Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MCHANJA: Bondia anayetembea na rekodi ya peke yake

Mchanja Pict

Muktasari:

  • Mchanja anayeshikilia mkanda wa ubingwa wa World Boxing Organization Global, amekuwa bondia wa kwanza kutoka Tanzania kushinda mkanda huo akiwa ndani ya ardhi ya Tanzania, rekodi hiyo itaishi milele na haifutiki kwani kabla yake hakuna aliyewahi kufanya hivyo na ikitokea mwingine amefanya itakuwa ni baada ya yeye.

YOHANA Mchanja ni mmoja kati ya mabondia wenye rekodi kubwa katika mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini anayetokea Jiji la Tanga.

Mchanja anayeshikilia mkanda wa ubingwa wa World Boxing Organization Global, amekuwa bondia wa kwanza kutoka Tanzania kushinda mkanda huo akiwa ndani ya ardhi ya Tanzania, rekodi hiyo itaishi milele na haifutiki kwani kabla yake hakuna aliyewahi kufanya hivyo na ikitokea mwingine amefanya itakuwa ni baada ya yeye.

Bondia huyo maarufu kwa jina la Computer kama anavyotambulika na mashabiki wengi wa ngumi, ameshinda mkanda huo wiki iliyopita kwa kumtandika kwa pointi mpinzani wake Miel Farjado kutoka Ufilipino katika pambano la raundi 12 lililofanyika Ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar likipewa jina la Knockout ya Mama ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.

Rekodi zinaonyesha kwamba, Mchanja aliyeanza ngumi mwaka 2016, tayari amecheza mapambano 25 sawa na raundi 133, akishinda 18 yakiwemo 13 kwa KO ikiwa ni asilimia 72, huku akipoteza mara sita na sare moja, hajawahi kupigwa kwa KO. Katika uzito wa fly, Mchanja anashika nafasi ya 68 duniani kati ya mabondia 790 wakati kwa Tanzania ni namba moja kwa mabondia 46 wa uzito huo.

MCH 05

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalum na bondia huyo ambaye amefichua mambo mengi mazito ikiwemo alichoambiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya ushindi wa pambano lake wakati alipoitwa kwenda kukabidhiwa zawadi ya ushindi wa Knockout ya Mama, shilingi milioni tano.

Bondia huyo ameanza kwa kueleza namna alivyojiunga na Mafia Boxing Primotion ambayo kwa sasa imekuwa ikisimamia mapambano yake kupitia Mafia Boxing Gym Academy.

Mchanja anasema wazi kwamba hawezi kujiona yeye bora kuliko wengine hadi kuwa sehemu ya Mafia isipokuwa ni mipango ya Mungu mwenyewe ambaye ameshaona kuwa ameshajitoa kutaka kutafuta riziki kupitia michezo.

"Kiukweli sioni sababu ya kutaka kujiona kwamba Mchanja ni bora kuzidi wengine isipokuwa Mungu mwenyewe ameona nimejitoa kusaka riziki yangu kupitia mchezo huu wa ngumi na ndiyo tumekuwa makini nao kiasi cha kupelekea watu wengine kutokea kutupa sapoti ya kutosha tuweze kufikia ndoto zetu.

"Unajua kutokana na hivyo hata watu wengine wanaotuona ambao wanatafuta sehemu ya kuwekeza pesa zao inakuwa rahisi kutusaidia kutokana na umakini wanaouona kutoka kwetu.


MCH 04

SWALI: Umecheza mapambano mengi chini ya promota wa Tanga, Ally Mwazoa kabla ya kujiunga Mafia, nini kilitokea kati yako na Mwazoa?

JIBU: "Mwazoa yule ni baba yetu na mlezi wetu wa mchezo wa ngumi Tanga, ametusogeza na ametutoa mbali sana, kukosa yeye asingekuwepo Yohana Mchanja, Salim Mtango wala Hassan Mwakinyo kwa hiyo ni baba yetu aliyetulea kwenye ngumi, alipotufikisha, ikabidi atuachie ili wengine waendeleze kijiti.

"Tunamshukuru sana promota wetu Mwazoa, ametutoa mbali, tulikuwa hatujuani na hatujulikani lakini amefanya tumejulikana.


MCH 03

SWALI: Huko kote hukujulikana hadi ulivyocheza na Haidari Mchanjo, unadhani kwa nini?

JIBU: "Ni kweli pambano la Yohana Mchanja na Haidari Mchanjo ndiyo watu wakaja kunijua lakini hadi nacheza na Mchanjo nilikuwa nishasafiri sana mapambano ya nje na hata nilivyocheza na Mchanjo wengi walishangaa kwa sababu hawakuamini kwamba mimi Mtanzania, wakati nahojiwa nilisikia watu wakisema jamaa anaongea kiswahili kumbe.

