Fiston ajiapiza kukiwasha

Tuesday February 16 2021
fiston pic
By Clezencia Tryphone

Kuna mchezaji mmoja tu ambaye mashabiki wa Yanga wanasubiri kushangilia bao lake la kwanza kwenye mechi za mashindano. Huyu unayemuona hapo. Fiston Abdul Razaq. Mwenzie waliyetoka nae nchi moja Saido Ntibanzokiza ameshatupia na Yanga wanamkubali kinoma. Wawili hawa wamekuwa na historia nzuri za utikisaji nyavu kutoka katika klabu mbalimbali ambazo wamezitumikia kabla ya kutua Yanga katika dirisha dogo la usajili msimu huu.

fiston pic

Safu ya Yanga ilikuwa na changamoto kubwa ya upachikaji wa mabao licha ya Yanga kupata pointi tatu katika michezo yake lakini safu hiyo ilikosa nafasi nyingi za kufunga katika michezo yake.

Ilipelekea aliyekuwa Kocha wa Klabu hiyo Cedrick Kaze kupata wakati mgumu katika upangaji wa kikosi chake.


NAMNA ALIVYOTUA

Advertisement

Fiston nyota wa zamani wa timu ya JS Kabylie ya Algeria alitua Tanzania Januari 29, lakini licha ya ustaa wake hakulakiwa na mashabiki wengi kama ilivyokuwa kwa nyota wengine waliomtangulia. Kaze alisisitiza mchezaji awahi kambini haraka kwani hakuna muda wa kupoteza.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Fiston anakiri kuwa na kazi kubwa ya kulipa fadhila kwa wanayanga kutokana na mapenzi ya dhati juu yake.

“Kwa namna nilivyopokelewa niliona fahari sana na mimi kama mchezaji naimani nina deni kubwa sana kwa wanayanga,”anasema.


NAFASI YAKE YANGA

Anaamini nafasi ya kucheza anayo na ndio maana wakamtafuta kuja kuongeza nguvu ndani ya kikosi hicho.

“Yanga nafasi ninayo na ndio maana wamenisajili, namuomba sana Mungu anisimamie sana niweze kutimiza malengo hasa ya kile kilichonileta,”anasema mshambuliaji huyo.


NENO KWA MASHABIKI

Katika maisha yake ya kandanda anatambua kiu ya mashabiki uwa ni kuona mshambuliaji anafunga ili kuisaidia timu kupata matokeo.

wa Yanga wanataka nini, najua mashabiki hawataki kudroo au kufungwa wao wanataka kushinda tu, japokuwa hakuna timu duniani ambayo haijawahi kufungwa, hata Arsenal, Real Madrid, Liverpool zinafungwa japokuwa zinatwaa mataji lakini utakuta zimefungwa hata mechi mbili au tatu na kudroo pia,”anasisitiza.

Anasema yeye anajua kazi yake na majukumu yake, hivyo atahakikisha anaziba masikio na kuweka umakini kwa kufanyia kazi kilichomleta.

“Nawaomba sana mashabiki waniamini namwamini pia Mungu ataweka njia niweze kutimiza malengo na wao watafurahi tu ila wajue mpira una matokeo matatu na wayakubali pale inapotokea,”.


MATAJI JANGWANI

Yanga imekosa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara misimu mitatu mfululizo likitwaliwa na watani zao Simba wanaeendelea kutamba.

Fiston anasema, kwa uwezo wa Mungu kwa kushirikiana na wenzake anaimani msimu huu ni wa Yanga na sio timu nyingine kwa kuamini umoja ulipo ndani ya timu utapelekea kulitwaa taji hilo.

“Mimi kama mchezaji napenda sana kuona mafanikio katika timu ambayo naitumikia hivyo basi tutaanza na taji la ligi kuu mengine yatafuata,” anasema.


WATANZANIA WANAPENDA SOKA

Anasema Tanzania wanapenda sana mpira sio tu kwa klabu zao hata timu zao za Taifa zinapokuwa uwanjani hujitosa sana na kusapoti.

“Mimi kama mchezaji najua nina deni kubwa sana kwa klabu yangu ya Yanga na pia nataka kuwapa kile ambacho mashabiki wanakitaka, najua wanayanga wanapenda kuona mpira safi ndani ya timu yao”


HAPENDI MITANDAO

“Mimi sio mpenzi sana wa Mitandao lakini naitumia kutokana na wasifu wangu kwa sasa, najiepusha sana na mitandao inaweza kukujenga au kukubomoa, hivyo mimi naingia tu napost kitu alafu natoka, hata sijui wamelike wangapi na kukomenti,”anasema.

