Waziri Junior afichua namna alivyokatwa jina Simba

UKIZUNGUMZIA The King of CCM Kirumba utamtaja mshambuliaji Waziri Junior ambaye anaichezea klabu ya Yanga kwasasa.

Hilo limetokana baada ya kuonyesha uwezo wake akiwa na kikosi cha Toto African akiifungia timu hiyo magoli 10 msimu wa 2016/2017.

Akiwa mkoani humo msimu wa 2019/20 akiwa na klabu ya Mbao aliifungia timu hiyo magoli 13 na kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari katika Ligi Kuu.

Msimu huu amejiunga na Yanga lakini mpaka sasa ameifungia timu hiyo bao moja tu tena katika mechi dhidi ya KMC iliyochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba.

Mwanaspoti lilizungumza na mchezaji huyo na kufanya naye mahojiano wapi alipokwama tangu aingie Yanga na safari yake ya soka kiujumla itamalizikaje.


APITIA MAJANGA

Junior anasema wakati anatoka Toto Afrika na kujiunga katika klabu ya Azam alipitia katika maisha magumu ya majeruhi zaidi ya mwaka mmoja.

Mshambuliaji huyo alisema baada ya kukaa nje kwa mwaka mmoja, bado alikutana na changamoto katika mwaka wake wa pili lakini hilo halikumfanya aonyeshe utovu wa nidhamu.

“Mwaka wa pili nilikuwa nafanya mazoezi Azam na kucheza mechi za kirafiki, kuna muda nilitolewa kabisa timu ya wakubwa nikawa nafanya mazoezi na timu ya watoto ikiwa chini ya kocha Mingange.”

Junior aliongeza kwa kusema “Baada ya kuona kama napoteza ilibidi niombe kutoka kwa mkopo, wakati huo kulikuwa na timu nyingi zinanihitaji lakini niliamua kuichagua Biashara Utd.”


ATUA MBAO NA NEEMA

Baada ya kwenda Biashara UTD, bado Junior hakuwa na wakati mzuri katika kikosi hiko hivyo mkataba wake ulipomalizika Azam hawakumuongezea.

Junior anasema alituliza kichwa chini na kuanza kupiga hesabu ni wapi ambapo anaweza tena kuinukia ndipo ikaja ofa ya kwenda Mbao Fc.

“Nashukuru sana watu waliokuwa wamenizunguka mimi kwa kunishauri kwani licha ya mimi kujiamini tu wao pia walinitia sana moyo.”

“Said aliniambia mpira sio pesa tu bali ni kupata nafasi ya kucheza na kuwa vizuri pale unapocheza mara kwa mara unapokuwa upo uwanjani.”

Junior aliusifu ubora wa makocha wake Kidu na Baba Katalaiya kwani licha ya kupitia mazingira magumu walikuwa pamoja na timu.


ALIVYOTUA YANGA

Junior baada ya kufanya vizuri katika msimu uliopita akiwa na Mbao, anasema alipata ofa nyingi ikiwemo klabu yake ya zamani Azam lakini aliona ni bora aende Yanga kutokana na ukongwe wake.

Mshambuliaji huyo alisema ilipokuja ofa ya Yanga aliona ni muda sahihi kwake kwenda kucheza mpira ili pia atengeneze wasifu mwingine.

“Matarajio ya wachezaji wengi ni kwenda katika timu kubwa, huku unaweza ukapata vikombe ili kuongeza wasifu wako kama mchezaji.”

“Azam sio kama ni timu mbaya, wao wana kila kitu cha mchezaji ambacho anatakiwa kuwa nacho lakini niliona ni muda sahihi wa kusaini Yanga.”


HANA PRESHA

Licha ya kwamba Junior amekuwa hayupo katika kikosi cha kwanza Yanga mbele ya Michael Sarpong na Saido Ntibazonkiza, mshambuliaji huyo ameonyesha kutokuwa na presha.

Junior alisema suala la kucheza ni la muda tu kwani yeye hana majeruhi na ana imani akiendelea kupewa nafasi atafanya vizuri.

“Kipaji hakiwezi kufa bali fitinesi tu ndio itapungua, mimi sina majeruhi na hilo ndio jambo ambalo namshukuru Mungu, lakini nitaangalia nini natakiwa kufanya kulinda kipaji changu wakati ukifika.”

Aliongeza kwa kusema “Nafasi ipo sababu tunafanya kila tunachoelekezwa na mwalimu, kuhusu kwanini sio chaguo la kwanza inawezekana siendani na mfumo wake unavotaka kwa sababu hata Ulaya hayo mambo yapo.”


SAIDO AMPA UFUNDI

Junior anasema kucheza na wachezaji wa kigeni kwa pamoja ukiwa makini unajifunza vitu vingi na hilo pia amefaidika nalo akiwa na Saido Ntibazonkiza.

Mshambuliaji huyo alisema sio mara ya kwanza kucheza na wachezaji wa nje kwani alishacheza na wachezaji wengine wa nje akiwa Azam napo alijifunza vingi.

“Ukweli ni wachezaji ambao wazungu sana, kwenye maisha unatakiwa ujue jinsi ya kuishi na watu ili uwe na faida baadae, Saido ni mtu ambaye anapenda ufanye kitu chenye faida katika timu.”


ALIFANYIWA UHUNI SIMBA

Hii inawezekana ikawa ndio kali zaidi kwani Junior anasema wakati anatafuta kucheza soka la kulipwa nchini aliwahi kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Simba.

Junior anasema mwaka 2014 kulikuwa na majaribio katika uwanja wa Kinesi na alifika uwanjani hapo na alifanikiwa kupita katika majaribio lakini jina lake halikurudi.

“Ni kweli nilienda Kinesi mimi na ndugu yangu Swada kulikuwa na nafasi tano za kwenda kucheza Simba B, nilikuta watu wengi sana lakini mimi na mwenzangu tulifanikiwa kupita.”

“Licha ya kupita kilichokuja kutokea majina yaliyokuja kutajwa baadae mimi na mwenzangu hatupo, sijui nini kilichofanyika hapo lakini nashukuru Mungu mwaka 2015 nikapata nafasi Toto Afrika na nikacheza Ligi.”


KAZE HABARI NYINGINE

Hakuna ubishi kwamba kocha wa Yanga, Cedric Kaze ameifanya Yanga kuwa inapiga soka safi na mashabiki wamekuwa na imani nae kubwa.

Lakini kumbe kocha huyo ni mtu ambaye amekuwa akizungumza mara kwa mara na wachezaji wake ili kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.

Junior alikiri hilo kwa kusema, ”Kaze ni mwalimu ambaye anapenda umoja na usawa kwa timu nzima, hiko kitu ndio kinachotuunganisha sisi sote.”


MALENGO YAKE

Junior anasema anaamini kabisa kwamba taa ya kijani kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi imewaka baada ya kusaini na Yanga.

Mshambuliaji huyo alisema timu hiyo inafahamika kiola kona hivyo inakuwa ni rahisi kwake yeye kutoka na kujaribu kucheza soka nje.

“Kila kitu ni mipango ya Mungu, acha kwanza tusubili tuone nini kitatokea kwa sababu bado nina mkataba na Yanga, lakini hata wakati natoka Mbao kuna timu zilinihitaji lakini walikuwa na wasiwasi na mimi labda kutokana na timu niliyokuwepo.”

Junior alisema “Nina imani nitafanya vizuri na kujitengenezea wasifu bora zaidi ili isiwe tabu kwangu kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa.”