"Hii ilitokana na kwamba wao walifahamu mimi siyo Mtanzania ingawa kwa sasa sina cha kuwaambia Watanzania na mashabiki zangu ila nimpongeze Shekhe Mwazoa kwa kututoa kwenye macho ya watu na mpaka sasa nitoe pongezi kubwa kwa menejimenti yangu ya Mafia kunipa nafasi ya kuwania mkanda wa ubingwa wa Global.


MCH 02

SWALI: Ukiondoa pambano lako na Mchanjo sehemu kubwa ya nchi imekufahamu baada ya pambano la juzi, unadhani kwa nini?

JIBU: "Siyo kwamba nilikuwa nimewekeza sana ila mapambano yanavyokuja ndiyo nilivyokuwa nayapokea, mapambano yote niliyocheza ni magumu sana tofauti na pambano la juzi hata Tanga naongoza kucheza mapambano mengi ya nje ambayo nilimaliza raundi zote tena katika nchi ngumu kama Filipino, Ghana na Urusi.

"Lakini nimshukuru Mungu kwamba pambano la juzi limefanya Watanzania wengi waweze kujua ubora wangu ingawa binfsi najua mimi bora zaidi kwa sababu nimekutana na viama vingi vigumu ambavyo nchi yangu haijashuhudia imeshuhudia pambano la juzi.


SWALI: Je, ni kweli ukimya pia umekufanya usijulikane tofauti na mabondia wengine ambao kelele zao zimewafanya watambulike?

JIBU: "Unajua sisi kazi zetu siyo kuongea ni kupigana, wanaongea huwa ni madalali maana wakati mwingine maneno yanazidi uwezo, nimejifunza kwa wale ambao wanaongea sana halafu mwisho wa siku hakuna kitu yaani hawafanyi kuendana na maneno yao ila mimi naongea na mikono yangu ndani ya ulingo.


MCH 01

SWALI: Wakati unapigana na Mchanjo alikuzidi wapi?

JIBU: "Binafsi naona alinizidi nguvu pekee kwa sababu mimi ndiye nilikuwa nimemfuata kwenye uzito wake, nilikuwa naona akicheza anashinda na wale waliokuwa wakicheza nao hawakuwa wakifanya nilichokuwa nakiona ndiyo sababu kubwa ya mimi kupigana na yeye.

"Unajua mara zote mbili nilicheza naye kwa kufuata kilo zake 55 kwa sababu nilitaka kumuonyesha kwamba aliokuwa akicheza nao kuna jambo walikuwa hawalifanyi dhidi yake na nilifanikiwa kumuonyesha kile ambacho nilikuwa nakitaka.


SWALI: Kwa nini unaitwa Computer?

JIBU: "Hili jina lilitokana na mtangazaji mmoja wa TK FM ya Tanga, alikuwa na kawaida ya kuja kufanya mazoezi ndiyo yeye alianza kuniita kwa jina hilo kutokana na spidi ya mikono yangu lakini siyo jina hilo tu kwa sababu Urusi kule mara nyingi huwa wananiita Bruce Lee wa Tanzania.

"Binafsi nimeshazoea kwa sababu hata kwenye soka wachezaji wanapewa majina mengi ya utani na nikawaida kabisa.


SWALI: Kitu gani kilikufanya uchague ngumi?

JIBU: "Kwanza nataka nikwambie tu kwamba mimi katika familia yetu hakuna hata mtu mmoja anayecheza mchezo wa ngumi, nipo mimi peke yangu ila wengi wapo kwenye mambo ya soka.

"Kitu ambacho kimenivuta hadi kuwa bondia ni wakati ule wa kina Inspekta Seba na Jay Plus ndiyo walivutia kupitia muvi zao za mapigano lakini yupo bondia mkongwe, Allan Kamote pamoja na Mfaume Mfaume, wamechangia asilimia kubwa kuupenda mchezo.


SWALI: Uliwahi kufikiria kuwa bingwa wa dunia tena kwa pambano la kucheza ndani ya nchi?

JIBU: "Zamani katika mipango yangu na ndoto kubwa ambayo ilikuwepo ni kwamba nilikuwa nacheza ngumi kwa kuamini nataka kubadilisha maisha yangu pekee kutumia kipaji changu.

"Kuhusu ubingwa wa dunia, nilikuwa nawaza kwa sababu tunawaona wenzetu duniani wanavyofanikiwa maana mara nyingi tunafanya vitu kwa kutamani walivyofanya wengine, hii ni ndoto iliyokuwa kichwani hatimaye ikatimia.


SWALI: Kitu gani alikwambia waziri mkuu wakati anakukabidhi pesa za KO ya Mama?

JIBU: "Kiukweli sikutegemea kabisa kama kuna siku nitapiga picha na kiongozi mkubwa katika serikali ya nchi yetu kama Waziri Mkuu, sijategemea kabisa kuona itatokea hivyo zaidi ya viongozi wengine wa chini yake.

"Lakini nashukuru nimekutana na Waziri Mkuu na wakati ananipa zawadi ya KO ya Mama alinipongeza kwa kuiheshimisha nchi maneno ambayo yamekuwa faraja kubwa moyo mwangu," anasema Mchanja.