza kufifia.
Ukiwa hauchezi haufuatiliwi sana kama wale wanaocheza. Lakini zaidi ni kwamba kadri vizazi vinavyopita ndivyo ambavyo kidogo kidogo umaarufu wa mtu maarufu unaanza kupungua. Watoto wenye umri wa miaka 20 kwa sasa ambao ni wazi ni watu wazima hawajui Beckham alikuwa maarufu kiasi gani.
Wameishi kidogo katika dunia ya Messi na Ronaldo, lakini wasichofahamu ni kwamba bila kujali ukweli kwamba Messi na Ronaldo walikuwa bora sana uwanjani kuliko Beckham, lakini Beckham alikuwa maarufu zaidi kuliko walivyo katika zama hizi.

Lilikuwa suala la muda tu kabla ya Beckham kuwa sir. Hatimaye amekuwa sir kama ilivyokuwa kwa Sir Alex Ferguson. Na mkewe Victoria atakuwa akitambulika kama Lady Beckham. Tumetoka mbali na hawa watu. Sir Alex anaweza kuwa anasaga meno kwa sasa, lakini ukweli ni kwamba hakuweza kuuzuia umaarufu wa Beckham wakati ule. Ule moto ulikuwa mkubwa na haujawahi kutokea kwa mwanamichezo mwingine yeyote duniani.
Mtu ambaye hatujui kama anaweza kuja kuwa sir siku moja ni Wayne Rooney ‘Wazza’. Namba zake ni kubwa kuliko za David Beckham, lakini maisha yake binafsi yana tofauti kubwa na Beckham - Waingereza walishatengeneza kwamba Beckham ni ‘malaika’ na Rooney ni ‘shetani’.