MEDDIE KAGERE: Mashabiki Simba tulieni, mambo matamu yanakuja

WIKI iliyopita tulipata ushindi wa kwanza ugenini katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwafunga wenyeji wetu, AS Vita ya nchini DR Congo.

Miongoni mwa sababu ambazo zilitusaidia kupata ushindi katika mchezo huo ni uzoefu wa mashindano ambao tumeanza kuwa nao.

Nakumbuka mara ya mwisho mpaka tunafika kwenye hatua ya robo fainali misimu miwili iliyopita tulikuwa na matokeo mabaya katika mechi zote tatu za ugenini.

Tulifanikiwa kufuzu kwenye hatua ya robo fainali kwa faida ya kucheza vizuri mechi za nyumbani, lakini ugenini tulikuwa vibaya.

Wakati tunacheza mechi hizo za ugenini licha ya kupata matokeo mabaya tulikuwa tunajifunza mambo mengi na kuna ambayo tumeanza kuyatumia msimu huu.

Wakati huo tulikuwa na ugeni wa mashindano kwani hatukuwahi kufika kwenye hatua kubwa kama hiyo katika mashindano haya makubwa kwa ngazi barani Afrika.

Kale kauoga ambako kalikuwepo kutokana na kutocheza mashindano haya kwa muda mrefu sasa hakapo na tunakwenda tukiwa na uzoefu kama washindani kweli.

Niwahakikishie msimu huu mambo yatakuwa tofauti kwa upande wetu katika mechi za ugenini, na tumelianza hilo dhidi ya AS VIta ambao ni moja ya timu kubwa na yenye uzoefu katika mashindano haya.

Kushinda Kinshasa dhidi ya AS Vita siyo kama ni jambo ambalo tulibahatisha, bali tulitenga muda wa kutosha kufanya maandalizi pamoja na mafunzo ambayo tuliyapata misimu miwili katika mashindano haya.

Msimu uliopita kwenye mashindano haya tuliondolewa na UD Songo katika hatua ya awali, jambo ambalo liliwaumiza wachezaji wengi ndani ya kikosi chetu pamoja na mashabiki.

Tuliondolewa na UD Songo kutokana na sababu kadhaa ikiwemo kushindwa kupata muda wa kutosha kufanya maandalizi tofauti na wenzetu walikuwa katikati ya msimu.

Hili nalo tumelichukua kama elimu kwetu na ndio maana katika mechi zetu za hatua ya awali zote tulifanya vizuri mpaka kufika kwenye hatua ya timu 16 bora barani Afrika.

Mipango ambayo tunayo baada ya kujifunza yote hayo na maandalizi ambayo tumefanya ni kufika katika hatua ya robo fainali.

Ubora wa wachezaji ulivyo pamoja na kucheza kitimu linawezekana kwani tuna benchi la ufundi zuri ambalo linatupatia mbinu za kutosha kwenda kuwakabili wapinzani.

Nguvu nyingine ambayo tunaipata msimu huu ni viongozi kutupatia mahitaji ya msimu kama motisha endapo tutacheza mechi za ugenini na nyumbani ambazo tutacheza katika Uwanjani wa Benjamin Mkapa.

Motisha hiyo ya pesa nyingi ambazo mchezaji anaweza kwenda kuzitumia na kumsaidia mchezaji katika maisha yake binafsi, mbali ya pesa ya mshahara ambayo huchukuwa kila baada ga mwisho wa mwezi ni kitu kizuri sana.

Msimu huu tuna faida ya kucheza nyumbani tukiwa na faida ya kuingiza mashabiki ambao wengi wao watakuwa wanatushangilia na kutupatia morali muda wote wa mchezo.

Unajua tunapocheza ugenini viwanja vya wenzetu haviruhusiwi kuingiza mashabiki, ila kuna wachache tu ambao wanalazimisha kupenya na kuja kushangilia timu zao.

Wakati kwetu hilo ni tofauti, tunaingiza mashabiki ambao nina imani kubwa ile nguvu ambayo watatuonyesha katika kutushangilia sioni sababu ya kushindwa mechi zetu za nyumbani il itakuwa kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita.

Lakini silaha nying-ine ambayo tunayo ni kufanya vizuri kwenye mechi za nyumbani, kwani unajua msimu uliopita tuliondolewa katika mashindano haya tukiwa bila kutarajiwa na UD Songo.

Awali nilieleza hilo yote tumeyachukua na haya tumeyafanyia kazi baada ya kujifunza na kutumia vizuri silaha zetu kwa maana maeneo ambayo tupo bora ili kufikia malengo.