Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ibenge: Mtihani upo hapa Azam FC

IBENGE Pict

Muktasari:

  • Azam ilimleta jijini Dar es Salaam kocha huyo kutoka DR Congo mapema wiki hii na kufanya mazungumzo na inaelezwa kila kitu kimeenda freshi na kilichobaki ni kutangazwa tu na kuchukua nafasi ya Rachid Taoussi wanayetarajia kuachana naye.

DONE Deal! Ndiyo, Azam FC kwa sasa inasubiriwa kutangaza tu juu ya kumnasa kocha mwenye heshima zake katika soka la Afrika, Florent Ibenge (63) aliyekuwa akiinoa Al Hilal ya Sudan.

Azam ilimleta jijini Dar es Salaam kocha huyo kutoka DR Congo mapema wiki hii na kufanya mazungumzo na inaelezwa kila kitu kimeenda freshi na kilichobaki ni kutangazwa tu na kuchukua nafasi ya Rachid Taoussi wanayetarajia kuachana naye.

Licha ya kwamba bado imefanywa siri kubwa, lakini ukweli ni Ibenge na Azam kila kitu kimeenda sawa na huenda isiwe ajabu kumuona akiinoa timu hiyo kwa msimu ujao wa 2025-2026 wa mashindano na tayari ina tiketi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ibenge ni mzoefu wa soka la Afrika, akizifundisha timu kadhaa ikiwamo AS Vita ya DR Congo, RS Berkane ya Morocco na sasa Al-Hilal ambayo mkataba alionao na timu hiyo upo mwisho na tayari ameipa taji hivi karibu ikishiriki Ligi Kuu Mauritania badala ya Sudan kuwa na usalama mdogo.

IBE 01

Hata hivyo, kama atakuwa yeye au mwingine kuna mambo manne yanayomsubiri kocha mpya ndani ya Azam iwapo atakabidhiwa mikoba ya kukinoa kikosi hicho na kipo nafasi ya tatu kwenye msimamo kikiwa na mchezo mmoja mkononi baada ya juzi kucheza na Tabora United.


AZAM MPYA

Ibenge mara atakapoanza kibarua hicho Azam, atakuwa na kazi kubwa ya kutengeneza timu mpya kabisa itakayofikia malengo ya mabosi wa klabu hiyo hususan kwa michuano ya kimataifa.

Hii ina maana sehemu kubwa ya wachezaji wa Azam wataondoka baada ya baadhi kumaliza mikataba, lakini wengine wataachwa na kuuzwa, kutokana na wachezaji wengi msimu uliopita kuonekana kuwa chini ya kiwango hali ilyochangia timu hiyo kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea mwanzoni mwa msimu.

Hapo kocha mkuu atakuwa na kazi ya kuijenga timu hiyo upya bila kujali wachezaji atakaowasajili ama atakaowakuta.

Kwa maana hiyo kuna majembe mapya ambayo kocha huyo anaweza kutua nao wakiwamo wanaotokea Al Hilal kwa nia ya kuipa nguvu timu, ili siku ya mwisho akichemsha asipate wa kumlaumu.

IBE 02

MAZINGIRA YA KAZI

Eneo lingine ambalo ni gumu kwa Ibenge au kocha atakayetangazwa Azam ni mazingira ya kazi kutokana na historia ya nyuma.

Makocha wengi waliopita Azam wamekuwa wakilalamikia baadhi ya vitu kwenye timu hiyo vimechangia wao kushindwa kufanikiwa.

Mfano kutokuwa na presha kubwa kwa wachezaji ili waweze kuwa bora na kuonyesha mchango mkubwa wa kuipambania timu hiyo kufikia mafanikio licha ya kuwa na kila kitu.

Azam licha ya kutokuwa na mashabiki wengi ni timu ambayo imejitosheleza na imekuwa ikisajili nyota wengi na bora kila msimu, lakini kwenye suala la ushindani sio timu shindani hasa ishu ya ubingwa.

Ni wazi Ibenge atakuwa na kazi ya kupambana na mazingira hayo ili kufikia malengo, vinginevyo yatamkuta kama yaliyowakuta makocha wenzao wenye majina walioinoa timu hiyo wakiwamo Mfaransa Dennis Jean Lavagne, Hans Van Pluijm (Uholanzi), George Lwandamina (Zambia), Joseph Omog (Cameroon) George ‘Best’ Nsimbe (Uganda) na Youssouf Dabo (Senegal).

IBE 03

ANGA ZA KIMATAIFA

Tangu Azam imeanza kushiriki mashindano ya Afrika haijawahi kufika hatua makundi. Imeshindwa hadi na Namungo iliyopata nafasi hiyo japo nayo ilitia aibu kwa kucheza mechi zote sita za kundi ilililokuwapo bila kushinda wala kufunga bao.

Kwa Azam wengi wanajiuliza nini kinawashinda? Azam ina pesa. Inafanya usajili mkubwa. Inaajiri makocha wakubwa. Kwa nini hawafanyi vizuri kwenye mashindano ya Afrika? Inafikirisha sana.

Hii ni mara ya pili inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. Wamerudi baada ya miaka tisa. Mara ya kwanza ni 2015 ilipotolewa na chama la zamani la kipa wao wa sasa, Mohammed Mustafa, Al Merrikh ya Sudan.

IBE 05

Mwaka jana wengi walikuwa  wanatazamia kuwaona wakifika makundi lakini mabo yakawa yale yale sasa endapo Ibenge atapewa mikoba ya kuinoa timu hiyo huenda akawa sehemu ya mafanikio au akawa timu wa kwanza kuandika rekodi kutokana na uzoefu alionao kwenye michuano hiyo, pia ana rekodi ya kufika hatua hiyo na kutwaa mataji.

IBE 04

UBINGWA WA BARA

Ni zaidi ya miaka 10 sasa, tangu Azam ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Ilifanya hivyo msimu wa 2013-2014 na wengi waliamini huo ni mwanzo wa timu hiyo kukusanya mataji ya ligi, lakini mambo hayakwenda hivyo.

Hiyo tayari ni presha kwa kocha mpya atakayetambulishwa Azam ili kurejesha ushindani na kubeba taji hilo sambamba na ile ya michuano ya Kombe la Shirikisho ilililotwaa mara ya mwisho 2018-2019.

Ibenge ana rekodi nzuri katika kuzipa timu mataji, hivyo hiki ni kibarua kingine cha kutaka kuonyesha ukubwa wake kwa kuibebesha Azam mataji ya michuano hiyo mikubwa nchini na kula sahani moja na vigogo Simba na Yanga zilizotawala kwa muda mrefu.