Anasema anajua madhara ya mitandao anajitahidi kujiepusha nayo kwa namna fulani kwani inanisaidia kudili na kazi yake zaidi.

“Mara nyingi mke wangu ndiye anaingia akiona mtu kaniuliza kitu cha msingi ananiambia mimi mtu akisubiri nitamjibu kupitia mitandao atachemka kwani siingii huko mara kwa mara naweza kuingia leo mpaka miezi minne ndio narejea tena,”anaeleza Fiston.


MAZINGIRA YA TANZANIA

“Mimi nipo tu niko hotelini hata kambini sijaingia, viongozi wanakuja wananichukua tunaenda kuangalia mpira wa nje alafu narudi hotelini mpaka pale nitakapoungana na wenzangu kambini,”


KANDARASI YAKE YANGA

Anaamini wanajangwani hao watamuongezea mkataba mwingine kwa kuamini na kuutambua uwezo wake awapo ndani ya uwanja.

“Kwa sasa nimesaini mkataba mfupi wa miezi sita kwa ajili ya kuwatumikia wananchi waniamini najua na natambua kilichonileta na mpira ni kazi yangu,”


WACHEZAJI SIMBA

Japokuwa hajapata nafasi ya kuwatizama wapinzani wao Simba, Fiston anakiri kuna baadhi ya wachezaji ambao anayasikia majina yao licha ya kuwa bado hajawaona.

“Najua Simba wanawachezaji wazuri nasikia wanatajwa Meddie Kagere, Bernard Morrison na mimi natamani kukutana nao ili niweze kuwaona ila kwa sasa akini kwa saukiniuliza nani mzuri nitakuwa muongo sijawahi kuchukua muda kutizama Simba inacheza,”anasema.

“Siunajua mimi nilikuwa Ligi nyingine na sikuwa na mpango wa kuja Tanzania, nilikuwa Misri hapo nilikuwa natizama Zamalek na timu za huko,”anasema na kuongeza kuwa, kwa kuwa yuko katika Ligi Tanzania atawafuatilia.


NAFASI YA WARUNDI YANGA

“Ni kitu kizuri sana na nafurahi sana, kuona Kocha wangu Kaze na hata wa makipa wametoka kwetu na hata Saido kwa hiyo nimekuja Yanga nikiwa mwenyeji,”

“Kaze ananifahamu sana ananijua vilivyo hata mimi namjua vilivyo tutaisaidia sana timu yetu ya wananchi wawe na imani na sisi,”anasema

Anasema warundi waliopita katika timu hiyo kama Amisi Tambwe na wengineo wamepeperusha vyema bendera ya Burundi hivyo hata wao hawatawaangusha.


AMCHAMBUA SAIDO

Fiston anaamini endapo Kocha Mkuu wa Klabu hiyoKaze akimpa nafasi ya kucheza na Saido atafanya makubwa zaidi.

“Ikitokea bahati mimi kuanza kipindi cha kwanza na Saido tutafanya vizuri sana kwanza, sio mchoyo anauwezo wa kudribo na kutoa pasi,kwani ni mtu wa kutoa pasi nzuri vile vile ana uwezo mkubwa wa kufunga na anajua nini anakifanya awapo katika eneo lake.

“Nategemea kila game nafasi mbili lazima nizipate kutoka kwake nyingine nasubiri kutoka kwa wengine”anasema Fiston.

Anayasema hayo kwa uhakika kabisa na kujiamini kutokana na namna ambavyo yeye anacheza na anajua namna ambavyo Saido anavyocheza.

“Nikiwa na yeye tutacheza vizuri sana kwa sababu tunajuana uwezo wa kutoa pasi na kufunga, Saido ni mtoa pasi mzuri namjua vizuri sana tofauti na wengine”.

Anasisitiza kwa kuwataka mashabiki wa Yanga kumwamini juu ya kilichomleta ndani ya timu yao hivyo wasiwe na wasiwasi nae kwa kuwa anatambua ana deni kubwa dhidi yao.


ALIWANIWA KITAMBO

Simba na Yanga zilianza harakati za kusaka saini ya nyota huyu mwaka 2013 katika michuano ya Challenji iliyofanyika Nchini Kenya huku Klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ikawazidi kete na kusajili Sh. Milioni 500 kutoka klabu ya Sofapaka ya Kenya.

Yanga imeweza kutimiza ndoto yake ya kumpata nyota huyu na kuwapiku Simba ambao walishindwa kumnasa. Mbali na Saido, Fiston na Kaze , Yanga ina Mrundi mwingine ambaye ni Kocha wa Makipa, Vladmin Niyonkuru ambaye aliwahi kuidakia Azam miaka ya nyuma na timu yake ya Taifa kwa mafanikio.

Advertisement